KATIBU MWENEZI WA CHADEMA JIJI LA MBEYA AACHIA NGAZI.
Aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wilaya ya Mbeya,Bwa.Lucas Mwampiki.
======= ====== =======
SIKU
mbili baada ya aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Jiji la Mbeya Lucas
Mwampiki kutangaza kujiuzulu wadhifa wake, chama hicho kimedai kuwa
kilishamvua nafasi hiyo kabla hajatangaza kujiuzulu kutokana na
kuvujisha siri za chama kwa upinzani.
Mwampiki
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwakibete alitangaza kujiuzulu nafasi
ya Katibu Mwenezi kwa madai kuwa amekuwa akitengwa na baadhi ya viongozi
wa chama katika shughuli mbalimbali za chama kwa nafasi yake kama
mjumbe.
Akitangaza
uamuzi wa chama hicho dhidi ya Mwampiki, Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya
ya Mbeya mjini John Mwambigija alisema kuwa kikao cha kumvua uongozi
Katibu Mwenezi huyo kiliketi April 14 baada ya kujiridhisha mwenendo wa
utendaji wake na yeye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo April 16.
Alisema
kuwa kufuatia hali hiyo uongozi wa chama wilaya kwa kuhusisha vikao
halali vya chama umeridhia kumuengua katika nafasi yake ikiwa ni pamoja
na kumzuia kutojihusisha na shughuli zozote za chama.
Mwambigija alisema kuwa kiongozi huyo
wa juu wa chama alikiuka vifungu vya katiba ya chama kwa kusambaza
taarifa za majungu na kutokuwa mkweli na muwazi ikiwa ni pamoja na
kujihusisha na upotoshaji juu ya maamuzi halali ya chama.
‘’Tumeamua
kwa kauli moja kumsimamisha shughuli zote za chama kwa mwaka
mmoja,ataendelea na Udiwani wake, hatakiwi kufanya chochote
kinachohusiana na chama chetu,akiendelea tutachukua uamuzi wa
kumnyang’anya kadi na kumvua uanachama,’’alisema Mwambigija.
Alifafanua
kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha avuliwe wadhifa wake ni pamoja
na kuvujisha siri za chama kwa wapinzani ikiwa ni pamoja na kutotoa
ushirikiano katika harakati za chama za sasa za ‘Chadema ni Msingi’ na
kwamba uamuzi waliouchukua uko katika sheria zinazolindwa na Katiba ya
chama.
Alisema
kuwa kabla ya kuchukua uamuzi huo chama kilimuita kiongozi huyo katika
vikao mara nne ambapo alishindwa kuhudhuria hivyo uamuzi waliouchukua
una baraka za vikao halali vya chama na kuwa hata hivyo anayo nafasi ya
kukata rufaa kwa ngazi za juu iwapo ataona kuwa hajatendewa haki dhidi
ya uamuzi huo.
Kwa
upande wake Katibu Mwenezi aliyejiuzulu Mwampiki alisema kuwa aliamua
kujiuzulu baada ya kuona hapewi ushirikiano na viongozi wenzake na kuwa
mara nyingi alipokuwa akihoji mambo ya msingi ya kukiendeleza chama
amekuwa akinyooshewa kidole kama msaliti.
‘’Nimeamua
kujiuzulu mwenyewe bila kushinikizwa na mtu, kutokana na afya ya chama,
kwa mujibu wa Katiba ya chama ya mwaka 2006 kifungu 6.3.4(a) hiki
kinaainisha ukomo wa uongozi, nimetumikia chama kwa kila hali hadi
rasilimali fedha, nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu,’’alisema
Mwampiki.
Aidha alisema kuwa hajawahi kuitwa na viongozi wala
kuandikiwa barua yoyote inayomtaka kufika ofisini ambayo kulingana na
taratibu ilipaswa kumfikia ndani ya siku 14 na yeye kuweka saini yake
hivyo uamuzi wowote uliochukuliwa dhidi yake ulipaswa kuzingatia
taratibu hizo.
‘’Siwezi
kuchukuliwa hatua bila maandishi ambayo yanapaswa kunifikia ndani ya
siku 14, vinginevyo uamuzi wowote dhidi yangu mbali na kutamka kujiuzulu
kwangu, haujafuata taratibu za kisheria,’’alisema Mwampiki.