NAPE AMJIBU DK.SLAA
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
Nape Nnauye akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa
Sekretarieti,Makao Makuu ya CCM Ofisi Ndogo Lumumba,ambapo aliwaeleza
kuwa Kamati Kuu imemteua Ndugu Philipo Mangula kuongoza Timu ya Kamati
Maalum ya CCM itakayoandaa Ilani ya CCM katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa pia Kamati Kuu imemteua Ndugu Adam Kimbisa kuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Uhuru Media tarehe 16 Julai 2014.
Jana Julai 15, 2014
Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Wilbroad Slaa alitoa shutuma kadhaa dhidi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
Katika shutuma hizo,
Dk. Slaa aliwatangazia wanahabari kuwa wamefanikiwa kudaka mawasiliano ya siri
pamoja na waraka wa Chama Cha Mapinduzi uliodai kuwa umeandaliwa na Kamati
maalumu na kuuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa CCM ili aupeleke kwa Mwenyekiti wa
CCM Rais Jakaya Kikwete ikiwa ni taarifa ya mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba.
Ukweli ni kwamba
taarifa za hicho ambacho Dk. Slaa amekiita ni waraka kutoka kwa Kamati Maalum
kuhusu mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba ni uzushi mtupu na unadhihirisha namna walivyo wavivu wa kufikiri kiasi cha kuanza
kutunga andiko na kutangaza wenyewe kwa jina la waraka.
Jambo
moja wanaloonekana kulimudu Chadema ni uwezo wao wa kutunga uongo na kupanga maandamano.
Na hii ndio siri ya Watanzania kuwakataa kila kukicha na ndio siri ya kufa kwa
chama hicho, kwani njia ya muongo ni fupi.
Dk. Slaa na Ukawa
lazima wajue kuwa hesabu waliyoipiga katika kujitafutia umaarufu kupitia
mchakato wa Katiba mpya umeshindwa kufanikiwa, hivyo kubakia wakitapatapa bila
hoja hakutawasaidia.
Ukweli ni kwamba CCM
haina haja ya kuhofia mchakato wa Katiba mpya kwa namna yoyote, kwa sababu
Mwenyekiti wake aliuanzisha akijua umuhimu wake kwa wakati wa sasa hasa
ikizingatiwa kuwa tayari Katiba tuliyonayo ishatufikisha mahali pa kuridhisha kwa
miaka hamsini iliyopita.
Kikubwa ni kwa Watanzania
kutokubali upotoshaji na uzushi wa baadhi ya viongozi akiwemo Dk. Slaa, badala
yake wananchi wajikite katika kufuatilia na kushiriki katika awamu mbili
zilizobakia kwa kuwa ndizo zitakazofanikisha kukamilika kwa mchakato wa Katiba
mpya bila matatizo.
Aidha, Dk. Slaa
ametumia nafasi hiyo na kujigeuza kuwa msemaji wa CCM kwa kuanza kutangaza juu
juu bila takwimu uhusiano wa CCM na taasisi ya Friederich Herbert Stuftung
(FES). Suala la uhusiano wa FES na CCM si la namna ambayo Dk. Slaa anataka
kulielezea. Bali uhusiano wa karibu kati ya Rais wa zamani wa Ujerumani na Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere uliojenga mahusiano makubwa ya kisiasa miongoni
mwao.
Kwa kuwa busara ya
Dk. Slaa ni kutunga uongo nalo hilo kwake limekuwa ni utetezi wa misaada ya
masharti magumu wanayopokea wao kutoka nje bila kuwaambia Watanzania malipo ya
misaada hiyo.