BAADA ya msimu mmoja wa kuwa nje, hatimaye mlinda mlango mkongwe Tanzania, Juma Kaseja Juma amerudi kazini baada ya jana kusaini Mkataba wa miezi sita kujiunga na Mbeya City FC.
Kaseja amekuwa mchezaji huru tangu aondoke Yanga SC msimu uliopita- ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu arejee Jangwani akitokea klabu aliyoichezea kwa miaka tisa, Simba SC.
Kaseja alijiunga na Simba SC mwaka 2002 akitokea Moro United kabla ya mwaka 2009, kuhamia Yanga kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea Msimbazi mwaka 2010.
Akiwa Simba SC, Kaseja aliiwezesha klabu hiyo kutwaa jumla ya mataji saba, matano ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika misimu ya 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 2012 na matatu ya Tusker, mwaka 2003 na 2005 mawili ya Tanzania na moja la Kenya.
Katika msimu wake wa kwanza, 2003 Simba SC, Kaseja ndio alifanya makubwa zaidi, kwanza akiifikisha timu hiyo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda ikifungwa na SC Villa 1-0, bao pekee la Mkenya Vincent Tendwa, pasi ya kiungo Mtanzania, Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Baadaye mwaka huo akaiongoza Simba kufuzu hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa Afrika, ikiitoa timu ngumu, Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi, akifanya kazi kubwa ya kupangua mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1 katika mechi zote mbili.
Akiwa na Yanga SC pia alitwaa taji la Ligi Kuu Bara mwaka 2009, wakati katika timu ya taifa, Kaseja alitwaa Kombe la Challenge mwaka 2010.
Kaseja arudi kwa kishindo Mbeya City
Reviewed by
Unknown
on
12:55 AM
Rating:
5