Header Ads

UKAWA…Kusimamisha Mgombea Kutoka CCM

BABA wa Taifa hayati Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa upinzani wa kweli utakaokiondosha madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM), utatoka ndani ya chama hicho.
Wakati akitoa kauli hiyo, alijua fika kuwa baadhi ya makada wa chama hicho walikuwa hawakubaliani na baadhi ya mambo, hivyo wangeweza kuondoka na kujiunga na upinzani.
Miaka hiyo ni tofauti na sasa, wapinzani hivi sasa wana nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa miaka hiyo.
CCM wanahangaika kufanya hila kuwafitinisha na kuwafifisha kwa kuwa wanaona dalili ya kuondoka madarakani.
Ujio wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unaoundwa na vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na vinginevyo, unaonekana kutoa taswira mpya ya siasa za kishindani.
UKAWA, wameshatangaza nia kuungana na kuweka mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu ujao mwakani, na taarifa kutoka ndani ya kundi hilo zimedokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa mgombea kutoka ndani ya CCM.
Kinachofanywa na UKAWA kwenye mchakato wa katiba mpya kinaipeleka Tanzania kwenye mazingira ya kisiasa kama yale yaliyoikumba Kenya kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Hiyo, ni baada ya kuibuka kwa makundi mawili yenye nguvu kisiasa; Cord (Coalition for Reforms and Democracy) na Jubilee ambayo yalikuwa na ushindani mkubwa.
Kundi maarufu la UKAWA linaongoza mkakati wa kupatikana kwa katiba mpya yenye mtazamo wa hoja za wananchi, hasa zilizotolewa kwenye mapendekezo ya rasimu ya katiba, iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.
Wakati UKAWA wakionekana kupata umaarufu zaidi, limejitokeza kundi jingine linaloitwa Tanzania Kwanza. Hili limebeba wajumbe kutoka CCM, TLP na baadhi ya vyama vya upinzani.
Makundi haya mawili yamechukua sura za makundi ya Cord na Jubilee yaliyokuwapo nchini Kenya. Katika hatua hii, ni lazima wananchi watagawanyika.
Binafsi nimefuraishwa sana niliposikia vyama vikuu vya upinzani vinafikiria kuungana kwenye uchaguzi mkuu ujao na kusimamisha mgombea mmoja.
Hatua hii imezua hofu kubwa ndani ya chama tawala – CCM, kinachotajwa kuwa na mpasuko mkubwa, lakini kinakwenda kwa woga na kuvumiliana.
Nina imani kuwa hii ni fursa adhimu kwa vigogo wa CCM waliodhibitiwa ndani ya chama hicho kwa kupata sehemu ya kurukia endapo wataamua kuchukua maamuzi magumu kisiasa yasiyokubaliana na chama chao.
Tayari CCM wameshawafungia mwaka mmoja makada wake sita wanaotajwa kuwania urais kwa kuanza kampeni kabla ya wakati, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Makada hao ni William Ngeleja, Edward Lowassa, Stephen Wassira, Benard Membe, January Makamba na Fredrick Sumaye. Hawa wote wanaweza kuingia UKAWA kwa lengo la kutimiza ndoto zao.
Najua Nyerere alisema upinzani wa kweli utatoka CCM kwa kuwa anajua chama hicho kina mizizi mikubwa sana, kina uwezo wa kucheza na Tume ya Uchaguzi, polisi, wasimamizi wa uchaguzi na watendaji wengine wanaohusika na uchaguzi, ili mradi ushindi upatikane.
Kwangu itakuwa faraja kama makada nguli wa CCM wakihamia UKAWA, najua wakihamia huko wataungwa mkono, kuna wenzao watawaunga mkono, watadhibiti wizi wa kura kwa kuwa wanajua njia walizokuwa wakizitumia wakiwa CCM.
Ndani ya UKAWA kuna uwezekano wa namna mbili, ambapo wa kwanza ni ule wa mgombea urais kutoka ndani ya kundi hilo na wa pili ambao ni mkubwa zaidi, ni kupata mgombea kutoka ndani ya CCM.
Ndani ya CCM kuna mvutano mkubwa sana wa chini kwa chini kuhusu suala la urais. Makada wake hawaivi chungu kimoja katika hili, wapo wanaoamini kwamba kwa namna yoyote hawawezi kutendewa haki katika uteuzi huo.
Pia wapo wanaotembea na madukuduku yao ya muda mrefu, lakini wameshindwa kuibuka na kujitoa ndani ya CCM kuhofia kushindwa kwani bado inaonekana kama chama chenye nguvu.
Ninaamini kuwa UKAWA watafanya mazungumzo na vigogo wenye majina na nafasi nyeti ndani ya CCM kama njia ya kuhakikisha inatumia vyema muungano huo kupata ushindi kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Sina shaka UKAWA wako vitani katika kutafuta uongozi wa nchi, hivyo hawatoacha fursa ya kuwatumia vigogo wa CCM wanaobezwa na kukejeliwa kila siku ndani ya chama chao. Hata pale wanapofanya mambo mazuri na yenye maslahi kwa nchi.
Hawa watakuwa silaha muhimu ya kuhakikisha chama hicho tawala, kinashindwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Ni jambo la kheri mageuzi yanaonekana kupata mwelekeo mpya baada ya CCM kutaka kushinikiza matakwa yake ndani ya Bunge la Katiba, jambo ambalo limesaidia kuibua hasira za wapinzani kususia vikao vya Bunge hilo.
Naamini kuwa CCM wamefanya kosa kuonyesha moja kwa moja shinikizo la kutaka kupata katiba yenye maslahi yao. UKAWA, wanapaswa kulitumia kosa hilo kujipatia uungwaji mkono wa wananchi.
UKAWA, wameamua kwenda kuwaelimisha wananchi sababu za kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, lililotawaliwa na kauli za vitisho, ubaguzi, matusi na misimamo ya vyama ambayo kwa kiasi kikubwa haitotoa katiba ya wananchi.
Najua ushirikiano wa umoja huo pia ni faraja kwa makada wa CCM kupata kimbilio pale watakaposhindwa kuafikiana na chama chao katika mambo mbalimbali, hususani hili la urais.
Si lazima kila atakayetoka CCM akagombee urais kupitia UKAWA, lakini ukweli ni kwamba watu wanaotajwatajwa kuwa wameanza kunyemelewa na UKAWA, wana majina makubwa na kuheshimika ndani ya jamii.
Kuondoka kwao na kujiunga UKAWA kutasababisha kundi kubwa kuondoka ndani ya CCM. Inawezekana kuwa UKAWA, itatengeneza njia nzuri ya CCM kuondoka madarakani mapema zaidi kuliko ilivyotarajiwa.
Mabadiliko ya uongozi katika nchi hii ni jambo la muhimu sana kwa kuwa, kwa muda mrefu imeshindwa kupiga hatua kubwa za maendeleo, licha ya kuwa na rasilimali lukuki.
Bado hadi sasa bajeti ya Tanzania inategemea wahisani na wafadhili kwa asilimia 30 mpaka 40. Madini, mbuga za wanyama, mito, maziwa na bahari vimeshindwa kuwasaidia wananchi. Tatizo kubwa hapa, ni uongozi mbovu.
UKAWA, wanaweza kuleta mabadiliko kama wataendelea kuunganisha nguvu zao na kuibomoa CCM. Nawasihi wasifunge milango kwa makada wa CCM, wanaotaka kujiunga nao.
Powered by Blogger.