WALIOPIGA KURA YA HAPANA WALALAMIKA KUTISHWA
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliopiga kura za hapana wamelazimika kuondoka Dodoma na kurudi Zanzibar kwa madai ya vitisho walivyopata kutoka kwa wenzao.
Mmoja wa wajumbe hao, Salma Said alisema jana jioni kuwa yeye na
wajumbe wenzake wamekataa kuitikia wito wa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel
Sitta kwenye Kamati ya Mashauriano ili kuhojiwa kuhusu kura hiyo na
kutokana na vitisho wanavyopata kutoka kwa wajumbe wenzao wameamua
kuondoka Dodoma.
Vitisho hivyo vimeripotiwa muda mfupi baada ya Sitta kuunda Kamati ya
Mashauriano ya watu tisa inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti, Samia
Suluhu Hassan kushughulikia kura hizo zilizopigwa na wajumbe saba
zinazoweka njiapanda uwezekano wa kupatikana akidi ya kupitisha Katiba
inayopendekezwa.
Wajumbe waliopiga kura za wazi za hapana kwa ibara zote ni Adil
Mohamed Adil, Dk Alley Soud Nassor, Fatma Mohamed Hassan, Jamila Ameir
Saleh, Salma Hamoud Said, Mwanaidi Othman Twahir na Ali Omary Juma.
Kwa upande wa Tanzania Bara aliyepiga kura ya hapana kwa rasimu nzima
ni Mbunge wa Mpanda Kati (Chadema), Said Arfi na wajumbe 30 kutoka
Zanzibar wakipiga kura ya siri.
“Baada ya kupiga kura za hapana leo (jana), walijitokeza wajumbe
akiwamo (jina tunalihifadhi kwa sasa) wakaanza kutuzongazonga,” alisema
Salma.
“Walituambia kuwa tumebaki hadi dakika ya mwisho halafu tunasema
hapana kwa rasimu nzima ili kula fedha za bure, wanasema bora
tungeondoka na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).”
Hata hivyo, alipopigiwa simu yake ya mkononi mmoja wa watuhimiwa,
alipokea na baada ya mwandishi kujitambulisha alikata simu na
alipopigiwa mara ya pili alijibu alisema; “Mimi ni mheshimiwa mwana na
niko Sudan.”
Salma alisema miongoni mwa wajumbe hao wakiwamo baadhi ya mawaziri
waliwafuata hadi nje ya ukumbi wakiwatishia kuwa watawafanyia hujuma kwa
kukataa kuunga mkono rasimu hiyo.
“Sisi tumeamua kuondoka kurudi kwetu, hatutaingia tena bungeni maana hivi vitisho vimezidi sasa,” alisema Salma.
Juhudi za kuwapata wajumbe wenzake kuzungumzia vitisho hivyo
hazikuzaa matunda, lakini Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad
alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba amelichukulia kama suala la
kisiasa.
Alisema wajumbe hao hawajasema wametishiwa kufanyiwa kitu gani, bali
walimweleza kuwa wameambiwa kuwa wamekaa pale (bungeni) kwa ajili ya
kupata pesa.
Kuhusu kukataa kwao kuhudhuria katika Kamati ya Mashauriano, Hamad
alisema hawezi kulitolea jibu kwa kuwa litafanya maridhiano yasifanyike.
Kamati ya Maridhiano
Akitangaza kuunda kamati hiyo, Sitta alisema ana suala mbele yake
ambalo linahitaji mashauriano chini ya Kanuni ya 54(4) kutokana na
baadhi ya wajumbe kupiga kura ya hapana kwa ibara zote.
Kanuni hiyo inasema: “Mwenyekiti baada ya kushauriana na kamati ya
uongozi anaweza kuunda kamati ya mashauriano pale linapojitokeza suala
linalohitaji mashauriano.
“Baadhi ya wajumbe jana (juzi), walipiga kura za hapana kwa ibara
zote, jambo ambalo haliwezekani kuwa hivyo. Kwa kushirikiana na Makamu
Mwenyekiti, nimeunda kamati hii ambayo naomba ikafanye kazi leo,”
alisema.
Alisema kamati hiyo yenye wajumbe tisa itakayoongozwa na Samia na
baada ya kikao chake cha jana itatoa matokeo bungeni. Wajumbe wengine ni
Rashid Mtuta, Shamsi Vuai Nahodha, Omary Yusuf Mzee, Mohamed Aboud,
Andrew Chenge, Dk Asha-Rose Migiro, Dk Francis Michael na Brigedia
Jenerali Hassan Ngwilizi.
“Hawa watakaa na wale wawili walioniomba kwamba wanataka kusikilizwa
kwa nini wamesema hapana kwa kitendo ambacho inaonekana kama wamepoteza
muda kukaa bungeni ili kukataa Katiba yote,” alisema.
Alitoa nafasi kwa wajumbe wengine ambao walipiga kura za hapana
watakaopenda kwenda katika kamati hiyo kueleza ni kwa nini waliikataa
rasimu hiyo.
Hata hivyo, kabla ya kuanza kwa upigaji kura jana, Sitta alisema kuwa
hali inakwenda vizuri… “Inshallah hali inakwenda vizuri na dua la kuku
halimpati mwewe.”
Kwa mujibu wa Kanuni 36(3). Endapo mjumbe baada ya kukataa ibara za
Rasimu ya Katiba, mwenyekiti ataunda kamati ya mashauriano ambayo
itasikiliza hoja zake na kupata mwafaka.
