TFF YAVURUGWA NA USAJILI WA DOMAYO AZAM, YATEUA WAKILI KUCHUNGUZA
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc ndani ya siku
mbili wamefanya usajili wa wachezaji wawili kutoka klabu ya Yanga SC
ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya kocha mkuu, Mcameroon,
Joseph Marius Omog.
Juzi walifanikiwa kumsainisha aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga,
Mrundi Didier Kavumbagu kwa mkataba wa mwaka mmoja, huku kipengele cha
kuongezewa mwaka mwingine kikiwepo kulingana na uwezo atakaouonesha.
Wakati wapenzi wa soka wakijadiliana usajili wa Kavumbagu, jana
wengi walishituliwa na usajili mwingine mkubwa wa kiungo mahiri wa
ukabaji wa Yanga, Frank Domayo `Chumvi”.
Domayo alisaini Mkataba wa miaka miwili kuitumia klabu ya Azam,
huku taarifa zikieleza kuwa mkataba wake na Yanga ulikuwa umemalizika
mwishoni mwa msimu uliopita.
Usajili wa Domayo ulifanyika jana katika kambi ya timu ya taifa
ya Tanzania, Taifa Stars iliyopo Tukuyu jijini Mbeya kwa maandalizi ya
mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi mei 4 mwaka huu uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya.
Stars ipo katika mipango ya mchezo huo na wachezaji wote
wanaufikiria, lakini kwa Domayo imekuwa tofauti ambapo akiwa huko
ameamua kusaini Azam fc.
Ukirejea nyuma sio mara ya kwanza mchezaji kusaini akiwa katika kambi ya timu ya taifa ya Tanzania.
Kelvin Yondani wakati anasaini Yanga kutokea Simba alikuwa kwenye kambi ya Taifa stars.
Ilielezwa kuwa alitoroshwa na kiungozi mmoja kwenda kusaini Yanga.
Kitendo kile kilitafsiriwa kuwa utovu wa nidhamu, lakini baadaye suala hilo lilizimwa kiaina kwasababu ni utamaduni wetu.
Domayo si mara yake ya kwanza, kwasababu miaka miwili iliyopita
wakati akijiunga na Yanga kutoka JKT Ruvu alisaini mkataba wake akiwa
kambi ya Stars.
Baada ya usajili huo kukamilika, Katibu wa Azam FC, Nassor
Idrisa Mohamed ‘Father’ amekaririwa na Tovuti ya Azam akisema katika
kuendelea kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wamepiga
hatua nyingine kwa kumsaini Domayo.
“Kama unavyojua, baada ya kumaliza msimu vizuri tukiwa mabingwa
wa Bara, tuligundua mapungufu kwenye kikosi chetu na kwa ushauri wa
mwalimu wetu (Joseph Marius Omog) ndiyo tunayafanyia kazi,”alisema
Father.
Domayo anakuwa mchezaji wa wa pili ndani ya siku mbili
kusajiliwa na Azam FC kutoka mabingwa wa zamani na mabingwa wa
kihistoria Tanzania Bara, Yanga SC baada ya jana klabu hiyo kumsaini
mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbangu.
Kufautai usajili wa aina hiyo kujitokeza tena katika kambi ya
Taifa stars, shirikisho la soka Tanzania, TFF limeshituka na kuanza
taratibu za kuchunguza suala hilo linaloihusisha Azam fc na mchezaji
Frank Domayo akiwa kambini.
Taarifa iliyotumwa na afisa
habari wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo, asubuhi hii inasema kuwa:
“Kutokana na tukio lililotokea jana (Aprili 30 mwaka huu) kwenye kambi
ya timu ya Taifa (Taifa Stars) iliyopo Tukuyu mkoani Mbeya likihusisha
usajili wa baadhi ya timu, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Jamal Malinzi amemteua Wakili Wilson Ogunde kuchunguza mlolongo
mzima wa tukio hilo.
Baada ya kukamilisha uchunguzi wake, Wakili Ogunde ataishauri TFF kuhusu hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua.
TFF inatoa wito kwa wachezaji, klabu na wadau wa mpira wa miguu kufuata kanuni na taratibu katika utendaji wao”.