Utata wagubika muswada wa kura ya maoni
Na Fidelis Butahe na Habel Chidawali,Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba29 2013 saa 9:16 AM
Posted Jumanne,Oktoba29 2013 saa 9:16 AM
KWA UFUPI
- Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, aliiambia Mwananchi kuwa hawajaupitia muswada huo baada ya kufanyiwa marekebisho.
Dar es Salaam/Dodoma. Kuna uwezekano wa kuzuka mvutano mkali kwenye Mkutano wa 13 wa Bunge unaoanza leo mjini Dodoma kutokana na utata wa maandalizi ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni unaotakiwa kuwasilishwa.
Mijadala ya miswada miwili, ambayo inahusiana na mchakato wa kupata Katiba Mpya ndiyo inatazamiwa kuwasha moto katika Bunge hili.
Miswada inayosubiriwa kwa hamu ni pamoja na ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na ule wa Sheria ya Kura ya Maoni.
Maandalizi ya Muswada wa Kura ya Maoni huenda yakazua zogo bungeni kutokana na kuwapo malalamiko kuwa upande wa Zanzibar haukushirikishwa kikamilifu.
Pia inasemekana Kamati ya Haki, Sheria na Utawala haijakaa kupitia muswada huo na pia haijakutana na wadau mbalimbali.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, aliiambia Mwananchi kuwa hawajaupitia muswada huo baada ya kufanyiwa marekebisho.
Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi alisema muswada huo uliondolewa kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ambayo alieleza kuwa tayari yameshafanyika.
“Muswada sio kama uliondolewa bila kujadiliwa, ulijadiliwa na baadaye tulikubaliana ufanyiwe marekebisho ambayo tayari yameshafanyika. Wiki hii tutauwasilisha tena mbele ya Kamati,” alisema Lukuvi.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana kueleza kama Kamati hiyo ilikutana na upande wa Zanzibar alisema, “Siwezi kuzungumzia suala la miswada na gazeti lenu (Mwananchi), sitaki kueleza lolote, kama unataka maelezo mtafute Katibu wa Bunge au Spika,” alisema na kukata simu.
Muswada huo unaeleza kuwa kura ya maoni inatakiwa kupigwa Tanzania Bara na Zanzibar, jambo ambalo lilipingwa na upande wa Zanzibar kwa madai kuwa nao wana sheria kama hiyo na kwamba masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano
Muswada wa Sheria ya Marekebisho
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa wa Bunge, Deogratias Egidio alisema kuwa pamoja na miswada hiyo miwili pia kutakuwa na miswada zaidi