WAKATI Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli akisema atahakikisha
anasimamia sheria ili jitihada za serikali za kudhibiti uharibifu wa
barabara zisidhoofishwe, wamiliki wa malori wamemtunishia misuli wakidai
kuwa hawajagoma bali wameegesha malori yao wasiendelee kuharibu
barabara.
Wamiliki hao walieleza kuwa waziri huyo amerudisha tozo ya asilimia
tano kwa maslahi yake na amekuwa mtu ambaye haambiliki, hashirikiani na
wadau pamoja na kujichukulia sheria mkononi.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam jana, wamiliki hao walieleza kuwa
sheria hiyo ilitangazwa na Magufuli kuanza kutumika Oktoba Mosi, na wao
walipatiwa barua Oktoba 2 ya kueleza kuwa tozo hiyo imeondolewa hali
iliyosababisha msongamano.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Consolidated Ltd, Karim Radha alisema kuwa
wanaomba sheria hiyo ifuate utaratibu wa kwenda bungeni na kupitishwa.
“Kwamba wasafirishaji tunataka faida kubwa! Huo ni uongo na sheria ya
tozo ipo nchi nyingi, hata kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata
zile za SADC, aseme kuwa anaogopa barabara zake hazina viwango, hivyo
zitaharibika,” alisema.
Davis Mosha kutoka Delina Group, alisema kuwa wao hawabishani na
kiongozi ila waziri hana dhamana ya kuvunja sheria iliyopo miaka 40
iliyopita.
“Hatutaki kukurupuka kwenda mahakamani kama ambavyo waziri alisema,
tunasubiri majibu, pia sisi hatupo kisiasa wala hatutumiki, hatujagoma
ila tumepaki vyombo vyetu,” alisema.
Naye Ibrahim Ismail alisema kuwa tozo hiyo ilikuwepo kutokana na mizani zote kutokuwa na viwango sawa.
Naye Waziri Magufuli kupitia kwa msemaji wa Wizara, Martin Ntemo
alisema kuwa nia ya serikali sio kuwatoza faini wasafirishaji hao bali
kuwaona wakiwa wazalendo katika kulinda barabara nchini.
Alisema hivi karibuni kumejitokeza wasafirishaji wasio waaminifu
waliokuwa na mawasiliano ya karibu na watendaji wa zamani waliokuwa
wakishirikiana nao kupitisha mizigo kinyume cha taratibu.
“Mianya hiyo kwa sasa imezidi kudhibitiwa na hali kwa sasa ni nzuri
tofauti na awali kabla ya kuwabadilisha wafanyakazi takriban 400 ambao
ni sawa na asilimia 85 ya watumishi wote katika vituo vya mizani na
kuajiriwa wapya,” alisema.
Ntemo alizipongeza baadhi ya kampuni za usafirishaji kuwa mfano wa
kuigwa, akizitaja Dar Express, Cargo Star, Hood Bus, Coca Cola, BM
Coach, Bakharesa (AZAM Transport), TBL, Golden Coach, Kanji Lanji Bus,
Taqwa, Consolidated Logistic, Lamada na Puma.
“Kumbukumbu zilizofanyiwa uchambuzi kwa kipindi cha miaka kumi
zimebainisha kuwa yapo makampuni ambayo hayana rekodi ya kuzidisha
mizigo wakati wote yanapopimwa katika vituo vya mizani ya barabarani,”
alisema.
|