PANYA WATAJWA KUWA MOJA YA KIONGEZA VITAMINI
Mimi mwenyewe imenishangaza hii mtu wangu kwamba
watanzania wameshauriwa kufuga na kula panya aina ya ndezi wakieleza
kuwa nyama hiyo haina mafuta mengi, ikiwa pia na virutubisho muhimu na
vilivyo adimu.
Hiyo ni kwa mujibu wa wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha
Kilimo cha Sokoine (SUA) katika Maonyesho ya Vyuo Vikuu nchini
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Wataalamu hao walisema kuwa ili kukabiliana na uharibifu wa
kuchoma moto misitu kwa ajili ya kuwatafuta wanyama hao, ni vyema
wananchi wakaanza kuwafuga kwa kuwa nyama yao ina ladha nzuri na ni
laini.Mhadhiri Mwandamizi wa SUA, Idara ya Uzalishaji, Mirende Matiko
alisema kuwa ingawa wanyama hao wanafugwa kwa wingi katika nchi za
Afrika Magharibi, hapa nchini ufugaji wake unakabiliwa na changamoto
nyingi.
“Wakulima wetu hapa tunawapa wafuge, siku chache baadaye
ukienda utaambiwa walikufa, lakini ukiwauliza majirani wanakuwambia
‘jamaa aliwachinja’, ni sawa na kumpa mkulima mbegu halafu anakula,”
alisema Matiko.Akizungumzia namna nyama hiyo inavyoliwa, Matiko alisema:
“ Nyama yake ina viinilishe vingi, yanatupwa manyoya na miguu yake tu,
vitu vingine vyote vinaliwa. Tena utumbo ndiyo mtamu sana, si unajua
wanakula nyasi tu.
”“Mtu akitaka kufuga wanyama hao anatakiwa kuwa na banda
madhubuti lenye ubora, chakula na maji safi yawepo bandani muda wote na
upandishaji ufanyike katika muda mwafaka,” alisema.
Mhadhiri huyo alitoa hadhari kwa wafugaji akiwataka
kuwakamata wanyama hao kwa umakini kutumia chandarua, kuepuka
kusababisha majeraha.
Ndezi ni jamii ya nungunungu na pimbi, wakiwa wa aina
mbili, ambapo wadogo huwa na uzito wa kati ya kilo nne hadi sita na
wakubwa hufikia hadi kilo tisa.
Wanyama hao hupendelea kuishi kwenye maeneo yanayolimwa
mashamba ya miwa, ulezi na mpunga. Hata hivyo, Dk Loth Mulungu alisema
kuwa wawindaji wa ndezi porini husababisha madhara makubwa ikiwamo
uchomaji wa misitu, uharibifu wa bioanuwai, kukanyaga mazao mashambani
na upotevu wa muda.
Mmoja wa watazamaji waliotembelea Banda la SUA, Elizabeth
Maro alisema kuwa ingawa kwa muda mrefu amesikia watu wakila mnyama
huyo. Binafsi hawezi kula nyama yake kwa kuwa anaamini hana tofauti na
panya wengine.
“Siwezi kumla kwa namna yoyote, huyu ni panya tu ndiyo
maana hata jina lake kwa Kiingereza anaitwa ‘canerat’, maana yake panya
mla miwa,” alisema.Kwa hisani ya Gazeti la mwananchi.