Sitta apiga jaramba kuongoza Bunge
Dodoma. Siku moja baada ya
kuteuliwa na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia
sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki
kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta alisema:
“Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa
nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba.”
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo
ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo
na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani ya chama
hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi Magharibi,
Andrew Chenge alisema: “Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu ndani ya
CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta msuguano,
basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua majina
mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa kuniteua na
kwa sasa najiandaa na uchaguzi.”
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa
na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan
aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa
kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo
haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi
hiyo.
“Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote,” alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake
na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema
ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake
kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa
ushauri. Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana
alisema: “Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba,
angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili
walionyesha nia; Sitta na Chenge.