Header Ads

WACHAPWA VIBOKO KWA KUSHINDWA KULIPIA MAHAFALI

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida na kushangaza wanafunzi wa shule ya Sekondari Kivukoni katika halmashauri ya mji wa Geita Mkoani hapa wamepewa adhabu ya viboko wakilazimishwa kuchangia sherehe ya kuhitimu elimu ya Sekondari.
Wakizungumza na Tanzania Daima, wanafunzi hao ambao waliomba kuhifadhiwa majina yao kwa sababu ya usalama wao shuleni hapo walisema uongozi wa shule hiyo umetoa agizo la kila mwanafunzi kulipa shilingi elfu tano kila mmoja kwa ajili ya mahafali hayo.
Wanafuzi wanaosoma kidato cha kwanza hadi cha tatu walishangazwa pia wao kulazimishwa kuchangia sherehe hiyo kwa nguvu wakati ilipaswa kuwa hiari.
"Juzi sisi wanafunzi wa kidato cha tatu tuliitwa na walimu wale ambao tulikuwa hatujalipa tulichapwa viboko vitano kila mmoja tukiambiwa tumegoma kutoa mchango huo," alisema mwanafunzi mmoja na kuongeza.
"Sasa hivi kila mwalimu anapoingia darasani tunaitwa majina wale ambao hatujachanga tunapigwa viboko bila huruma tunawaaambia hatuna pesa tunaongezewa adhabu ya viboko vingine," alisema.
Pia  walisema pamoja na kuchapwa viboko walitakiwa kuandika barua za kujieleza  kisha kupelekwa kwa mkuu wa shule huku wakitishiwa kufukuzwa.
Alipotafutwa kuelezea juu ya tuhuma hizo kaimu mkuu wa shule hiyo ambaye alikataa kata kata kutaja jina lake alisema hajui suala hilo wala  kuwepo kwa mchango wa aina hiyo shuleni.
Alipoulizwa kuhusu wanafunzi kupewa adhabu wakikataa kutoa michango alikubali kwa kusema aliyetoa idhini hiyo ni mkuu wa shule.
Ofisa Elimu wa Halmashauri ya mji wa Geita, Cosmas Kibiti, alisema kisheria inatakiwa michango iwe imekubaliwa na vikao halali kisha kuwepo na muhtasari wa vikao tofauti na hapo ni kosa
Chanzo:Tanzania Daima
Powered by Blogger.