WANAFUNZI 17 WAJERUHIWA KWA RADI JIJINI MWANZA
WANAFUNZI 17 wa Shule ya Sekondari ya Kabuholo wilayani Ilemela jijini Mwanza, wamejeruhiwa na radi.
Tukio hilo limetokea jana asubuhi ambapo radi iliwapiga wanafunzi 15
wa kidato cha nne, mmoja wa kidato cha tatu na mwingine kidato cha
kwanza.
Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu wa mazingira wa shule hiyo, Humphrey
Massawe, alisema tukio hilo lilitokea wanafunzi hao wakiwa darasani
ambapo mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iilikuwa ikinyesha.
“Tulikuwa ofisini wakati mvua ikiendelea kunyesha walifika baadhi ya
wanafunzi wakasema wenzao wa kidato cha nne wamepigwa na
radi…nilipokwenda nikawakuta baadhi yao wakiwa wamepoteza fahamu huku
Joyce Juma (19), akiwa amelala chini na ameng’ata ulimi na shati lake
likiwa limeungua mgongoni,” alisema Massawe.
Muuguzi wa zamu katika katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou
toure, Aquilina Shai, alisema waliwapokea wanafunzi 17 kutoka sekondari
hiyo.
Aliwataja wanafunzi hao ni Jofrey Dioniz (19), Joyce Juma (19), Flora
Magesa (18), Lucy Jonas, John Bwire (17), Yohana Zabron, Mohamed Edwin,
Frank Cuthbert na Asimwe Joseph.
Wengine ni Aisha Juma, Lucy David, Hawa Musa, Faraja Richad, Anita Robert, Martha Zakaria na Neema Deus.
“Kati yao 14 miwongoni mwao waliruhusiwa baada ya kutibiwa huku
watatu Joyce, Neema na Dioniz wakiwa wamelazwa kutokana na hali zao kuwa
mbaya,” alisema Shai.
Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alisema bado hajapata taarifa kuhusiana na tukio hilo.