Header Ads

Mbunge aambulia mshahara 50,000/- kwa mwezi

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaWAKATI baadhi ya watu wakiamini wabunge hulipwa zaidi ya sh milioni 10 kwa mwezi, mmoja wa wabunge wa Bunge la Muungano, amejikuta akitoka na mshahara wa sh 50,000 kwa mwezi, Tanzania Daima limebaini.

Mbunge huyo ambaye jina limehifadhiwa, amejikuta akiambulia kiasi hicho cha fedha kutokana na makato makubwa ya marejesho ya mkopo wa Bunge wa zaidi ya sh milioni 300 aliouchukua baada ya kuingia bungeni.
Mbali ya mbunge huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni, inaelezwa kuna wabunge wengine wengi wanakabiliwa na tatizo hilo la kuambulia mishahara kiduchu kutokana na makato ya mikopo na kodi.
Akizungumza na gazeti hili, mbunge huyo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye alisisitiza jina lake lihifadhiwe, alisema yeye pamoja na wabunge wengine wengi, wanakabiliwa na tatizo la makato makubwa ya madeni waliyokopa na watakuwa wakilipwa kiasi hicho kwa muda wote wa Bunge.
“Karatasi yangu ya mshahara kila mwezi inaonyesha napata sh 50,000 tu na huo ndio ukweli maana nilikopa nikajengea nyumba zangu tano za nguvu, najua hata nikikosa ubunge mwakani, maisha yangu yataenda vizuri, lakini wapo waliokopa kwenda kutekeleza ahadi walizozitoa majimboni, hao wasiporudi bungeni wamekwisha,” alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo ambaye ni mmoja wa wapiga vijembe wakubwa dhidi ya wenzao wa upinzani, alisema maisha yake ya ubunge kwa kiasi kikubwa yanategemea zaidi posho za vikao, ambavyo kwa mwaka huu vimekuwa mfululizo, vikiwemo vikao vya Bunge la Katiba.
Alisema anaomba ratiba ya vikao vya Bunge la Muungano linarotarajia kuanza tena Julai baada ya Bunge la Bajeti linaloendelea kumalizika, isibadilike ili aendelee kupata posho ya sh 300,000 kila siku.
Bunge la Julai
Hata hivyo, matumaini ya wabunge kuunganisha vikao vya Bunge la Bajeti linalomaliza vikao vyake Julai mosi na jingine lililotarajia kufanyika Julai, yameanza kufifia.
Awali kulikuwa na taarifa zilisema kuwa baada ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti linaloendelea, wabunge hao wangepumzika kwa wiki moja kisha kuanza tena vikao vya kamati na kurejea tena bungeni Julai.
Kufifia kwa matumaini hayo kunatokana na taarifa ilizozipata gazeti hili kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Uongozi katika kikao walichoketi wiki iliyopita, hawakufikia muafaka juu ya pendekezo la kuwepo kwa mkutano mwingine wa 16 wa Bunge ifikapo Julai.
Tanzania Daima, limedokezwa kuwa baadhi ya wajumbe walisema ratiba hiyo itawafanya wachoke zaidi kwani kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti walikuwa wakishiriki kwenye Bunge la Katiba ambalo liliahirishwa mwishoni mwa mwezi wa nne.
Baada ya kuahirishwa kwa Bunge la Katiba, wabunge walipumzika kwa takriban wiki moja na kuanza vikao vya kamati za Bunge na baadaye kuingia kwenye Bunge la Bajeti ambalo wakimaliza watajiandaa kushiriki lile la katiba litakaloanza Agosti 5.
Awali baada ya taarifa za kuwepo kwa Bunge jingine Julai kabla ya lile la katiba, baadhi ya wabunge walionekana kuzifurahia wakidai litawasaidia kupata posho zitakazopunguza ukali wa maisha.
Baadhi ya wabunge wamekwa na kilio cha mara kwa mara kuwa fedha wanazolipwa haziwatoshi kutokana na mikopo mingi waliyonayo na upandaji wa gharama za maisha.
Akizungumza na Tanzania Daima, Kaimu Katibu wa Bunge John Joel, alisema hadi sasa bado Bunge halijaamua uwepo wa Bunge la Julai kama baadhi ya watu wanavyotoa taarifa.
Alisema kama jambo hilo litaridhiwa na vikao husika Bunge litauarifu umma.
Bunge la Julai litakuwa kwa ajili ya kujadili miswada mbalimbali ya sheria iliyowasilishwa bungeni, ambayo haitaweza kujadiliwa katika Bunge la Bajeti.
Itakumbukwa kuwa Bunge la Muungano lilikutana Desemba mwaka jana, badala ya Januari kama ilivyo kawaida kupisha ratiba ya Bunge la Katiba.
Baada ya Desemba, wabunge walipumzika kwa mwezi mmoja na kurudi tena bungeni Februari kwa ajili ya Bunge la Katiba ambalo lilikaa kwa siku 67 hadi Aprili ambapo walipumzika kwa wiki moja na kurudi kwenye Bunge la Bajeti Mei 6, mwaka huu.
Powered by Blogger.