SIENDI BUNGENI KUTAFUTA UTAJIRI, ANENA MGOMBEA WA CCM KALENGA
akisisitiza kazia atakazofanya |
MGOMBEA ubunge wa uchaguzi mdogo jimbo
la Kalenga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Godfrey Mgimwa amesema ajaingia
katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kujitafutia utajiri.
“Wapo baadhi ya wanasiasa wanatafuta
nafasi hii kwa lengo la kutafuta fedha na sio kuwatumikia wananchi; naomba
mniamini mimi sijaingia kwa lengo hilo,” alisema.
Aliyasema hayo wakati wa kampeni zake
alizofanya kwa nyakati tofauti jana katika vijiji vya Ilalasimba, Magubike,
Kidamali na Nzihi vya kata ya Nzihi jimbo humo.
Mgimwa alisema ametoka kwenye ajira
iliyokuwa ikilimpa vizuri kabla ya kuamua kutimiza ndoto yake ya siku nyingi ya
kuwatumikia wananchi wa jimbo lake hilo.
“Kabla sijaja kugombea ubunge katika
jimbo hili, nilikuwa mtumishi wa benki ya Stanibic makao makuu, huko nilikuwa
nikilipwa vizuri sana, lakini nikasema siwezi kuendelea ili nirudi kwenu kwa
lengo la kuwatumikieni,” alisema.
Aliwaomba wananchi wa kata hiyo na jimbo
hilo kumuamini huku akisisitiza kwamba yeye ni msomi asiye na majivuno, msikuvu
na asieyekata tama anapotaka jambo fulani lifanikiwe.
Katika mikutano kwenye kata hiyo, Mgimwa
alisema atazibeba na kuzifanyia kazi nyingi ya ahadi ilizotolewa na marehemu
baba yake, Dk William Mgimwa ili kuwaletea wananchi wa jimbo hilo maendeleo.
“Maendeleo ya jimbo hili yataletwa kwa
kutekeleza Ilani ya CCM ya 2010 lakini kuna ahadi zilitolewa na marehemu Dk
Mgimwa nje ya Ilani hiyo; niaminini nitazifanyia kazi,” alisema.
Akiwa katika kijiji cha Magubike
alisema, wakati wa uhai wake Dk Mgimwa aliahidi kutoa mabati 400 kwa ajili ya
ujenzi wa shule na zahanati ya kijiji hicho.
“Pamoja na ahadi hiyo aliahidi pia kutoa
Sh Milioni moja kwa kikundi cha wajasiariamali wanawake, nazichukua ahadi hizo
na nitazifanyia kazi,” alisema.
Akimuombea kura kwa wapiga kura wa kata
hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba alisema katika uchaguzi huo mdogo vyama vinavyoshiriki havishindanishi
sera.
“Serikali ilikwishaundwa baada ya
Uchaguzi Mkuu wa 2010, kinachofanywa sasa ni kuziba nafasi ya mbunge
aliyekuwepo, kwahiyo ahadi zinazotekelezwa ni zile zile zilizotolewa kupitia
Ilani ya CCM na mgombea husika,” alisema.
Alisema hiyo ni sababu tosha kwa wana
Kalenga kumpa kura za ushindi mgombea wa CCM kwa kuwa ndiye atakayemalizia
utekeleza wa Ilani na ahadi za Dk Mgimwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Nchemba aliwahakikishia wana Kalenga
kwamba Mgimwa ana kila sababu ya kumalizia kazi iliyoanza kutekelezwa na
marehemu baba yake ili aweze kutengeneza jina.
“Mnajua Uchaguzi Mkuu uatakaoshindanisha
sera za vyama mbalimbali utafanyika mwakani; kujiweke katika mazingira mazuri
ni lazima Mgimwa atatekeleza ahadi anazowapeni katika uchaguzi huu mdogo,”
alisema.
Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kalenga unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Dk Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu wakati akiendelea na matibabu yake nchi Afrika Kusini.