INSPEKTA WA POLISI AUA MWANAYE, ATIWA MBARONI
Jeshi la Polisi linamshikilia Inspekta wake,
Celestine Makene (40) kwa madai ya kumpiga hadi kumsababishia kifo mtoto wa
kaka yake, Alerd Makene (16).
Makene anadaiwa kutenda kosa hilo Julai
24, mwaka huu katika makazi ya polisi, Mtoni Kijichi, Dar es Salaam na
anashikiliwa katika Kituo cha Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya
wa Kihenya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema marehemu Alerd
alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Mbagala Kuu.
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa kifo
chake unaendelea na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa endapo
itathibitika kuwa alitenda kosa hilo.
“Tunamshikilia mtuhumiwa wa mauaji hayo
ambaye pia ni askari polisi katika Chuo cha Polisi Kurasini, tutahakikisha kuwa
haki inatendeka bila kujali nafasi aliyonayo mtuhumiwa,” alisema kamanda huyo.
Imedaiwa kuwa Makene alimwadhibu baada ya
kupokea malalamiko kutoka kwa mzazi wa jirani akimlalamikia kwamba Alerd
alimpiga mwanaye hivyo kumtaka amkanye juu ya tabia hiyo.
Akizungumzia tukio hilo, jirani ambaye
hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alisema watoto hao walikuwa wakicheza
mpira lakini kwa bahati mbaya Alerd alimpiga rafiki yake huyo usoni kwa mpira
na baada ya kupigwa kwa mpira, alikwenda kwao kumshtaki.
“Usiku huo baba yake alimfungia chumbani
na kumpiga kwa fimbo, ngumi na mateke kiasi kilichomfanya mtoto huyo kupiga
kelele sana,” alisema na kuongeza kwamba majirani walijaribu kwenda kumwamulia
lakini hakusikiliza.
Alisema siku iliyofuata mtuhumiwa
alisafiri kikazi Nairobi lakini akadai kuwa kabla ya kuondoka, aliamuru mtoto
huyo asifunguliwe mlango.
Alidai kuwa baada ya mtoto huyo
kulalamika sana, mama yake mdogo alimfungulia mlango na kumkuta akiwa amevimba
uso na akivuja damu nyingi.
Alisema waliamua kumpeleka Hospitali ya
Temeke kwa matibabu na alifariki dunia usiku wa Ijumaa Agosti Mosi.
“Baba yake alirudi haraka kutoka Nairobi
alipopigiwa simu kuwa Alerd ana hali mbaya na alifahamishwa baada ya muda mfupi
kuwa amefariki,” alisema.
chanzo; mwananchi.co.tz