Kanuni 36 (4), baada ya kamati ya mashauriano kukutana na kujadili
ibara inayobishaniwa, itapeleka taarifa ya matokeo ya mashauriano yake
kwenye Bunge Maalumu kwa ajili ya kujadiliwa na ibara hiyo kama ilivyo
au baada ya kuandikwa upya kwa kuzingatia taarifa ya Kamati ya
Mashauriano.
Endapo theluthi mbili haitapatikana kwa mara ya pili, ibara hiyo
itahesabiwa kuwa haikukubaliwa wala kupitishwa na Bunge Maalumu kwa
mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria na kanuni hizi.
TEC yamshukia Sitta
Kauli ya Sitta kuwa baadhi ya nyaraka kuhusu mchakato wa Katiba Mpya
zinazotolewa na makanisani, “hazina utukufu wa Mungu na ni za kipuuzi”
imepondwa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC),
likisema hajui nguvu ya umma.
Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu wa Rais wa TEC, Askofu
Severine Niwemugizi alisema: “Unadhani tulivyotoa waraka tulikuwa
tunawataka waumini wafanye nini? Je, ni kufuata dhehebu lako limesema
nini au kufuata kilichomo katika waraka? Wewe (mwandishi) si Mkristo?
Jibu hilo.”
Aliongeza, “Wenye mapenzi na nchi hii wamfute kichwani Sitta na huo
upuuzi aliosema ni wake mwenyewe. Huyu anadhani kuwa ana akili kuliko
mamilioni ya Watanzania waliopendekeza wanataka kujitawala namna gani?”
Sitta alitoa kauli hiyo mjini Dodoma juzi wakati akiwatambulisha
viongozi 13 kutoka Jumuiya ya Image ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa
Msalaba ya mjini Dodoma.
Licha ya Sitta kutotaja taasisi husika, lakini Jukwaa la Wakristo
Tanzania ndilo lililotoa waraka unaotaka kusitishwa kwa mchakato wa
Katiba Mpya na kusambazwa makanisani.
Waraka huo ulitolewa kwa pamoja na TEC, Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (FPCT) na Kanisa la
Waadventista Wasabato (SDA).
“Anadhani wanaweza kutunga Katiba ya kuwatawala wananchi. Kauli
aliyoitoa ni sawa na kuwapuuza Watanzania na ni sababu ya madaraka tu,
maana ndiyo yanayowapa watu wengi kiburi,” alisema.
Askofu huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa kauli hiyo ya Sitta
maana yake ni kwamba CCM itabaki milele madarakani na Watanzania
hawawezi kuwafanya jambo lolote.
“Unajua mtu mwenye kiburi na dharau anayedhani hawezi kuambiwa
chochote unatakiwa kumwacha kama alivyo ila Watanzania ndiyo watakaoamua
nini wanataka katika maisha yao,” alisema.
Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Antony Lusekelo alisema:
“Bunge la Katiba limemwelemea Sitta na ndiyo maana ameanza kutukana
watu.”
Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako alisema kwa jinsi jamii
ilivyogawanyika katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, ilikuwa jambo la
busara kwa makanisa kutaka kusitishwa kwa mchakato huo mpaka makundi
yote yanayovutana yafikie mwafaka.
Masheikh waishtukia Serikali
Viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu nchini wamesema hawana
imani kuwa Serikali itatekeleza kauli yake kwamba mwakani itawasilisha
bungeni muswada wa sheria ili kutambua Mahakama ya Kadhi.
Wamesema kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, moja ya ajenda za CCM
ilikuwa ni kuhakikisha kuwa mahakama za Kiislamu zinatambulika kisheria,
lakini licha ya chama hicho kushinda mpaka sasa ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Juzi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kuokoa jahazi la
‘kuzama’ kwa Katiba Mpya kwa kupoza hasira za Waislamu kuhusu mahakama
hiyo kutoingizwa kwenye Katiba inayopendekezwa.
Msemaji Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na Shura ya Maimamu
Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba alisema: “Waziri Pinda amesema Januari
lakini sisi tunaona wazi kuwa kauli yake haina ukweli.
“Mahakama za Kiislamu zilizopo sasa hazitambuliki kisheria na
tunachokitaka ni kutambulika kwake na maamuzi yake yasiingiliwe.”
Akitolea mfano wa ahadi ya mwaka 2010 alisema, “Mahakama ya Kadhi ni
sehemu ya ibada kwa Waislamu. Ingesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo
wanalipwa watumishi wa mahakama kwa ajili ya kusikiliza kesi zinazoweza
kuamuliwa na mahakama za Kiislamu.”
Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani ya Kiislamu Tanzania (TIPF), Sheikh
Sadiki Godigodi alisema: “Wasiwasi wangu ni juu ya utekelezaji wa kauli
ya Pinda. Si mara ya kwanza Serikali kusema jambo hilo lakini
halitekelezwi.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh Wanazuoni wa Kiislamu
Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema: “Tulikuwa na madai ya asilimia
100 lakini Serikali imetupa asilimia 50. Tunazipokea lakini tunaendelea
kudai nyingine 50 kwa sababu si busara kukataa kupokea nusu ya kitu
ulichokiomba.
“Tunaamini Serikali itatekeleza maagizo yake na kuzifanya mahakama za
Kiislamu kutambulika kisheria. Itekeleze jambo hili kama ilivyoahidi.
MWANANCHI
MWANANCHI