KIJANA WA KIMASAI ANAYELITAKA JIMBO LA WILLIAM LUKUVI AWA MAKAMU MWENYEKITI WA BAVICHA
Patrick Ole Sosopi |
YULE
kijana anayetarajia kutoa upinzani mkali kwa William Lukuvi endapo chama chake
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitamsimamisha kuwania ubunge Jimbo
la Isimani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Patrick Ole Sosopi amechaguliwa kuwa
Makamu Mwenyekiti Bara wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
Chadema(BAVICHA).
Mbali
na kuwa mbunge wa Jimbo la Isimani kwa awamu ya tatu sasa, William
Lukuvi ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (sera na uratibu wa
bunge).
Katika
uchaguzi huo wa BAVICHA uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, nafasi ya Mwenyekiti
ilikwenda kwa Patrobasi Katambi na Zeudi Abdalla alichaguliwa kuwa Makamu
Mwenyekiti Zanzibar.
Kuchaguliwa
kwa Sosopi kushika nafasi hiyo nyeti ndani ya chama hicho kumeelezwa na baadhi
ya wafuatiliaji wa siasa za mkoa wa Iringa kwamba kunamuongezea nguvu kisiasa.
Patrick Ole Sosopi ambaye ni baba wa mke mmoja na
mwenye mtoto mmoja, ni mmasai aliyezaliwa na kukulia mkoa Iringa, jimbo la
Ismani.
Ana umri wa miaka 28. Ni msomi wa shahada ya kwanza
ya Biashara na Utawala (rasilimali watu) kutoka chuo kikuu cha Ruaha (RUCO).
Kwa sasa kazi zake ni kufuga ng'ombe.
Historia yake ya uongozi ilianzia akiwa shule ya
msingi, sekondari hadi chuo kikuu cha RUCO ambapo alikuwa waziri wa Fedha
kwenye serikali ya wanafunzi 2011/2012.
Alijiunga rasmi na CHADEMA mwaka 2009 alipokuwa
mwanafunzi wa mwaka wa kwanza akiamini ni chama pekee ambacho kina tija ya
kuboresha maisha ya jamii yake ya kimasai na changamoto mbalimbali ambazo
zilikuwa zikiwakabili.
Aliaminiwa na vijana wa Ismani na kupata kura zote
bila kupingwa na kuwa Mwenyekiti wa BAVICHA jimbo la Ismani. Baada ya
kushauriwa na kushauriana na familia yake na vijana mbalimbali kutoka sehemu
mbalimbali za Tanzania, aligombea nafasi ya Umakamu Mwenyekiti wa BAVICHA Bara
na ameshinda.
Ingawa ni mojawapo wa wasomi wachache kwenye jamii
yao ya kimasai, ni mtu ambaye usomi wake haujamfanya asahau mila na tamaduni za
kimasai. Chakula chake, mavazi yake, desturi yake ya maisha ya kila siku ni
desturi za kwao na zenye kuhuwisha Utanzania.