MAAJABU; Soma Inaweza Kukujenga Kiimani.
UKIPATA NAFASI YA KUSOMA STORY HII SOMA INAWEZA IKAKUJENGA KIIMANI.
Ni stori inayosimuliwa na mmoja wa aliyekutwa na jambo hili linalofunza
na kusikitisha sana. Lengo ni kutambua baadhi ya mambo mengi ya kidunia
na kiroho ili kuepukana na mambo ambayo huwezi jua mwisho wake na
kwanini yanakukuta.... Isome hapo chini.
Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma
sana. Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje
Mungu anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati
ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na hasa baada ya
kujifunza maarifa haya ya utambuzi.Ilikuwa ni mwaka 197...9 nikiwa
nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini
ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni.
Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kama siku
hizi.Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa
ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja
serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga.
Hata hivyo sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi
kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili. Tulifika mji
unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji maarufu kwa hoteli
zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha.
Tulipofika Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata
chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba
ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na
muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo
nililosafiri nalo.Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa.
Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza
kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria
wengine wahuni bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao
kila siku hasara tu" Mwenye hoteli alisema kwa kudhamiria hasa.
Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima anipeleke
polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha
polisi ili nishughulikiwe..Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja
aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana
alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta
nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana.Alikuwa ni kijana mtu
mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi.
Nilimsalimia na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza
kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha
ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote na ningerudi
vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama huko
polisi ningeaminika.Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa
fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake.
Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee
fedha zake ofisini kwake.
Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua
kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na
maisha haya ni mzunguko. Nilimshukuru na kuondoka kukimbilia basini.
Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria
wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda basi
letu lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi
tuegeshe pembeni ili litengenezwe.
Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.Karibu na mji
wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria
walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje
kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini
walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo
nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili.
Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu
kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga
kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa sio
sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu.
alikuwa ameumia kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai.
Bila shaka wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi
yalinitoka.Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani
kuchukua maiti wale tulipanda basini kuendelea na safari yetu. Kale
katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali
kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu
ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani
tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili .Nililala kwenye
hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake.
Ni hiyo kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata
mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile
ya Same walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto
wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina
la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na
picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.Nillishindwa kujua ni
kwa nini afe.
Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo
na majibu na pengine maswali ya kijinga pia.Nilijua kwamba nilikuwa na
deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini zilikuwa
ni sawa na shilingi laki moja za sasa.Kwa mara ya kwanza sasa
nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule aliniamini nakuamua kunipa fedha
zile. Sikupata jibu.Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza
kilichokuwa na habari ile.
Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni,
Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba mungu
anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia yoyote.
'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na namna
ujuavyo wewe. Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo
marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo hiyo.
Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule kuwa
mbaya kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka sana
kuhusu mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata hivyo
kupata nafasi ya kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha ufundi na
hatimaye nilibahatika kwenda nchini Uingereza.
Mwaka 1991 nilianza shughuli zangu.Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini
kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco ambalo liliungua mwaka 1996, ambapo
lilijengwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa Water Front. Nikiwa
nafanya kazi zangu niliambiwa na sekratari wangu kwamba kulikuwa na
kijana aliyekuwa anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema
hamjui.
Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni
kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo.
Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya yake ikiwa
hairidhishi sana.Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona
atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu
mwenye huruma sana na nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au
majina.
Nilimuuliza, "nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru
maana nina kikao baada ya muda mfupi". Nilisema na sikuwa na kikao
chochote , lakini nilitaka tu aondoke haraka."Samahani mzee, nilikuwa na
shida...nimefukuzwa shule na sina tena mtu wakunisaidia kwa sababu
...nime..niko ..kidato cha pili na hivyo tu natafuta tu kama atatokea
mtu....Nilimkatisha. "Sikiliza kijana.
Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi
unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule si
nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie..Kwanza wazazi
wako wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe ...Kwa nini walikupeleka
shule ya kulipia kama hawana uwezo, wanataka sifa?"
"Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa hata kazi hafanyi..,"
Alianza kulia. Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu
na matumizi, kwa nini nisiwe mwema, angalau kwa mara moja tu. "Baba na
mama walifariki lini?" Niliuliza nikijua kwamba, watakuwa wamekufa kwa
ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo
kila anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi.
"Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndio shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa." Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana.
"Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi wako
walikufa mwaka gani na wapi?"Yule kijana alisema, "Nimeona nijaribu tu
kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, na ndio nimejikuta nikiingia
hapa, sijui....sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko
Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu
hapa."
Alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso.Nilihisi kitu fulani
kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona kama vile nimebanwa na
kushindwa kupumua. "Baba yako alikuwa anaitwa nani?" "Alikuwa anaitwa
Siame..Cosmas Siame.." Niliinuka ghafla hadi yule kijana alishtuka .
Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye droo moja
na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti
ndani ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi."Ndio alikuwa anaitwa
Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika."
Nilinong'ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali.
"Mungu, wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani."
Halafu nilinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa
nguvu zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.Nilisimama nikiwa
nimesawajika kabisa. Nilihisi kuwa mtu mwingine kabisa. Nilimfuata yule
kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. "Mimi ni baba yako
mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi mwisho"
Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa.
Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17
iliyopita.Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo
la maziwa ambako alikuwa amepanga chumba.
Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia
kilichotokea. Huyo dada yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa
kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki hata hivyo mwaka mmoja baadae,
lakini akiwa ameridhika sana.Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu
na hivi sasa yuko nchini Australia anakofanya kazi.
Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa.
Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile walichokipanda
miaka mingi sana nyuma. Lakini nami najiuliza bado. Ilikuwaje Cosmas
akanipa msaada ule? Halafu najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame
hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie,
usiwe mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo
maishani mwetu....