KADA WA CHADEMA APINGA WANAOTAKA UDIWANI NA UBUNGE KUWA NA ELIMU INAYOANZIA KIDATO CHA NNE, ASEMA KIFUNGU HICHO KIKIFUTWA KITAWANUFAISHA BAADHI YA WABUNGE WA CCM
ABOU MAJEKI |
KADA
maarufu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa mjini Iringa, Abou
Changawa amekiri kukoseshwa usingizi na pendekezo katika rasimu ya katiba Mpya linalotaka
mgombea wa udiwani na ubunge angalau awe na elimu ya kidato cha nne.
Mbali
na kuwa na elimu chini ya iliyopendekezwa katika rasimu hiyo, Changawa, maarufu
kwa jina la Majeki ni mmoja kati ya wanasiasa wachache walioko kambi ya
upinzani mjini Iringa wanaosifika kwa kujenga hoja.
“Naomba
Mungu kila uchao, wabunge wa bunge hilo la Katiba wakikatae kifungu kinchotaka
wagombea wenye elimu chini ya kidato cha nne wasigombee nafasi hizo za
uwakilishi wa wananchi,” alisema.
Alisema
kama kifungu hicho kitapita kitafutilia mbali ndoto zake za muda mrefu za kuwa
diwani na baadaye Meya wa Manispaa ya Iringa.
“Katika
siku zote za maisha yangu ya kisiasa nimekuwa nikisema, halmashauri ya manispaa
ya Iringa inahitaji diwani mwenye uwezo wa hoja kama mimi ili awe meya,”
alisema.
Aliwaomba
viongozi na wabunge wa chama chake cha Chadema kukikataa kifungu hicho kwakuwa
kitawanyima haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa watu wenye elimu kama
yake.
“Tunataka
Katiba Mpya lakini kipengele hicho kinataka kutopoteza kwenye siasa za
uwakilishi tusio na elimu ya kidato cha nne,” alisema.
Majeki
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Soka ya Lipuli ya mjini Iringa aliwaomba
watanzania kukikataa kufungu hicho kama kitapitishwa na bunge hilo maalumu la
Katiba.
Kama
kifungu hicho kitakataliwa imeelezwa na wadau wa siasa mkoani hapa kwamba kitaleta
faraja kubwa kwa baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) wenye elimu hiyo.
Mmoja
wa wabunge hao ni Deo Sanga maarufu kwa jina la Jah People; mbunge huyu wa
Njombe Kaskazini alichaguliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa huo muhimu mwaka
2010.
Wakati
wa kampeni zake za kutafuta ridhaa ya wana CCM kumchagua katika kura zake za
maoni ili awe mbunge wao, Jah People alitumia wasifu wake wa elimu ya msingi kujinadi.
Katika
moja ya mikutano ya kampeni zake iliyofanyika mwaka 2010 katika kata ya
Makambako yalipo makazi yake, Jah People alijinadi kwamba yeye ni msomi mwenye ELIMU YA JUU YA DARASA LA SABA na ndio
maana anamiliki mali nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni
yake kubwa ya usafirishaji ya Jah People.
Elimu
yake hiyo iliibua hoja katika uwanja wa siasa wa jimbo hilo kwa aliyekuwa
Mgombea ubunge kupitia Chadema, Alatanga Nyagawa kuahidi kumfungulia mashitaka Jah
People kwa madai kwamba alishindwa kumaliza elimu ya msingi ambayo kwa mujibu
wa sheria ya nchi ni ya lazima.
“Kitaaluma
mimi ni mwanasheria, na katika hili sina mzaha, nitampeleka Jah People Mahakamani
kwasababu alikimbia elimu ya msingi ambayo ni ya lazima na kwa hilo amevunja
sheria,” Nyagawa alisema mwaka 2010 wakati Chadema kikifanya uzinduzi wa
kampeni za ubunge jimbo la Iringa Mjini katika uwanja wa Mwembetogwa.
Alisema
kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani ambapo elimu ya msingi imefanywa kuwa ya
lazima, na wale wanaoikosa wametengenezewa utaratibu mwingine wa kuipata,
atamfikisha mahakamani ili athibitishe kiwango chake cha elimu na hatimaye
kulazimishwa kujiunga na Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (Memkwa).
Hata
hivyo Nyagawa hakutekeleza ahadi hiyo na mpaka sasa Jah People ni mbunge wa
jimbo hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe.
Wasifu
wa mbunge huyo uliopo katika mtandao wa bunge unaonesha kwamba alizaliwa
Januari 1, 1965 na kuanza elimu yake ya msingi mwaka 1970 katika shule ya
Ikwega iliyopo wilayani Mufindi mkoani Iringa; hata hivyo wasifu huo hauoneshi
mwaka ambao mbunge huyo alimaliza elimu hiyo ya msingi.
Bila
shaka kukataliwa kwa kifungu kinachotaka wagombea udiwani na ubunge wawe na
elimu ya kidato cha nne kutakuwa na manufaa zaidi kwa mtu kama Jah People wa
CCM zaidi ya manufaa ya Majeki ambaye hajui raha ya kuchaguliwa.