HOTUBA YA MALINZI: HAFLA YA KUPOKEA KOMBE LA DUNIA TANZANIA
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Dk. Fennela Mukangara- Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Ndugu Dioniz Malinzi- Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
Mkuu wa msafara wa FIFA/Coca-Cola
Bw Yebeltal Getachew- Meneja Mkazi wa Coca-Cola
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF
Wageni waalikwa
Mabibi na mabwana
Mheshimiwa Rais, nianze kwa kukushukuru
kwa heshima uliyoupatia mpira wa Tanzania kwa kukubali kuwa mgeni rasmi
katika hafla yetu hii ya kupokea Kombe halisi la Dunia.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kupewa heshima hii na FIFA na washirika wake kampuni ya vinywaji ya Coca-Cola.
Coca-Cola ni washirika wetu wa karibu na wamekuwa wakidhamini mashindano ya kitaifa ya vijana tangu
mwaka 2007, mashindano ambayo kwa kiasi
kikubwa yamesaidia kuibua vipaji vingi ambapo baadhi yao wameweza
kuchezea timu zetu za Taifa na klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza.
Tunawashukuru sana Coca-Cola na tunaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano katika jitihada zao za kuendeleza soka ya vijana.
Mheshimiwa Rais, tarehe 19 Novemba, 2009
wakati unapokea kombe hili hili hapa Tanzania ulitoa changamoto kadhaa
kwa uongozi wa mpira wa Tanzania.
Ulitushauri tuimarishe uongozi na
utendaji wetu kuanzia ngazi ya Taifa, Mikoa, Wilaya hadi klabu,
ulitushauri tupate walimu wenye uzoefu wa kutosha kufundisha timu zetu
za mpira na pia ulitushauri tuwekeze katika kuibua na kuendeleza vipaji
vya wachezaji toka wakiwa na umri mdogo.
Mheshimiwa Rais ushauri wako kwetu
tuliuzingatia na tulifanya jitihada za kuufanyia kazi. Hali ya utulivu
katika uendeshaji mpira wetu imeimarishwa na pale palipoonyesha dalili
za migogoro tulikemea na ikibidi tulichukua hatua madhubuti kutatua
migogoro.
Tumefanya kozi mbalimbali za
kuwaendeleza walimu wetu wa mpira, waamuzi, madaktari na viongozi wetu
wa ngazi mbalimbali na matokeo yake yanaonekana katika kuinuka kwa
viwango vyao vya ufundishaji na utoaji uamuzi uwanjani.
Mheshimiwa Rais kama ulivyotuelekeza
mwaka 2009 maendeleo ya soka ya vijana ndio ufunguo wa maendeleo ya
mpira kwa Taifa letu. Uongozi mpya wa TFF ulioingia madarakani alfajiri
ya tarehe 28, Oktoba 2013 tayari unalifanyia kazi jambo hili kwa umakini
mkubwa.
Uongozi wetu umeamua kuwa ufunguo wa
mpango endelevu wa soka ya vijana utakuwa ni Tanzania kuwa mwenyeji wa
fainali za Afrika za vijana chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.
Fainali hizi uhusisha mataifa manane
yanayogawanywa katika makundi mawili ya awali akiwemo mwenyeji ambaye
anaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya fainali hizi. Aidha
timu mbili zinazoongoza makundi haya mawili moja kwa moja huwa zinacheza
fainali za dunia za vijana chini ya umri wa miaka
17.
Fainali hizi ndizo ziliwaibua akina Luis
Figo, Ronaldino, Nwankwo Kanu, Michael Essien, Nii Lamptey, Celestine
Babayaro na wengine kadhaa.
Ili tupate timu nzuri ya vijana umri
chini ya miaka 17 mwaka 2019 itabidi mwaka kesho 2014 tufanye mashindano
ya kitaifa ya vijana chini ya umri wa chini wa miaka 12 ili tupate
kikosi cha kwanza cha Taifa U-12, kikosi ambacho kitakuwa pamoja
kuelekea 2019.
Katika kuboresha kikosi hiki mwaka 2015
tutafanya mashindano ya kitaifa ya umri chini ya miaka 13, 2016 yatakuwa
ya umri chini ya miaka 14, 2017 yatakuwa ya umri chini ya miaka 15 na
2018 yatakuwa ya umri chini ya miaka 16 na ambayo yatatupatia kikosi cha
mwisho cha kuingia nacho fainali za vijana mwaka 2019.
Tunaamini timu nzuri za Taifa U-17 ya
mwaka 2019 itatuzalishia kikosi imara kitakachoshiriki Olimpiki za 2020,
kucheza CHAN na AFCON zitakazofuata na hatimae kufaulu fainali za dunia
2026 ambayo ni miaka kumi na tatu kuanzia sasa.
Ninashukuru tarehe 21 Novemba 2013,
Shirikisho la mpira barani Afrika (CAF) liliniteua kuwa Mjumbe wa Kamati
ya Maandalizi ya michuano ya Afrika umri
chini ya miaka 17 (CAF U-17 Organizing
Committee), tunaamini kuwepo kwangu katika kamati hii muhimu ya CAF
kutasaidia Tanzania ipate wenyeji huu mwaka 2019.
Mheshimiwa Rais kwa mujibu wa kanuni za
CAF nchi inayoomba uenyeji wa fainali za michuano ya Afrika haina budi
ionyeshe barua ya kuungwa mkono na nchi yake(Letter of support from
Government).
Wiki ijayo tutawasilisha barua kwenye
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya kuomba kuungwa mkono
na Serikali katika azma yetu hii, tunaomba Serikali ituunge mkono katika
jambo hili.
Mheshimiwa Rais nimalizie kwa
kukushukuru tena kwa uwepo wako katika shughuli hii muhimu, ninaishukuru
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano
wanaotupa katika shughuli zetu za kila siku, FIFA nawashukuru sana kwa
kutuwezesha kuwa moja ya nchi 88 duniani zilizopokea kombe hili,
Coca-Cola asanteni sana tuzidi kuwa karibu.
Watanzania wenzangu ninaomba tuje kwa
wingi kesho Jumamosi kutembelea Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na
kuliona Kombe hili na kupiga nalo picha. Imani yangu ni kuwa ipo siku
Kapteni wa Timu yetu ya Taifa atamkabidhi Rais wa Tanzania kombe hili.
Asante