Header Ads

SITTA AMPA TAARIFA YA MWENENDO WA BUNGE MAALUM DKT. SHEIN

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Samuel Sitta akimpatia taarifa juu ya mwenendo wa Bunge Maalum la katiba na ulipofikia, Rais Wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, alipomtembelea nyumbani Ikulu ya Migombani Zanzibar. Mhe Sitta alikuwa Visiwani Zanzibar kwa lengo la kuonana na Mhe. Shein kumpatia taarifa kamili ya shughuli za Bunge Maalum la Katiba. Picha na Owen Mwandumbya - Bunge Maalum

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Samuel Sitta jana amefanya ziara ya kikazi Visiwani Zanzibar na kutana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, kumpatia taarifa juu ya mwenendo wa Bunge Maalum la katiba na hatua lilipofikia. Mhe. Sitta amekutana na  Dkt. Shein katika Ikulu Ndogo Ya Migombani, Zanzibar ambapo aliweza kumpatia picha halisi ya maendeleo ya Mkutano wa Bunge Maalum la Katiba unaoendelea Mjini Dodoma, Rais wa Zanzibra.

Akizungumzia mchakato wa Utungaji Kanuni, Mhe. Sitta amemwambia Dkt. Shein jinsi hatua hiyo ilivyokuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na jinsi Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo Mhe. Pandu Ameri Kificho alivyoweza kufanikisha zoezi hilo kwa kuunda kamati ya watu 20 kuongoza utungaji wa Kanuni hizo ikiongozwa na Mheshimiwa Profesa Costa Ricky Mahalu, ambapo alisema matarajio utungaji wa Kanuni ulikadiriwa kukamilika ndani ya muda wa siku tatu, hata hivyo, kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe na haja ya kuwa na Kanuni makini kwa ajili ya kuendesha Bunge, muda huo haukutosha na badala yake Bunge lilichukuwa wiki tatu kukamilisha kazi ya kutunga Kanuni hizo.

Mhe. Sitta alisema baadhi ya mambo yaliyojitokeza na kuchukua muda mwingi wa mjadala wakati wa Kutunga kanuni ni suala la mfumo wa upigaji kura kwenye vifungu vya Rasimu na Rasimu yenyewe.

“Wajumbe walijadiliana na kutofautiana kwa hoja kuhusu mfumo upi wa upigaji kura utumike kati ya ule wa kura ya wazi na wa kura ya siri. Katika hatua hiyo, wajumbe walikubaliana kupitisha Azimio la Kanuni huku suala la mfumo wa upigaji kura likiachwa katika hatua ya maridhiano ambapo Azimio la upitishwaji wa Kanuni za Bunge Maalum lilifanyika tarehe 11/3/2014” Alisema Mhe. Sitta
Kuhusu kuundwa kwa Kamati za Bunge Maalum, Mhe. Sitta amemweleza Dkt. Shein kuwa  kazi yake ya kwanza kama Mwenyekiti baada ya kuapishwa ilikuwa ni kufanya uteuzi wa wajumbe kwenye kamati kumi na mbili kwa ajili ya kupitia sura za rasimu na kuwasilisha ripoti, ambapo Kwa wastani kila kamati ina wajumbe wasiopungua hamsini na wawili (52) ukiacha Kamati Maalum za uandishi na ile ya Kanuni, ambapo pia ipo Kamati ya Maridhiano.

“Nilipata fursa pia ya kuteuwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ambayo inaundwa na wenyeviti wa kamati za Bunge Maalum., ikiwa ni pamoja na wajumbe wengine watano kwa mujibu wa Kanuni ambao wanaingia katika kamati ya uongozi, ambapo hivi sasa Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wapo 21”. Alisema Sitta.

