Slaa: Rais Kikwete ana rungu la Katiba Mpya
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amemtaka Rais
Jakaya Kikwete kujitokeza hadharani kutafuta suluhu ya kupata mwafaka wa
mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hakuna mamlaka nyingine zaidi
inayoweza kuunusuru.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.PICHA|MAKTABA
Pia, amewatahadharisha viongozi wa dini kuwa makini na kauli zao
wanazozitoa za kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kurejea bungeni Agosti 5.
Dk Slaa aliyasema hayo juzi katika mahojiano maalumu na gazeti hili,
makao makuu ya Chadema Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Mwenye rungu la kuweza kutengua kitendawili hiki ili turudi bungeni ni
Rais (Kikwete) mwenyewe, hakuna mwingine,”alisema Dk Slaa.
“Tatizo aliyesaini waraka uliowasilishwa na Warioba ni Rais mwenyewe,
alisaini ukurasa wa kwanza na wa mwisho, kwa taarifa rasmi za kina
Warioba, Rais alishirikishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hatua kwa
hatua na kwa kila hatua alisema sawa mchakato uendelee,”alisema Dk Slaa.
Alikumbusha kuwa wakati akipokea Rasimu ya Pili ya Katiba, Rais Kikwete
alisema: “Mtapata rasimu, ijadilini na itapitishwa na Bunge. Kwa
mwanasheria yeyote, lugha kujadiliwa na kupitishwa haitoi ruhusa ya
kubadilishwa, inatoa ruhusa kuboreshwa. Ndiyo utaratibu wa sheria zote
duniani.”
“Sasa anapofika mahali anayeleta wazo ni Rais, lakini kwa bahati mbaya
anayekwenda kupindua pia ni Rais na amekwenda mbali zaidi kiasi cha
kusema kwamba kama Serikali tatu ile ile ambayo yeye ameisaini
itapatikana, jeshi litapindua nchi.
“Anayezungumza ni Rais, hakuna mamlaka nyingine inayoweza kutengua
kitendawili hiki. Wanaweza kuja maaskofu, ...masheikh, asasi
mbalimbali... hatimaye hakuna anayeweza kutengua kwa sababu aliyeufanya
ni mwenye mamlaka ya juu,”alisema.
Dk Slaa aliyewahi kuwa Mbunge wa Karatu kwa vipindi tofauti alitaja
mambo matano anayopaswa kuyafanya Rais Kikwete ili wajunge wa Bunge
Maalumu la Katiba wanaounda Ukawa waweze kurejea bungeni.Aliainisha la
kwanza ni majadiliano kuwa na misingi iliyo wazi akisema Ukawa haipo
tayari kufanya mambo na kuishia kupewa pipi na kwamba Katiba Mpya lazima
ipatikane kwa maridhiano.
Alitaja jambo la pili kuwa ni lazima wao , Ukawa wahakikishiwe kuwa
kanuni hazichezewi baada ya kupitishwa na siyo kama ilivyofanya CCM,
baada ya Ukawa kutoka bungeni akisema hatua hiyo ni sawa na uhuni.
Lingine ni kuhakikishiwa kitakachojadiliwa ni rasimu iliyowasilishwa na
Tume ya Marekebisho ya Katiba si kingine.
Huku akitoa mfano wa hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere ya Juni, 1965
akisema ndiyo iliyowajibu CCM kuhusu msimamo wa Serikali mbili waliodai
ni kuenzi aliyoanzisha Nyerere, Dk Slaa alisema;
“Itakuwa upumbavu kama watu wataamini kwamba katiba haibadiliki, hata
kama imedhihirika kuwa haitoshelezi tena haja ya wananchi kwa wakati
ule.”
Alihoji kwamba ikiwa Mwalimu Nyerere alitoa kauli hiyo kipindi hicho ni
nini msingi wa CCM kuendelea kung’ang’ania hoja zao wakidai kudumisha
misingi yake (Nyerere). Alifafanua kuwa kimsingi katiba hubadilishwa kwa
haja mbalimbali za wananchi akitaja baadhi yake kuwa ni za kijamii,
kiuchumi, kifedha.
“Kikwete ndiye mwenye rungu la Katiba Mpya, achukue nafasi yake kama
mkuu wa nchi na siyo kama mwenyekiti wa CCM...Rais wa nchi hapaswi
kuwagawa Watanzania na wala hatakiwi kuonyesha tofauti kama alivyofanya
yeye alipozindua Bunge,” alisema.
Aliongeza: “Arudishe mchakato katika reli, aite wadau wakiwamo Ukawa na
asipofanya hivyo msimamo wetu ni ule ule wa kusimamia na kutetea maoni
ya wananchi waliyoyatoa.”
Hakuna haraka ya Katiba
Hata hivyo, Dk Slaa alisema kuwa hakuna haja ya kukimbizana kupata
Katiba Mpya kwa kutaka kulazimisha iweze kutumika katika uchaguzi mkuu
ujao mwakani, akihadharisha kuwa hilo likifanyika haitapatikana katiba
bora.
Alisema kuwa awali, Rais Kikwete aliwatangazia Watanzania kwamba Katiba
Mpya ingepatikana Aprili 26 mwaka huu katika maadhimisho ya miaka 50 ya
Muungano, lakini ameshindwa kutimiza ahadi hiyo.
“Hata kama ikipatikana (Katiba) Machi au Aprili mwakani, bado haiwezi
kutumika katika uchaguzi huo kwani kutakuwa na utaratibu wa kufumua
sheria zote hizo ili zifanye kazi kama Katiba inavyoelekeza, jambo
ambalo haliwezi kutekelezwa kwa kipindi kifupi,” alisema.
Alisema kuwa kinachotakiwa sasa ni Bunge kufanya marekebisho ya katiba
iliyopo ya mwaka 1977 katika vipengele viwili ili kuhakikisha uchaguzi
huo unafanyika ukiwa huru na haki.
Alivitaja vipengele hivyo kuwa ni suala la kuwapo kwa Tume Huru ya
Uchaguzi na rais kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 52 ya idadi ya
wapigakura.
“Huwezi kuongoza taifa ambalo hukuvuka asilimia 50 ya kura zote, mfano
mwaka 2010 Kikwete waliomchagua hawafiki robo ya waliopiga kura, sasa,
jambo hili linahitaji kufanyiwa marekebisho,” alisema.
Aliongeza: “Rais anaweza kuwa na dhamira nzuri, lakini kuna wanachama
ndani ya CCM ambao hawapendi katiba ipatikane katika kipindi cha uongozi
wa Rais Kikwete na yeye hafanyi uamuzi wake bali husukumwa na
wanaomzunguka, wanaotamani utawala.”
Atahadharisha viongozi wa dini
Kuhusu viongozi wa dini kuwataka Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi kurejea bungeni, katibu mkuu huyo wa Chadema
alisema, maaskofu wanatakiwa kuwa makini kabla ya kutoa kauli hizo.
Alisema kilichowatoa Ukawa bungeni ni kutokufuatwa kwa misingi ya
mjadala wa katiba na maoni ya wananchi kudharaulika na kuanza kujadiliwa
kwa Rasimu ya CCM.
“Maaskofu wangu hawajui kilichomo bungeni, hoja yetu ni je, tunarudi
tutajadili rasimu iliyopo mezani? Hatuwezi kukubali kuona rasimu
ikichakachuliwa.
“Viongozi wangu wa dini nawapenda sana, ila nawasihi wasiingie katika
hili kwani litakuja kuwahukumu siku ya mwisho kwa kutoa kauli ambazo
hawajafanyia utafiti,”alisema.
Aliongeza: “Wakumbuke, katika Biblia kuna maandiko yanasema; yeyote
anayewapotosha wadogo, anastahili kufungiwa jiwe shingoni. Wabunge
wanapotoka bungeni wanajali wakitaka sauti ya wanyonge isikike,
waliotutuma wanataka haki itendeke.
“Ukawa inapinga ‘dictatorship of the majority’(Udikteta wa wengi).
Tunachofanya ni njia halali ya mapambano inayoweza kutumika dunia nzima,
pale wengi wanapogeuka madikteta.”
Julai Mosi, Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania (TEC),
liliwataka Ukawa kurudi bungeni bila masharti na kuendelea na mjadala wa
Katiba Mpya kwa manufaa ya taifa.
Pia, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Jimbo la
Mashariki Kaskazini, Geoffrey Massawe aliomba wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba kuungana na kuwa kitu kimoja katika mchakato huo wa Katiba.
Askofu Massawe alitoa ombi hilo wakati wa ibada maalumu ya sherehe ya
maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo nchini
iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kinondoni, Dar es Salaam.
Akitoa salamu za TEC wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya uaskofu wa
Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa Kichangani, Iringa, Makamu Rais
wa TEC, Askofu Severine Niwemugizi alisema ni vyema wajumbe hao
wakarudi kwenye bunge hilo linalotarajia kuanza Agosti 5, mwaka huu.
“Ninatumia neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee bungeni mwezi ujao.
Wasipofanya hivyo au kufanya mizengwe mingine na kutupatia Katiba Mpya
isiyotufaa, nitawaomba Watanzania wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa
rasimu ya Katiba itakayoletwa pia tuwanyime uongozi katika uchaguzi
mkuu ujao,” alisema.
Nguvu ya Chadema
Katibu Mkuu huyo alisema chama hicho hivi sasa kina nguvu nchi nzima
kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu hivyo kinaweza kupambana vyema na
CCM.
Alisema wamekuwa wakitumia ruzuku wanayoipata kutoka serikalini ya Sh233
milioni kila mwezi kupeleka vitendea kazi katika majimbo na kanda.
“Tuliamua kufanya hivyo kwani tulivyokuwa tukipeleka fedha walikuwa
wakizigombania na mpaka sasa kanda kumi zina gari moja moja na wilayani
kuna pikipiki moja pamoja na kompyuta.
“Yaani, sasa hivi kama CCM ina wachezaji 11 uwanjani nasi (Chadema)
tunao wachezaji 11 ni tofauti na ilivyokuwa mwanzo hivyo mpira
unachezeka sawasawa,” alisema.
Aliongeza kuwa kanda na majimbo yanajiendesha kwani wamepeleka zaidi ya
kadi milioni 75 ambazo kila kadi ni Sh1500 na ada ni Sh1,000 hivyo fedha
hizo zinaweza kuendesha ofisi hizo bila kutegemea fedha kutoka makao
makuu.
Ofisi ya Zitto
Akizungumzia kubadilishwa kwa matumizi kwa ofisi ya aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, Dk Slaa alisema amefanya hivyo kutokana na
mhusika kutoitumia kwa muda mrefu.
“Nimefanya hivyo kwani siwezi kuiacha ofisi ikakaa bila mtu wakati kuna
watu wangu hapa wanabanana na hata mkipita mtaona nimebadili matumizi ya
ofisi,” alisema Dk Slaa.