SAMATA, ULIMWENGU KUTUA JUMAMOSI
Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania
wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mbwana Samata
na Thomas Ulimwengu wanatarajiwa kuwasili Jumamosi mchana (Mei 17 mwaka huu)
kujiunga na Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Washambuliaji hao watatokea moja
kwa moja Sudan ambapo kesho (Mei 16 mwaka huu) TP Mazembe itacheza mechi ya
Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya huko.
Ujio wa washambuliaji hao utafanya
wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kuwa wamepatikana kwa
ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika ambalo fainali zake zitachezwa
mwakani nchini Morocco. Mchezaji mwingine wan je ambaye tayari ameripoti Stars
ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini Qatar.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linamshukuru Mmliki wa TP Mazembe ambaye pia ni Gavana wa Jimbo
la Katanga, Moise Katumbi kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga na Taifa Stars
kwa vile mechi dhidi ya Zimbabwe ipo nje ya kalenda ya FIFA.
Naye Kocha Nooij atakuwa na mkutano
na waandishi wa habari kesho (Mei 16 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5
kamili asubuhi kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo katika hoteli ya Accomondia.
Wakati huo huo, Zimbabwe inawasili
usiku wa kuamkia Jumamosi (Mei 17 mwaka huu) ikiwa na msafara wa watu 27. Timu
hiyo itatua saa 7.30 usiku kwa ndege ya Ethiopian Airlines na itafikia hoteli
ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi, Dar es Salaam.
Zimbabwe itafanya mazoezi siku hiyo
jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo itakayochezwa
Jumapili saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)