Serikali yashauriwa kutenga bajeti ya kununua vifaa tiba ili Kupunguza Vifo Vya Watoto
SERIKALI imepewa changamoto ya kutenga
fedha katika bajeti yake na kununua vifaa tiba pamoja na dawa zitakazosaidia
kupunguza au kuondoa kabisa vifo vya watoto wachanga hapa nchini ambapo ripoti
mbalimbali zinaonyesha mwaka jana pekee imefikia watoto elfu kumi na tatu.
Changamoto hiyo imetolewa na Taasisi ya
Doris Mollel Foundation muda mfupi baada ya kukabidhi vifaa vitakavyosaidia
kuokoa maisha ya watoto wachanga hususani watoto njiti katika Hospitali ya
Rufaa Mkoa wa Iringa.
Ndani ya chumba cha joto, katika
hosptali ya rufaa ya Mkoa wa Iringa, kila siku kinapokea watoto njiti
wasiopungua sita ikiwemo watoto wenye matatizo ya uzito uliopitiliza na
huhitaji matababu mazuri ili kuokoa uhai wao ikiwemo kuongezewa hewa ya oxygen
kupitia machine ziitwazo Oxygen Concentrator ambayo ni moja ya vifaa
vilivyotolewa na Taasisi hiyo
Mkuu wa Idara ya watoto katika hospitali
hiyo,Dr.Florida Kigosi amesema uhitaji wa mashine hizo ni angalau mashine sita
ambapo walizokuwa nao ni nne lakini zilizokuwa zinafanya kazi ni tatu tu na
sasa baada ya kupata msaada watakuwa na mashine nne
Pamoja na mashine hiyo, vifaa vingine
vilivyotolewa ni nguo mbalimbali, mipira
500 ya kulishia watoto wa aina hiyo ambapo Wauguzi wa chumba hicho cha watoto
njiti wameishukuru Taasisi hiyo huku Mkuu wa Mkoa wa Iringa,akikitaka kitengo
cha Malaria katika hospitali hiyo kuwa na mipango endelevu itakayosaidia
wajawazito kutojifungua watoto njiti kutokana na kuugua malaria
Ripoti ya mwaka juzi ya Shirika la
kuhudumia Watoto Duniani UNICEF inasema kuwa mwaka juzi watoto 9000 walipoteza
maisha kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo kuzaliwa njiti wakati Ripoti ya
Shirika la Mama Yee, inasema mwaka jana idadi ya vifo vya watoto wa aina hiyo
ilifikia watoto13,000.