Akifafanua kuhusu kazi za Kamati, Mhe. Sitta alisema Kamati kumi na mbili za Bunge Maalum, zilipewa jukumu la kupitia sura mbili mbili za rasimu ya Katiba yenye sura 17 na kuwasilisha ripoti zake Bungeni ili zijadiliwe. Kwa kuanzia, Kamati ya Uongozi, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kupanga ratiba ya shughuli za Bunge Maalum, iliagiza kamati zianze kupitia sura ya kwanza na sura ya sita kwa kuwa sura hizo ndiyo roho ya Rasimu ya Katiba, ambapo Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum, kamati zimeruhusiwa kujumuisha katika taarifa zao maoni yaliyoafikiwa na wajumbe walio wengi pamoja na maoni ya wajumbe walio wachache.

Akielezea kuhusu sura hizo, Mhe. Sitta alimweleza Dkt. Shein kuwa wakati wa kupitia sura ya 1 na sura ya 6 kwenye kamati, baadhi ya kamati zilifikia maamuzi na kupitisha ibara za sura hizo kwa kura za theluthi mbili za wajumbe kutoka upande wa Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka upande wa Zanzibar na baadhi ya kamati hazikupata idadi hiyo.

Hata hivyo, kwa kuwa kamati hazifanyi maamuzi ya mwisho ya kupitisha sura hizo, zilitakiwa kuwasilisha ripoti zao kwenye Bunge kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye maamuzi yafanyike. Kamati zote ziliwasilisha taarifa zao na mjadala wa sura hizo mbili ulianza tarehe 8/4/2014 na unaendelea hadi sasa.


Pamoja na hayo yote, Sitta alimweleza Shein kuwa mjadala wa Ripoti za Kamati ulitakiwa ufanyike kwa muda wa siku tatu. Hata hivyo, kutokana na maombi ya wajumbe wengi waliotaka kuchangia (433) na kutokana na umuhimu wa sura zilizowasilishwa kwenye ripoti za kamati, Kamati ya Uongozi iliamua kutoa fursa pana ya mjadala, kwa kuongeza muda wa siku zaidi, ili wajumbe wengi wapate fursa ya kuchangia, ambapo wajumbe wengi walitoa michango yao na mijadala ilikuwa mikali li cha ya kuwa baadhi ya wajumbe walitumia lugha kali na hata nyingine zisizofaa na Kutokana na hisia kali zilizotawala ilikuwa vigumu kudhibiti kikamilifu hali hiyo ukumbini.

Kuhusu Madai ya Kundi la UKAWA kususia Bunge Maalum, Mhe. Sitta alisema wakati Bunge likiendelea na mjadala tarehe 16/4/2014, kundi la “UKAWA” linaloundwa na baadhi ya wabunge na wawakilishi kutoka CUF, CHADEMA na NCCR – Mageuzi liliamuwa kutoka Bungeni kwa madai mbali mbali na kuamua kususia Bunge.

“Pamoja na kutoka nje siku hiyo, wajumbe hawa hawakutoa taarifa zozote katika Ofisi yangu kama ususaji huo ni kwa muda tu au ndiyo basi hawataendelea tena na mchakato huo”. Alisema Mhe. Sitta

Sitta anasema Juhudi za kukutana na viongozi wa “UKAWA” hazijafanikiwa kwa kuwa viongozi wa kundi hilo wameendelea kukataa kuonana na nae, licha ya kuwa jitihada zinaendelea kuwasiliana na kundi hilo kujua msingi wa madai yao ili yaweze kushughulikiwa kwa taratibu za kibunge.

“Moja ya jambo linalodaiwa kusababisha wajumbe hao kutoka ni madai ya kauli za kibaguzi zinazodaiwa kutolewa nje ya Bunge na mjumbe mmoja ambaye pia ni kiongozi wa Serikali. Kutokana madai hayo kuwa mazito, Nilitumia busara ya kumtafuta mjumbe huyo ili aje atoe ufafanuzi wa madai hayo Bungeni, na mjumbe huyo alifanya hivyo. Madai mengine ni kauli za matusi na ubaguzi walizodai ziliwalenga wao”.  Alisema Sitta.

Madhumuni ya ziara ya Mhe. Sitta kukutana na Rais wa Zanzibar ilikuwa ni kumpatia taarifa kuhusu mwenendo wa Bunge Maalum ulivyoanza na hadi hatua hii ulipofikia.
Powered by Blogger.