Huyu Ndiye Msanii Mwenye Elimu Ya Juu Kabisa "Masters" Asiyetaka Kazi
Kwa kawaida vijana wengi Afrika, hususan Tanzania wanapohitimu elimu ya juu, jambo ambalo hulifikiria ni kutafuta ajira.
Wengi
huanza kuchakaza viatu vyao wakipita ofisi moja baada ya nyingine
kuomba nafasi za kazi zilizotangazwa na mwishowe hujikuta wakiwa
wamefanya usaili zaidi ya ofisi 10 pasipo kuitwa kazini.
Hata
hivyo hii ni tofauti na msanii wa
Hip Hop kutoka Kundi la Weusi, Nickson
Simon maarufu kama Nikki wa II ambaye ana shahada ya Uzamili katika
maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDMS).
Nikki wa II
ambaye pia ni mshindi wa tuzo za muziki za Kilimanjaro 2014 KTMA kupitia
wimbo Bora wa Hip Hop “Nje ya Box”, aliowashirikisha G Nako na Joh
Makini wote kutoka Kundi la Weusi, anasema licha ya kwamba amehitimu
elimu ya juu na kupata alama kubwa, hayupo tayari kuajiriwa.
Rapa
huyu ambaye ni mdogo wa damu wa mwanamuziki John Simon maarufu kama Joh
Makini wiki hii ameachia wimbo wake mpya “Sitaki Kazi” wimbo ambao
umebeba maudhui makubwa yenye kutoa elimu kwa vijana wa rika na elimu za
aina zote.
Msanii huyu aliyeibukia katika fani mwaka 2008 na
wimbo wake “Good Boy” aliokuwa amemshirikisha Rama Dee, anasema hisia
alizonazo ndizo zilizomfanya atunge mistari ya wimbo huo, kutokana na
maisha halisi ya vijana wa sasa.
“Niliimba wimbo huu kutokana na
kuwaona vijana wengi wenye elimu ya juu wakihangaika kupita huku na kule
na vyeti vyao wakitafuta ajira, kwangu mimi naona ni utumwa kwa msomi
kutegemea kufanya kazi za watu wengine, badala ya kuibua cha kwako ili
utoe ajira kwa wengine,” anasema.
Hata hivyo anabainisha kuwa
namba ya vijana wanaohitimu stashahada, shahada ya kwanza na kuendelea
inazidi kuwa kubwa na ajira ni za kubahatisha.
“Ndani ya mistari
ya wimbo “Sitaki Kazi” kuna mistari inayoelezea namna kijana anavyoweza
kutatua tatizo la ajira kwa kubuni vitu mbalimbali ambavyo vitazalisha
pato na kuweza kuajiri maelfu ya vijana wanaohitimu mwaka hadi mwaka,”
anasema rapa huyo.
Anasema ingawa nchi haina utaratibu maalumu wa
kuwaandaa vijana pindi watakapomaliza elimu zao, kuna haja ya kutafuta
ufumbuzi wa tatizo hili kwa vijana husika.
“Tatizo kubwa katika
nchi yetu hakuna mtu au utaratibu ambao unawaandaa vijana, lakini sisi
wenyewe lazima tutambue kwamba hii ni karne ya kutengeneza ajira yetu
wenyewe, ndiyo maana nimeimba wimbo huu ili kubadilisha mtizamo na fikra
za vijana ambao wanategemea ajira, ni lazima jamii ibadilike,” alisema
Nikki wa II.
Nikki anasema katika usanii alionao anajivunia
kufanya kazi hiyo kwani ni kujiajiri inayomwingizia kipato kikubwa
ukilinganisha na ajira ya ofisini ambayo ingembana na asingeweza kupata
fedha ya ziada nje ya mshahara.
Anasema hiyo inamfanya avutiwe na
kazi yake kwani anaamini kwamba elimu inamsaidia kuiboresha kazi yake,
hivyo anaitumia kuongeza ujuzi katika muziki na kazi mbalimbali za
Kampuni ya Weusi.
“Kijana lazima ujiamini kwamba unaweza
kutengeneza ajira, watu ninaowapenda na maarufu walifanya kazi katika
jamii na kutoa ajira kwa vijana wangakuwaje iwapo Biliget angeajiriwa,
inakuwaje Bhakresa au Mohamed Dewji wangeajiriwa? Leo hii maelfu ya
Watanzania wasingekuwa na ajira,” anasema.
Anasema kiuna mambo
mengi aliyoyazungumzia katika wimbo huo ikiwamo ubunifu kwa
kuwahamasisha vijana wawe wabunifu ili kukuza nafasi za ajira na
kuongeza pato la taifa.
“Sitafuti kazi ila nataka nitafutwe na
watu wanaotafuta kazi’, haya ni moja ya mashairi yaliyopo katika wimbo
huu ambao niliimba nikiwa na nia ya kuwahamasisha vijana wawe wabunifu
ili elimu tulizozipata tuweze kuzitumia katika kukuza uchumi wa nchi na
kujiendeleza sisi na familia zetu,” anasema rapa huyo.
Nikki wa II
anatoa wito kwa vijana kujituma wao wenyewe kabla ya kufukuzwa kazi,
kwani wengi wao waliweza kufanya makubwa baada ya kufuzwa katika kazi za
kuajiriwa.
Anasema ni vyema vijana wakajituma wao wenyewe kwa
kufanya vile wanavyovipenda kuliko kufanya kazi wasizozipenda kwa
kutumikia mishahara.
“Wengi wanafanya kazi wasizozipenda kwa
kutumikia mishahara, mtu anafanya kazi ili apate mshahara na hii
inasababisha wengi kulipua kazi na wakati mwingine kutotekeleza majukumu
yao ya kikazi.”
“Iwapo mtu atafanya kazi anayoipenda au kujiajiri
hujikuta akifanya kazi mpaka usiku wa manane na hapo tayari anakuwa
ametengeneza pato kubwa kwake au kampuni yake kwani anafanya kitu chenye
masilahi kwake na siyo kwa kampuni fulani au mtu binafsi,” anasema
Nikki wa II.
Licha ya kutoa darasa hilo kwa wasomi nchini, rapa
huyo alirudi pia kwa watu wa uswahilini na wale wasio na elimu na
kuwataka kutokata tamaa na kuishia kuomba ajira kwa watu wengine kwani
na wao wana nafasi kubwa ya kujituma na kumiliki makampuni makubwa.
“Mimi
nimezaliwa uswahini huko Arusha, ninavyojua mimi watu wengi wa huko
hawana CV wala vyeti, ndani ya wimbo huo kuna mistari nimeimba kwa ajili
yao,” anasema.
Kuhusu Nikki wa II
Kijana huyu mzawa wa Daraja Mbili Arusha, alisoma Arusha Sekondari. Nikki anafahamika zaidi kwa kazi zake kama Good Boy, Nje ya Box, Gere, Pea, Kiujamaa, Bum Kubam na nyinginezo.