WAUMINI NA WACHUNGAJI WA KANISA LA MOROVIANI MBEYA WAFUNGA KANISA KUSHINIKIZA ASKOFU WAO AJIUZULU
Baadhi
ya wachungaji na waumini wa kanisa la Moravian jimbo kuu la kusini
magharibi wamefunga kanisa kuu la jimbo hilo jijini Mbeya wakishinikiza
askofu mkuu wa jimbo la kusini magharibi, mchungaji Alinikisa Cheyo
ajiuzulu kutokana na kukiuka katiba ya kanisa lao.
-
Ni wachungaji na waumini wa kanisa la Moravian jimbo kuu la kusini
magharibi ambao wameamua kufunga geti la kanisa pamoja na ofisi ya baba
askofu Alinikisa Cheyo wakishinikiza askofu huyo ajiuzulu na hapa baadhi
ya wachungaji hao wanaelezea sababu ya wao kuchukua uamuzi huo.
Akizungumzia tukio hilo, makamu mwenyekiti wa kanisa hilo,
mchungaji Zacharia Sichone amesema waliofunga kanisa hilo ni watovu wa
nidhamu kwa sababu wanajua kuwa kanisa linaendeshwa kwa taratibu na
katiba waliyojiwekea.
Ili kuepusha uvunjifu wa amani katika eneo hilo, imembidi
mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Mbeya ambaye pia ni
mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Norman Sigalla kuingilia kati na kuwataka
wachungaji hao kufungua kanisa hilo huku akiwaahidi kuwa ufumbuzi wa
mgogoro wao utapatikana kwenye kikao kitakachofanyika kesho kati ya
uongozi wa kanisa hilo na kamati yake ya ulinzi na usalama.