Katiba inayopendekezwa kuchapishwa upya tena
Uongozi wa Bunge Maalumu la Katiba, umemuagiza Mpigachapa Mkuu wa Serikali, kupiga chapa upya Katiba Inayopendekezwa, baada ya kubaini makosa ya uchapaji, ikiwemo kuandikwa kwa makosa kwa mjumbe wa bunge hilo kupitia NCCR-Mageuzi Zanzibar, Haji Ambar Khamis.
Katika
chapisho la Katiba Inayopendekezwa, mjumbe Khamis ameonekana kama vile
alishiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu la Katiba, wakati
hakushiriki.
Kosa
hilo na mengine ya uchapaji, yamekuwa yakitumika kwa makusudi kupotosha
umma kuwa Katiba Inayopendekezwa, ilipita katika mazingira ya
kuchakachua kura za wajumbe, ili kuiondolea uhalali wake wakati wa
kupiga kura ya maoni.
Moja
ya jitihada hizo ni pamoja na hatua ya mjumbe Khamis, kuangua kilio
juzi mbele ya waandishi wa habari na kukimbizwa hospitalini kwa
matibabu, baada ya kukiri chini ya kiapo cha chama chake cha
NCCR-Mageuzi, kuwa hakushiriki kuipitisha Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumza
na mwandishi jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Dar es Salaam, Naibu Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Dk
Thomas Kashililah, alisema jina la Khamis kuwepo katika orodha hiyo, ni
moja kati ya makosa kadhaa yaliyobainika.
“Sisi
tulibaini kasoro hiyo na mengine ya uchapaji siku ya kukabidhi Katiba
hiyo Pendekezwa na kuelekeza Katiba hiyo ichapishwe upya baada ya
kufanyiwa marekebisho,” alisema Dk Kashililah.
Alifafanua
kuwa kuna vitabu vya aina mbili, kimoja kinachotumika kwa ajili ya
kumbukumbu, ambacho kina majina ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu la
Katiba, wakiwemo wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na
wajumbe wengine ambao si wa Ukawa, lakini hawakushiriki kupiga kura.
Kitabu
cha pili kwa mujibu Dk Kashililah, kimeorodhesha majina ya washiriki wa
Bunge hilo katika awamu zote, ambacho wajumbe wa Ukawa na wengine ambao
si wa kundi hilo hawapo kwa kuwa hawakushiriki mpaka mwisho.
“Baada
ya kurekebisha (kile kitabu cha kumbukumbu) ili kupata kitabu
kinachoeleza wajumbe waliopitisha Katiba Inayopendekezwa, jina hilo
lilipita kimakosa wakati hakupiga kura, tunathibitisha hilo kosa kwa
kuwa ni kweli hakuwepo kupitisha Katiba hiyo,” alisema.
Alifafanua
kuwa katika orodha ya wapigakura, Mjumbe huyo wa NCCR-Mageuzi, alikuwa
namba 63 lakini hakupigakura jambo ambalo haliathiri hata kidogo kura
zilizopitisha Katiba Inayopendekezwa.
Pia
Dk Kashililah alitoa ufafanuzi kuhusu wajumbe waliopiga kura kwa kusema
jumla walikuwa 631, lakini baada ya mmoja kufariki walibaki 630 na kati
yao, 411 walikuwa wa Tanzania Bara na 219 wa Zanzibar.
Alisema
idadi hiyo ilipatikana baada ya mjumbe Salim Suleiman Ally kuondolewa
Zanzibar na kuwekwa upande wa Tanzania Bara baada ya kuwekwa Zanzibar
kimakosa.
Katika
upande wa Zanzibar theluthi mbili ya kura zilizotakiwa kupitisha Katiba
Inayopendekezwa, zilipaswa kuwa 146, hata hivyo Katiba hiyo kila ibara
ilipitishwa kwa wastani wa kura 146 na 148.
Kwa
upande wa Tanzania Bara, wajumbe 335 walipiga kura ambapo kila ibara
ilipata wastani wa kura 331 mpaka 334, na hivyo kuzidi theluthi mbili
iliyokuwa ikihitajika ya 274.
Katika
hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete, amewataka Watanzania kupuuza watu
wachache wanaodai kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, na badala yake
wajiandae kuipigia kura ya kuikubali wakati ukiwadia.
Rais
Kikwete alitoa ushauri huo kwa nyakati tofauti juzi kwa wananchi mkoani
Mwanza ambako yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu, kukagua na
kuzindua miradi ya maendeleo.
“Watakuja
watu kuwashawishi kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, wasikilizeni
lakini tumieni akili yenu, kama ile hadithi ya mbayuwayu. Jiandaeni tu
kupiga kura na kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa kwa sababu hii ni
Katiba nzuri sana,” alisema Rais Kikwete.
Alishangaa watu wanaodai kuwa Katiba Inayopendekezwa ni mbaya, akiuliza kuwa kama Katiba hiyo ni mbaya basi hiyo nzuri ikoje?
Aliisifu Katiba Inayopendekezwa kwa kujali makundi yote ndani ya jamii na kusisitiza kwamba kamwe haiwezi kuwa Katiba mbaya.
“Sijui
Katiba nyingine duniani ambayo inajadili makundi yote ndani ya jamii
kama hii Katiba Inayopendekezwa. Hakuna aliyeachwa – wavuvi wamo, wajane
wamo, wafanyabiashara ndogo wamo, akinamama lishe wamo, wakulima wamo,
wafungaji wamo….kila mtu yumo. Akinamama ndio usiseme kabisa wao
wamepata hata asilimia 50 kwa 50 ndani ya Bunge,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza
Rais Kikwete: ”Hivi katiba mbaya inakuwa kama inayopendekezwa na kama
hii inayopendekezwa ni mbaya sasa hivi nzuri ikoje?”