Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema tabia ya baadhi ya watu kupenda kuendeleza makundi,majungu na fitina na kuyaeneza miongoni mwa Viongozi na Wanachama wa CCM yanaweza kusababisha usaliti mkubwa unaoweza kuvuruga nguvu kubwa iliyopo ya chama hicho. Alisema sumu ya matendo hayo maovu ni kwa Viongozi na wanachama hao wa CCM kushikamana na kudumisha umoja miongoni mwao sambamba na kusahau kasoro zilizopita. Balozi Seif alisema hayo akiwa na msafara wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM waliofanya ziara maalum ya kuimarisha chama ndani ya Jimbo la Magogoni wakati akizungumza na Viongozi wa Jimbo hilo kwenye Mkutano wa ndani katika Tawi la CCM Magogoni Wilaya ya Dimani Mkoa wa Magharibi Kichama. Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwaomba Viongozi na wanachama hao wa CCM wa Jimbo la Magogoni kujipanga upya ili kuona nguvu za Chama cha Mapinduzi Jimboni humo zinakuwepo kama kawaida. Alisema katika kuunga mkono nguvu za wanachama hao za ujenzi wa ofisi zao amekubali kusaidia uendelezaji wa ujenzi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Magogoni pamoja na Tawi la CCM Mwenda Pole lililochomwa moto na vikundi vya kihuni ili yawe katika hadhi inayokubalika kichama. Akizungumzia maendeleo yaliyopatikana ndani ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mafanikio hayo ni vyema yakaendelea kulindwa na kudumishwa kwa hatma ya vizazi vijavyo. Aliwataka vijana wenye vipaji maalum kujikusanya pamoja na kuanzisha vikundi vya ushirika na serikali itajitahidi kuweka nguvu zake katika kuunga mkono Vijana hao kwa vile tayari imeshaanzisha mfuko maalum wa uwezeshaji. “ Tunafatajika sana kutokana na uamuzi wa Serikali Kuu kuanzisha mfuko maalum wa uwezeshaji ulio lenga kuwajengea uwezo wananchi katika kujiajiri wenyewe na kuongeza mapato yao “. Alifafanua Balozi Seif. Nao Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia Chama cha Mapinduzi waliwaomba wana CCM hao kuendelea kushikamana ili kuyapa fursa mashirika, Taasisi na hata wafadhili kupata shauku ya kusaidia nguvu za Wanachama hao pamoja na Wananchi katika kujipatia maendeleo yao kwa haraka. Wawakilishi hao walisema juhudi za makusudi zitaanzishwa kupitia uongozi wa Wawakilishi hao katika kuona umoja na mshikamano wa Jimbo hilo unaendelea siku hadi siku. “ Tumeshuhudia majimbo mbali mbali hapa Nchini yanavyoimarika kiuchumi katika miradi ya maendeleo likiwemo suala la michezo. Uwezo wa kusaidia kuanzisha ligi kwa timu za Jimbo hilo liko ndani ya mikono yetu na hili tunaahidi kulisimamia vilivyo “. Alisema Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura Hamza Hassan Haji. Mapema katika risala yao Viongozi na Wana CCM hao wa Jimbo la Magogoni wamewaomba viongozi wa Juu wa Chama hicho kuandaa utaratibu maalum wa kufanya ziara za makusudi kuhamasisha wanachama hao ili vugu vugu la kuendelea kuunga mkono chama hicho lidumu. Walisema hatua hiyo pia itasaidia kuelewa changa moto zinazowakabili wanachama hao na wananchi za mara kwa mara likiwemo tatizo la huduma duni za maji safi na salama pamoja na ajira kwa kundi kubwa la Vijana. Othman Khamis Ame Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar