MWALIMU ALIYEPIGWA MAWE NA WANANCHI HUKO SIMIYU ASIMULIA TUKIO ZIMA
NB-Picha haihusiani na tukio katika habari hapa chini |
Mwalimu
Festo Twange, aliyeshambuliwa kwa mawe akituhumiwa kuua mwanafunzi kwa
kumchapa viboko, amehadithia jinsi mkasa huo uliotaka kutoa uhai wake
ulivyo mpata.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, mwalimu huyo alisema siku
ya tukio alitoka nyumbani kwake akiwa amechelewa kwa sababu alikuwa
akimhudumia ndugu yake mgonjwa katika hospitali ya serikali ya Somanda
mjini Bariadi.
Alisema alifika shuleni akiwa amechelewa na kusaini kitabu cha maudhurio
na kisha kwenda moja kwa moja darasa la sita kufundisha somo la
hisabati.
Alisema akiwa darasani ghafla alifuatwa na walimu wenzake na kuambiwa
kuwa anatafutwa na Sungusungu kwa madai ya kumcharaza viboko mwanafunzi
wake na kusababisha kifo chake alipofika nyumbani.
Huku akionyesha hali yake kuendelea vizuri hospitalini hapo, alisema
baada ya kupata taarifa hiyo alikimbilia ofisi ya Mwalimu Mkuu kwa lengo
la kujificha kunusuru adhabu za walinzi hao.
Alisema pamoja na mbinu hiyo bado hakufanikiwa kwani walimwona na
kumfuata ofisi ya Mwalimu Mkuu na kuvunja mlango na kuanza kumshambulia
kwa silaha za jadi, fimbo, marungu na mawe na kujikuta amepoteza fahamu.
“Baada ya kumaliza kufundisha nilishangaa walimu wakija wanakimbia na
kuniambia natafutwa na Sungusungu kwa madai ya kumchapa mtoto na kumuua
hali ambayo ilinifanya nijifiche katika ofisi ya mwalimu mkuu..lakini
walivunja mlango na kuanza kunishambulia ambapo nilipoteza fahamu na
kujitambua nikiwa hapa hospitalini” alisema Twange.
Alisema anachokumbuka ni kipigo kikali na mayowe na baadaye kujikuta
akiwa yuko hospitalini huku kichwani akiwa amejeruhiwa vibaya.
Akisimulia zaidi mwalimu huyo alisema kuwa, siku hiyo mwanafunzi huyo
Shilinde Ng’holo (12) ambaye sasa ni marehemu hakufika shuleni hapo na
wenzake walipoulizwa na mwalimu akiwamo kaka wa binti huyo, alidai
mdogo wake amemuacha nyumbani kwao akiwa amelala.
“Shilinde siku hiyo hakufika shuleni hata kwenye mahudhurio ya wanafunzi
hakuwapo ambapo na nilipo wauliza wanafunzi wenzake na hata kaka yake
alieleza amemuacha nyumbani amelala” alisema mwalimu huyo.
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia watu saba kwa tuhuma ya
kuhusika katika tukio la kumshambulia mwalimu huyo, wakiwamo makamanda
wa Sungusungu ambao waliokwenda kumkamata mwalimu huyo.