APIGWA RISASI ZA KWAPA NA KUJERUHIWA VIBAYA,TUKIO LIKO HAPA
Mke wa Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wafugaji la
Pingos Forum, Edward Porokwa, Flora Porokwa aliyepigwa risasi.
MKE wa Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wafugaji la
Pingos Forum, Edward Porokwa, Flora Porokwa (37), mkazi wa Sakina Kwaidi
amepigwa
risasi na watu wanaohisiwa kuwa ni majambazi.Tukio hilo lilitokea
juzikati ambapo risasi hiyo alipigwa kwapani na kwenda kutokea mgongoni na
kulazimika kuendesha gari umbali wa kilometa moja akiwa na risasi mwilini.
Majeruhi huyo ambaye
amelazwa katika Hospitali ya Seliani jijini hapa, alionesha ujasiri wa
hali ya juu baada ya kumudu kuendesha gari hilo huku watu hao wawili waliokuwa
wamepanda bodaboda wakiendelea kumfuatilia hadi alipofika nje ya nyumba yake
ambapo aliishiwa nguvu na kupoteza fahamu akiwa anasubiri kufunguliwa geti la
kuingia ndani. Akizungumza kwa tabu hospitalini hapo, majeruhi huyo alisema
tukio hilo lilimtokea jioni ya saa moja kasoro katika Barabara ya Arusha -
Namanga eneo la Kwaidi ambapo watu hao walimvamia ghafla na kulizuia gari lake
kwa mbele wakitumia pikipiki hiyo.
Jeraha la mgongoni alilopata Flora Porokwa.
Alisema mmoja wa watu hao alimfuata na kushika kitasa cha
mlango wa mbele na kujaribu kufungua lakini mlango haukufunguka. Ndipo mwanamke
huyo alipoamua kushusha kioo cha mlango ili aweze kumsikiliza, lakini ghafla
jambazi huyo alichomoa bastola na kumpiga risasi kwapani.
“Kwenye gari sikuwa na fedha, sijui kama walilenga kunipora
au kuna tatizo lingine. Nikiwaona naweza kuwakumbuka kwa sura ila siwajui,
sikuwahi kuwaona kabla,’’
alisema mwanamke huyo na kuongeza kuwa:
“Namshukuru Mungu kwa kuniepusha na kifo kwani dhamira yao
ilikuwa kuniua.”
Majeruhi huyo ambaye hali yake bado siyo vizuri, alitoa rai
kwa jeshi la polisi mkoani Arusha kuwasaka watu hao kisha kuwafikisha
mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Hadi sasa tukio hilo halijafahamika undani wake kama watu
hao walilenga kupora fedha au ni kisasi,
kwani kabla ya tukio hilo kuna taarifa kwamba hata mumewe, Porokwa aliwahi
kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Jirani mmoja wa mama huyo ambaye hakupenda jina lake
liandikwe gazetini, alisema wamesikitishwa mno na tukio la mwenzao kupigwa
risasi.