TFF WASIKATE TAMAA NA STARS YA MABORESHO, AFCON NGUMU KUIFIKIA MWAKANI
0712461976
SHIRIKISHO la soka Tanzania limeshauriwa kutokata tamaa na
mpango wake wa maboresho ya Taifa Stars kupitia mkakati wake wa kusaka
vipaji mikoani ulioanzishwa hivi karibuni.
Taifa stars ya maboresho iliweka kambi mjini Tukuyu mkoani Mbeya
na kwa mara ya kwanza ilionekana aprili 26 mwaka huu uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi
kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mechi hii iliyowavutia wadau wengi wa soka kwa lengo la kuona
vipaji vipya kutoka mikoani, Stars ilipigwa vidude vitatu kwa bila,
(3-0).
Taifa Stars ilikuwa imesheheni vipaji vipya vilivyopatikana
katika mkakati wa maboresho ya Taifa stars ambapo jopo la makocha
waliteuliwa na TFF na kuzunguka nchi nzima kusaka vijana wa kuingizwa
katika timu.
Wakati mkakati huu ukitangazwa, wadau waliuchukuliwa kwa
mitazamo miwili tofauti ambapo na kundi moja liliunga mkono na lingine
likapinga kwa madai kuwa hautakuwa na tija kwa wakati huu ambao timu
inajiandaa kufuza AFCON mwakani nchini Morocco.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema mkakati huu ni kuisaidia
Stars ifuzu fainali za mataifa ya Afrika mwakani, na wachezaji
watakaopatikana katika maboresho haya wataweka kambi Tukuyu jijini Mbeya
na baadaye nchini Uholanzi.
Baada ya Taifa stars ya maboresho kuchapwa na Burundi katika
mechi ya kirafiki, maoni mengi yametolewa na wengi wanaponda mfumo huu
kuwa hauna msaada kwa sasa.
Wengi wanaeleza kuwa kumchukua mchezaji ambaye hachezi ligi
yoyote ile halafu unamleta Taifa stars , hawezi kukupatia matunda
unayotarajia.
Mtandao huu umehojiana na Mbwana Makata, Stephano Mwasyika na David Bugoya kwa nyakati tafouti.
Makata ambaye alikuwa kocha wa JKT Oljoro na JKT Ruvu kabla ya
kuziacha timu hizo kwa nyakati tofauti miaka ya karibuni, amesema
mkakati huu ni mzuri, lakini lazima mipango iwe imara.
Makata amefafanua kuwa kama TFF wanataka kufanikiwa katika
mkakati huu, basi wahakikishe unakuwa endelevu na wajenga mazingira
mazuri kwa wachezaji wanaopatikana.
“Kwa upande wangu naona si vibaya japokuwa una changamoto kubwa mno”.
“Naona itakuwa vizuri kama TFF wataharakisha ujenzi wa vituo vya
soka angalau mikoa mitano nchini ili kuwalea vijana hawa katika akademi
hizo”.
“Lakini kwa mazingira ya sasa, sina imani kama mfumo huu utasaidia sana”. Alisema Makata.
Kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na soka la Tanzania aliongeza kuwa ili kufanikiwa mpango huu kuna mambo yanatakiwa kuzingatiwa;
Mosi; lazima watanzania wawe na subira kwasababu si rahisi kufanikiwa kwa njia hii.
Makata alisema vitu kama hivi vinahitaji muda kwasababu hata mataifa yalitumia mfumo huu yalitumia miaka kadhaa kufikia malengo.
Pili; TFF na mashabiki wa soka wasiwe na matarajio ya kikosi
hiki cha maboresho kuipeleka nchi katika fainali za AFCON mwakani
kwasababu aina ya wachezaji waliopatikana hawana uzoefu wa kutosha na
wanahitaji miaka zaidi ya mitatu ili kuwa sawa.
Tatu; Makata alisema watanzania wasiwakatishe tamaa vijana kwa
kuandika na kuongea vibaya kwasababu watashindwa kujiamini na kila
wanapocheza watakuwa katika hali ya kukosa utulivu.
Makata alisisitiza kuwa uvumilivu ni muhimu kwa hili, na lazima TFF wasije na nguvu ya soda.
“Tatizo letu watanzania ni wepesi wa kupanga, lakini inapofikia utekelezaji inakuwa tofauti”.
“Zoezi liwe endelevu na inapobidi kwa pamoja tushauriane njia sahihi ya kwenda na sio kukosoa kila kitu”. Aliongeza Makata.
Naye meneja wa Mtibwa Sugar, David Bugoya alionesha wasiwasi wake juu ya mfumo huu kama kweli utafanikiwa mapema.
Bugoya alisema ni jambo zuri kutambua vipaji vya mkoani, lakini ni ngumu sana kufikia malengo kwa haraka.
“Mini nadhani TFF wangetumia mashindano mengi ya vijana yanayoendelea kusaka vipaji”.
“Sisemi mfumo ni mbaya, lakini nadhani unahitaji muda wa kutosha kufikia malengo”.
“Kwa jinsi ninavyoona mimi, labda kwa kuwa ni mapema. Nadhani kuna haja ya kuuangalia upya mfumo huu”.
“Kwenda AFCON kwa mfumo huu sina imani sana kwasababu mpira unahitaji muda na mipango” Alisema Bugoya.
Naye beki wa zamani wa Yanga, Moro United, Prisons na sasa Ruvu
Shooting, Stephano Mwasyika amewashauri watanzania kutokuwa na malengo
ya kufanikiwa kwa mwaka mmoja baadaye.
“Vijana hawa ni wazuri. Taifa stars labda itakuwa sawa miaka ya
2018/19 , kwasasa sidhani kama kweli mafanikio ya haraka yatapatikana”
“Tusiwakatishe tamaa vijana wetu, tuwape muda wa kujirekebisha na kujiimarisha zaidi. Uvumilivu uwepo na waaminiwe kwa asilimia kubwa”. Alisema Mwasyika.