HOFU YA EBOLA YATANDA HUKO SENGEREMA,BINTI AZIKWA KI EBOLA EBOLA
Watu
sita wakiwamo wahudumu watatu wa afya wa hospitali teule ya Wilaya ya
Sengerema mkoani Mwanza, wamewekwa chini ya uangalizi maalum baada ya
kumhudumia mgonjwa aliyefariki akiwa na dalili za ugonjwa wa ebola.
Mtu aliyefariki alitajwa kuwa ni Salome Richard (17), anayetoka katika kijiji cha Kahunda wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Akithibitisha
kuwapo kwa hali hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Wilaya ya
Sengerema, Dk. Mary Jose, alisema mgonjwa huyo alifikishwa katika
hospitali hiyo na ndugu zake watatu akiwa na homa kali huku akitokwa na
damu sehemu mbalimbali za mwili wake.Alisema vipimo vya mgonjwa huyo
vimepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
“Tulimpokea
juzi saa 7 mchana kutoka katika kijiji cha Kahunda wilayani hapa akiwa
na homa kali akitokwa damu mwilini, lakini kwa tahadhari tulimweka wodi
maalum peke yake akipatiwa matibabu na ilipotimu saa 8 usiku alifariki
dunia,” alisema
Alisema
kutokana na tahadhari ya ugonjwa huo, watumishi watatu wa idara ya afya
na ndugu watatu wa marehemu huyo, wamezuiliwa kwa kuwekwa katika
uangalizi maalum hadi matokeo ya vipimo vilivyochukuliwa
vitakaporejeshwa toka Muhimbili.
Akizungumzia
tukio hilo, muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo, Daniel Mihayo, alisema
timu maalum ya watalaam na viongozi wa mkoa walienda hospitalini hapo
juzi na kuondoka na vipimo vya mgonjwa huyo kabla hajafariki dunia kwa
kuzingatia maelekezo ya serikali ya kuchukua tahadhari linapotokea tukio
kama hilo.
“Kwa
sasa jamii inatakiwa kuepukana na uzushi uliozagaa kila kona kuhusu
mgonjwa huyo kufariki kwa ebola…tunawamba wasiwe na wasiwasi kwani hatua
stahiki zinachukuliwa kwa wagonjwa wa aina hiyo kama tahadhari,”
alisema Mihayo.
Mhudumu
aliyempokea mgonjwa huyo katika hospitali hiyo, Fungameza Majula,
alisema ndugu watatu walimpeleka mgonjwa huyo kwa taksi lakini
alipobaini dalili hizo aliujulisha uongozi wa hospitali na mara moja
hatua za tahadhari zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwazuia ndugu
kurudi nyumbani.
Hata hivyo, juhudi za kumpata mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Careen Yunusu, kuzungumzia tukio hilo hazikufanikiwa.
Akizungumzia
tukio hilo, Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw.Valentino Bangi, alisema
alipokea taarifa za mgonjwa huyo kufariki kwa homa inayofanana na
ugonjwa wa ebola au maburgh.
Bw.Bangi
alisema ofisi yake imetuma timu ya wataalam wa afya katika Hospitali ya
Wilaya Sengerema na kuchukua sampuli ya vipimo vya mgonjwa na kupeleka
Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Bw.Bangi
alisema ili kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo, tayari taifa,
uongozi wa mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na ofisi yake, wameweka vituo
vya kupima magonjwa katika mipaka ya Sirari, Mutukula na uwanja wa
Ndege wa Mwanza