Header Ads

Zaidi ya Asilimia 20 ya bajeti hupotelea halmashauri

kamati_c466a.jpg
Dar es Salaam. Wizi wa fedha za umma kwenye halmashauri mbalimbali nchini unasababishwa na elimu ndogo ya baadhi ya madiwani ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa fedha hizo, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (Laac), Rajab Mbarouk Mohamed alisema jana kwamba zaidi ya asilimia 20 ya fedha za bajeti hupotea kila mwaka kwenye halmashauri. "Fedha hizi zinapotea kwa sababu madiwani ambao ndiyo wasimamizi wakuu wameshindwa kudhibiti wizi wa fedha hizo," alisema.
Mbarouk alisema wataalamu kwenye halmashauri hizo wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kufanya ufisadi kwa sababu baadhi ya madiwani hawana uelewa wa fedha wanazozisimamia.
Alisema halmashauri hizo zimekuwa zikipewa fedha nyingi kuliko zinazotolewa kwa baadhi ya wizara. "Kwa hiyo tunapoteza fedha nyingi kwa sababu madiwani wengi hawana elimu, tunahitaji kubadilisha mfumo wa usimamizi wa fedha," alisema Mbarouk.
Akitoa mfano alisema wakati kuna baadhi ya wizara zinapata bajeti isiyozidi Sh3 bilioni kuna halmashauri ambazo zinapata Sh15 bilioni.
"Hizi ni fedha nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa watu wenye elimu ya masuala ya fedha," alisema.
Mbarouk alisema wakati umefika wa kuanza kutoa elimu kwa madiwani ili waweze kusimamia ipasavyo fedha za Serikali.(E.L)
Powered by Blogger.