Giza nene mabilioni ya IPTL, Tanesco
Dar es Salaam. Wakati
haijafahamika nani aliyelipwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa kwenye
akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na
mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya IPTL, imebainika kuwa Bunge
liliwahi kuagiza fedha hizo zisichukuliwe mpaka mitambo ya IPTL
itakapokuwa chini ya Tanesco mwakani.
Hiyo imo katika taarifa ya iliyokuwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwa mwaka wa
fedha ulioishia Juni 30, 2007.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu
alithibitisha jana kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 Milioni (Sh195.2
bilioni) katika akaunti hiyo, lakini akakataa kutaja nani hasa
aliyelipwa.
Mkataba wa miaka 20 baina ya IPTL na Tanesco
ulisainiwa mwaka 1995 na ulitakiwa kuisha 2015 na mitambo hiyo kuwa mali
ya Tanesco.
Hata hivyo, ukiwa umebaki mwaka mmoja kumalizika,
imebainika kuwa mitambo hiyo imeuzwa kwa Kampuni ya Pan African Power,
ambayo inatarajiwa kuingia mkataba mwingine na Tanesco ili iwauzie
umeme.
Ndulu alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo
ni Dola za Marekani 22 milioni na Sh161 bilioni za Tanzania ambazo zote
kwa pamoja ndizo zilizofikisha jumla ya Sh195.2 bilioni.
Vyanzo vingine vilitoa takwimu mbili tofauti,
kimoja kikisema kiasi cha fedha hizo kilifikia Dola za Marekani 270
milioni na kingine Dola 250 milioni. Kuhusu nani mwenye mamlaka ya kutoa
fedha hizo, Profesa Ndulu alisema kwa mujibu wa mkataba wa kufunguliwa
kwa akaunti ya fedha hizo, ni Wizara ya Nishati na Madini pamoja na
IPTL.
“Hakuna mtu mwingine anayeweza kuidhinisha
kutolewa kwa fedha hizo zaidi ya hao, kwa hiyo hao ndiyo waliosaini
kutolewa kwa hizo fedha na taratibu zote zilifuatwa,” alisema Profesa
Ndulu.
Alipoulizwa ni nani aliyelipwa fedha hizo, Profesa
Ndulu alisema IPTL ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kusema ni nani alipwe
na ilifanya hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim
Maswi alipoulizwa juu ya fedha hizo alisema: “Kwa kawaida huwa nina
majibu mafupi sana, lakini kwa kuwa mmeamua kuandika uongo, endeleeni,
siwezi kukujibu chochote wasiliana na hao IPTL wakujibu.”
Hata hivyo, haikuwa rahisi kumpata kiongozi wa IPTL kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari kampuni hiyo ni mufilisi.
Msimamo wa Bunge