UKAWA WAMSHUKIA KIKWETE, WASEMA YEYE NA CCM HAWAELEWEKI!
Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa
Na Ibrahim Yamola na Goodluck Eliona, Mwananchi
Umoja huo
pia umedai kwamba Mahakama Kuu ya Tanzania imeshindwa kutoa uamuzi
fasaha kuhusu tafsiri ya kisheria ya mamlaka ya Bunge hilo katika
kurekebisha Rasimu ya Katiba kwa kuogopa lawama kutoka Ukawa na CCM.
Ukawa
unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, DP, NLD na NCCR-Mageuzi ulieleza
hayo jijini hapa jana ulipozungumzia Mchakato wa Katiba ulipofikia, hasa
baada ya Bunge hilo kufanya marekebisho ya kanuni kwa wajumbe wake
kuruhusiwa kupiga kura kwa njia ya mtandao.
Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema kuwa makubaliano ya kusitishwa kwa Bunge hilo kati yao na Rais
Kikwete yameshindwa kutekelezwa, jambo ambalo wanashindwa kuelewa sababu
zake.
“CCM na Rais
Kikwete hawaeleweki, tulikubaliana liahirishwe, tufanye marekebisho
katika Katiba ya sasa hasa uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea
binafsi, mshindi wa urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Lakini, hatuelewi imekuwaje, Bunge linaendelea sasa tunashindwa
kumwelewa,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunaitaka
Serikali na Rais Kikwete wasiingize nchi hii katika machafuko.
Wasiwajengee utamaduni Watanzania wa kufanya mapambano yasiyo rasmi.
Ukizuia watu kufanya harakati zao za siasa, unawafundisha kufanya mbinu
zingine. Tusifikie huko.”
Akinukuu
kauli ya Rais wa Kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela
aliyoitoa mwaka 1964 alipohukumiwa kifungo cha maisha gerezani alisema:
“Utawala wowote unaotumia majeshi na vyombo vyake vya dola kuzima sauti
ya raia wake, unafundisha raia hao namna ya kutafuta mbinu nyingine
tofauti ya kupambana na utawala huo.”
Akifafanua
kauli hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni alisema kuwa miaka miwili na nusu imepita sasa tangu walipozuiwa
kufanya maandamano kupaza sauti na kilio chao, lakini CCM wanaruhusiwa.
Alisema
kwamba wakati yeye akizuiwa kufanya ziara katika jimbo lake la uchaguzi
la Hai, wabunge wa upinzani wa Arusha, Mwanza na maeneo mengine
wakiendelea kutoruhusiwa kufanya mikutano, Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana anaendelea na mikutano na ziara katika mikoa ya Pwani
na Tanga.
Mbowe
aliongeza: “Hawa polisi wanaosema hawana uwezo wa kulinda mikutano yetu,
leo wana uwezo mkubwa wa kuzuia mikutano yetu. Tunapoelekea katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, kama CCM hawatabadili
mbinu zingine, hakika...hakika wanawafundisha Watanzania kubuni njia
mbadala ya kupinga uonevu huu.”
Awali,
akisoma tamko la Ukawa juu ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu
mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu
Lissu alisema kuna mgongano katika maana ya maneno yaliyotumika kwenye
kifungu cha 25 cha Sheria hiyo kwenye toleo la Kiingereza la sheria
hiyo.
Hata hivyo,
licha ya mgongano huo, tafsiri sahihi ya maneno ya kifungu hicho ni
kwamba; mamlaka ya ‘kujadili na kupitisha masharti ya Katiba
inayopendekezwa’ maana yake ni mamlaka ya kutunga na kupitisha Katiba
inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi wa Tanzania ili
kupigiwa Kura ya Maoni.”
Lissu ambaye
pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuwa ilivyokuwa kwa Mahakama
ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila
dhidi ya Mwanasheria Mkuu iliyohusu mgombea binafsi, Mahakama Kuu ya
Tanzania imekwepa kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki kwa kufuata
Katiba na Sheria za nchi kwa kujificha nyuma ya kichaka cha ‘uamuzi wa
kisiasa.’
Naye
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Sitta anatutia aibu
Watanzania kwa kupitisha mambo ya ajabu ajabu...kwamba kura ya
kupitisha Katiba itapigwa kwa email, fax na itaweza kupigwa hata kwa simu watu wakiwa bar, guest. Halafu
wanabadilisha tena kanuni kwamba kura itapigwa kwa sura, si kwa
kifungu. Hii ni kuhalalisha mabilioni batili ya fedha wanayokula bila
faida yoyote baadaye.”
Aliongeza:
“Tatizo letu katika nchi yetu kuna ombwe la uongozi, Rais Kikwete
alikuwa anaunga mkono Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini
walipomtisha wenzake akaogopa. Ndiyo maana leo hii hayupo nchini huku
nchi ikiwa katika kipindi muhimu.”
Alisema,
“Tumeshawaeleza kwamba theluthi mbili haitapatikana hasa Zanzibar lakini
hawasikii, Sitta anasimamia mambo anavyojua yeye. Ni wakati wa
Watanzania kusimama kidete kupigania Katiba bora inayokubalika na
makundi yote.”
Chadema waandamana Dar
Katika hatua
nyingine, Polisi jijini hapa jana walizima maandamano ya wafuasi wa
Chadema Jimbo la Ubungo waliokuwa wakiandamana kupinga Bunge la Maalumu
la Katiba linaloendelea Dodoma.
Kabla ya
kuanza kwa maandamano hayo yaliyoanzia kwenye ofisi za Chadema Tawi la
Kimara Korogwe, wafuasi hao walipeana mbinu za kufanya endapo Polisi
wangetokea kuwasambaratisha.
Wakiwa na
mabango yenye maandishi mbalimbali ya kupinga Bunge hilo na fedha
zilizotumika kuliendesha, walikubaliana kuwa endapo Polisi wakitokea na
kumkamata mmojawao, wote wangeingia kwenye gari la polisi.
Saa 8:45
asubuhi maandamano yalianza kuelekea katikati ya jiji, huku baadhi ya
wafuasi hao wakisikika kuwalaumu madereva wa bodaboda waliokuwa
wakiogopa kujiunga kwenye msafara.
Akizungumza
baada ya maandamano hayo, Justine alisema kuwa lengo lao limetimia kwa
kuwa walitaka viongozi wa serikali wajue kwamba kuna watu hawakubaliani
na kinachoendelea kwenye Bunge Maalumu.
Kamanda
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kuwa kuna watu
walikuwa wameingia barabarani kwa ajili ya kuandamana eneo la Kimara
Korogwe saa 3:00 asubuhi.
Alisema
kuwa kundi hilo lilitawanyika baada ya kuwaona polisi wakienda sehemu
waliyokusanyika lakini haikuweza kufahamika mara moja kama watu hao
walikuwa ni wafuasi wa Chadema au la.