MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana iliziruhusu kampuni
tano za simu kuingia kwenye kesi ya msingi kupinga sheria ya kodi ya sh
1,000 kwa kila laini ya simu.
Kuruhusiwa kwa kampuni hizo kulitokana na mjadala ulioibuka Oktoba 7,
mwaka huu, mahakamani hapo baada ya upande wa Jamhuri kupinga kuingia
kwa kampuni hizo na kuzua mjadala wa kisheria.
Kampuni hizo ni Vodacom, Airtel, Mic Tanzania Ltd, TTCL na Zantel
ambazo zinaungana na Taasisi ya Kutetea Walaji wa Bidhaa na Huduma
kuitaka Mahakama itamke kwamba sheria hiyo ni kandamizi.
Uamuzi huo ulitolewa na Mwenyekiti wa jopo la majaji watatu, Aloysius
Mujulizi akisaidiana na Lawrence Kaduri na Salvatory Bongole.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri
wa Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kuziandikia
kampuni za simu ili zianze kutoza kodi hiyo Septemba 30, 2013.
Baada ya uamuzi wa jopo hilo, mawakili wa upande wa walalamikaji
wakiongozwa na Wakili Fatma Karume, walitakiwa kupeleka maelezo yao kwa
maandishi Oktoba 15, mwaka huu iwapo watafanya marekebisho kwenye maombi
ya msingi ya kesi hiyo.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,
George Masaju, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Elicia Mbuya,
ulikubaliana na uamuzi wa Mahakama.
Akiahirisha kesi hiyo, Mwenyekiti wa jopo hilo, Jaji Mujuluzi alisema kesi hiyo itasikilizwa tena Oktoba 21, mwaka huu.
Katika kesi ya msingi iliyofungiliwa chini ya hati ya dharura, taasisi
hiyo inadai kwamba watumiaji wengi wa simu za mkononi hawana uwezo wa
kukatwa fedha hiyo kwa mwezi, huku wakisisitiza kuwa itawaathiri
watumiaji wa huduma hiyo.
Sheria hiyo ilipendekezwa na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) na kupitishwa kwenye Bunge la
bajeti lililotaka utekelezaji wake uanze Julai 30, mwaka huu, ili
kukusanya sh bilioni 178 kwa ajili ya kusaidia shughuli za bajeti kuu ya
serikali.
Malalamiko hayo yalimlazimu Rais Jakaya Kikwete kukutana na wadau wa
mawasiliano wakiwamo mawaziri wake, kisha kuwaagiza waangalie namna ya
kuziba pengo hilo iwapo kodi hiyo itaondolewa.
Licha ya agizo la rais kutekelezwa kwa wenye kampuni za simu kutakiwa
kuongeza kodi nyingine iitwayo ‘Excise Duty’ kutoka asilimia 14 hadi 17
bila kujali kwamba katika Bunge la bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka
asilimia 12 hadi asilimia 14, kodi ya laini za simu haijaondolewa.
Takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonesha kuwa miongoni mwa
wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini ya sh
1,000 kwa mwezi
|