HOFU KUBWA YATANDA MBEYA:Samaki wazua hofu.
Samaki wazua hofu, taharuki Mbeya
Moja ya mitumbwi ya wavuvi katika Ziwa Nyasa. Picha ya Mtandao.
Taarifa za kuingizwa kwa samaki wanaodaiwa kuwa walikufa kwa sumu kwenye
masoko mbalimbali wilayani Kyela, Rungwe na Mbeya zilitolewa jana kwa
mtandao na baadaye kutolewa tamko na viongozi wa Serikali.
Mitandao hiyo ilisambaza ujumbe uliosomeka:-
Taarifa kwa watumiaji wa samaki: “Wilaya ya Kyela imepiga marufuku
uingizaji na utumiaji wa samaki kutoka Ziwa Nyasa (Malawi) kuanzia leo
tarehe 13.01.2015 hadi tamko lingine litakapotolewa. Hatua hii imekuja
baada ya kupatikana taarifa toka Malawi kwamba wananchi wamezuiwa
kutumia samaki wa ziwa hilo baada ya kugundulika majitaka yenye sumu
kutoka mgodi wa machimbo ya uranium wa Kailekera uliopo Karonga na
kuingia kwenye ziwa na kusababisha vifo vya samaki ambao wanaingizwa
nchini kwetu na kuuzwa kwa bei rahisi kwa upande wa Tanzania. Sampuli
itachukuliwa kwa uchunguzi. Tahadhari ichukuliwe kwa watumiaji wa
samaki. Acheni kuagiza mbasa kwa muda huu.”
Samaki hao wanadaiwa kuanza kufa tangu Januari 10 nchini Malawi na kwa
upande wa Tanzania wameonekana tangu Januari 11 na kwamba hivi sasa wapo
wanaoelea majini kana kwamba wameanikwa.
Taarifa hiyo ilizua hamaki na taharuki kwa wananchi ambako msaidizi wa
mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliyetajwa kwa jina la Marco Masaya
alipoulizwa kama wanayo taarifa ya kuzagaa kwa samaki hao alijibu kuwa
ni kweli.
Alisema bosi wake alikuwa ameshapata taarifa hizo na kwamba alimwelekeza
Mkuu wa Wilaya ya Kyela (DC), Margreth Malenga mambo ya kufanya kwa
haraka ili kuepusha madhara kwa wananchi.
Hata hivyo, DC Malenga alipopigiwa simu alikataa kuzungumza suala hilo
kwa simu, akisisitiza kwamba yeye amejiwekea utaratibu wa kuzungumza na
waandishi ana kwa ana.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kyela, Clement Kasongo
alipopigiwa simu kuhusu suala hilo alisema ni kweli wamewakuta samaki
mpakani mwa nchi hizo na kwamba wamechukua sampuli watazipeleka kwa
Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kupimwa kubaini sababu za kufa
kwao.
Aliongeza kuwa Serikali imezuia watu wasile samaki hao mpaka majibu yatakapotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mkazi wa Kasumulu, Kyela, Hebron Mwakapeja alipoulizwa kama amewaona
samaki kwa wingi, alisema tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, makundi ya
watu yanaelekea ziwani wanakosomba samaki kwa wingi na kuwauza kwa bei
ya ndogo.
Alisema watu wengi wamepigwa butwaa kutokana na samaki hao kupatikana wakielea majini kwenye ziwa hilo.
“Siyo kawaida kwa samaki wa Ziwa Nyasa hasa mbasa ambao siku zote huuzwa
kati ya Sh15,000 hadi Sh25,000 kwa samaki mmoja kuuzwa kuanzia Sh5,000
hadi Sh8,000,” alisema.
Naye Anna Kapeje wa Itunge alipoulizwa kuhusu samaki hao alisema makundi
ya watu yalihamia kwenye ziwa kuokota samaki kwa siku tatu zilizopita.
Mkazi wa Karonga nchini Malawi, Kassim Chimwemwe alipopigiwa simu
alisema ni kweli samaki walikufa wengi ziwani tangu Januari 7 baada ya
bomba la maji machafu lililopo kwenye kiwanda kupasuka na kumwaga maji
yake ziwani.
Alisema Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi alifika eneo la tukio na
kutoa siku 10 ili sampuli za samaki waliokufa zichukuliwe kwa uchunguzi.
MWANANCHI