Header Ads

Kasi ya Yanga yawavuruga Al Ahly

yanga_bd8d6.jpg
Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi (kushoto) akiwapita walinzi wa Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi Jumamosi.
Dar es Salaam. Beki wa Al- Ahly, Said Ahmed Shedid amesema mechi ya marudiano itakuwa ngumu kwao kutokana na kasi ya washambuliaji wa Yanga pamoja na uwezekano wa mechi hiyo kuchezwa nje ya Cairo na El Gouna.
Yanga na Ahly zitashuka uwanjani Jumapili hii kuumana katika pambano la marudiano la Ligi ya Mabingwa Afrika raundi ya kwanza.

Beki huyo Shedidin alisema pamoja na kubadilishwa uwanja huo bado wanategemea kupata ushindani mkali kutoka kwa washambuliaji wa Yanga wenye kasi kubwa katika kushambulia.
Alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwao kama itachezwa nje ya Cairo na El Gouna, ambako hali yake ya hewa inafanana na ile ya Tanzania.
Kutokana na vurugu zilizojitokeza kwenye fainali ya Kombe la Super Cup kati ya Al-Ahly na CS Sfaxien na kusababisha polisi 22 kuumia, mechi hizo zitachezwa bila mashabiki.
Serikali ya Misri imesema mechi zote za Cairo zitachezwa bila ya mashabiki au kucheza kwenye Uwanja wa Jeshi wa jijini Cairo.
Naye nahodha Mohammad Yousuf, akiuzungumzia mchezo huo wa Jumapili alisema mabingwa hao wa Tanzania wameoneka kuwa wazuri zaidi katika kushambuliajia kwa kasi na kujilinda.
"Nidhamu na kasi yao wanapokuwa na mpira ni jambo inabidi kulifanyia kazi ya ziada kabla ya mechi yetu ya marudiano."
Yousuf alifafanua kuwa mechi hiyo haitakuwa rahisi kwao kutokana na uchezaji wa wapinzani wao. Lakini kurejea kwa nyota wao kama Abdullah Saeed na Sherif Abdul-Fadil ni faida kwao.
Tayari CAF imeshamtangaza mwamuzi wa Badara Diatta kuchezesha mchezo huo akisaidiwa na Jay Haji Abdul Aziz, na Bangor Forbade, na mwamuzi wanne Kebbi Dauda, na msimamizi wa mchezo huo atakuwa Massa Diarra kutoka Mauritania.
Wakati huohuo; Serikali imeitoa hofu Yanga kwa kusema kwamba tayari imechukua hadhari ili kuhakikisha inakuwa salama muda wote itakapokuwa Misri kwa ajili ya pambano dhidi ya Al Ahly.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe akizungumza jijini Dar es Salaam alisema, wizara yake imefanya mawasiliano na Balozi wa Tanzania nchini Misri kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa msafara wa Yanga.
"Nichukue fursa hii kusema kwamba serikali ipo nyuma ya Yanga kwa kuhakikisha inakuwa salama muda wote itakapokuwa Misri kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly.
"Tayari wizara yangu imewasiliana na balozi wetu Misri. Watapewa ulinzi mkali na wa hali ya juu kuanzia mazoezini hadi hotelini,"alisema Membe.
Aliongeza:"Lengo ni kuhakikisha timu yetu haifanyiwi vioja au vituko vya aina yoyote itakapokuwa kule, tunataka icheze mechi ikiwa huru."
Tayari uongozi wa Yanga umethibitisha kwamba msafara wa timu hiyo utaondoka nchini kesho kwa ndege ya kuekelea Misri tayari kwa ajili ya mchezo wao.
Chanzo, mwananchi (R.M)
Powered by Blogger.