Header Ads

Majimbo matano yavuruga Ukawa

Mikoani. Siku chache baada ya vyama vinavyounda Ukawa kutangaza mgawanyo wa majimbo, baadhi ya majimbo hayo yamekumbwa na sintofahamu baada ya wanachama kutokubaliana na uamuzi ya viongozi wa kuachiana majimbo.

Vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani kwa kuangalia, pamoja na mambo mengine, chama chenye nguvu kwenye jimbo husika na kura za uchaguzi wa mwaka 2010.
Tayari Chadema na CUF vimeshatoa orodha ya majimbo vitakavyosimamisha wagombea wake na kuacha baadhi, ambayo yameibuka kutoelewana baina ya uongozi wa juu na wa wilaya.
Moja ya majimbo ambayo hayakuwekwa kwenye orodha ya mgawanyo ya Chadema iliyotolewa mapema wiki hii ni Ngara ambayo iliachiwa NCCR-Mageuzi, lakini uongozi wa wilaya wa chama hicho kikuu cha upinzani umesema utasimamisha mgombea.
Mwenyekiti wa Chadema wilayani Ngara, Kennedy Staford amesema Kamati Kuu ya Ukawa imewachanganya wananchi wa jimbo hilo kutokana na uamuzi huo wa kuipa NCCR-Mageuzi nafasi ya kusimamisha mgombea.
Staford alisema kitendo cha kuipa jimbo hilo NCCR-Mageuzi bila viongozi wa wilaya kushirikishwa ni kuwakatisha tamaa wanachama kuendelea kuunga mkono Ukawa kupitia Chadema.
Alisema chama kilichopendekezwa kusimamisha mgombea hakina wanachama na wafuasi wanaoweza kutoa ushindani kwa mgombea wa CCM. “Jimbo la Ngara tulishafanya mchakato wa kumpata mgombea aliyepigiwa kura za maoni na tayari amechukua fomu ya kuwania jimbo kupitia chama chetu,” alisema Staford.
Majimbo yaliyotangazwa na Chadema kusimamisha mgombea katika Mkoa wa Kagera ni pamoja na  Karagwe, Kyerwa, Bukoba Mjini, Muleba Kaskazini, Biharamulo na Muleba Kusini.
Wakati hayo yakitokea Ngara, Ukawa wilayani Kakonko pia imeingia katika mvutano baada ya baadhi ya vyama shirika kuweka wagombea wake kuwania ubunge kwa Jimbo la Buyungu na kukiuka makubaliano. Hali hiyo imejitokeza baada ya Samso Bilago kuchukua fomu ya kuwania ubunge kwa tiketi ya Chadema na kusababisha wasiwasi kwa wananchi kutokana na jimbo hilo kuachwa kwa NCCR-Mageuzi ambayo mgombea wake Mawazo Atanasi pia amechukua fomu.
Akizungumzia hali hiyo, katibu wa CUF jimboni humo, Odasi Kalimanzila alisema msimamo wa Ukawa haujavunjika licha ya kwamba kuna baadhi ya vyama ambavyo vimeonekana kwenda kinyume na makubaliano. Hata hivyo, katibu wa NCCR-Mageuzi wilayani Kakonko, Marco Bajora alisema bado kuna changamoto kubwa katika umoja huo, na kwamba wanachosubiri ni uamuzi wa wananchi kumchagua kiongozi atakayefaa katika kuleta maendeleo.
Ester Bulaya azua balaa
Wakati huohuo, aliyekuwa mshindi wa kura za maoni Bunda Mjini wa Chadema, Pius Masururi ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM huku mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Imanani  na wanachama 50 wakiwamo viongozi wakijivua uanachama.
Masururi, aliyepata kura 65 mbele ya wapinzani wake wa karibu, Magembe Makoye (40) na Ester Bulaya (37) katika kura za maoni zilizopigwa Julai 29 mwaka huu, ametangaza uamuzi wake huo jana kupitia kituo cha redio cha Mazingira FM cha mjini Bunda.
Masururi amesema ameamua kukihama chama hicho baada ya kutofurahiswa na kitendo cha Kamati Kuu ya Chadema kupuuza uamuzi wa wanachama kwa kukata jina la aliyeshinda kura za maoni.
Katika jimbo la Bunda Mjini, Chadema imebadilisha matokeo na kumteua mshindi wa tatu, Ester Bulaya kupeperusha bendera ya chama hicho, jambo lililowaudhi baadhi ya makada wake.
Baadhi ya wanachama walioongozwa na mwenyekiti wa jimbo hilo, Samuel Imanani wamesema kitendo cha makao makuu ya Chadema kutengua uamuzi wa kura zao za maoni ni udhalilishaji mkubwa, hivyo hawana budi kukihama chama hicho. “Tumeamua kuuachia uongozi wa makao makuu uendeshe mambo yote, nasi tusiwe tena wanachama maana hautusikilizwi,” alisema Mashaka Kipili mmoja wa wanachama hao.
Katika tukio jingine, aliyekuwa mbunge Mbarali kupitia CCM, Dickson Kilufi amekumbana na vikwazo kwenye chama chake kipya cha Chadema  baada ya uongozi wa wilaya  kusema hauna taarifa za kutaka agombee ubunge wa jimbo hilo.
Mwenyekiti wa Chadema wilayani Mbarali, Peter Mwashiti alisema taarifa za Kilufi kujiunga Chadema anazisikia kwenye vyombo vya habari na mitaani na kwamba suala la kutaka agombee ubunge halipo kwa vile tayari alishapitishwa Liberatus Mwang’ombe kuwa mgombea wa jimbo hilo.
‘‘Kama amejiunga na Chadema, tunamkaribisha, lakini kibaya ni kwamba hajawahi kuwasiliana na kiongozi yeyote wa Chadema Wilaya ya Mbarali na cha kushangaza tunasikia ameanza kujitangaza eti kateuliwa kugombea ubunge kwa tiketi ya Chadema. Sisi tuna mgombea wetu na ameshachukua fomu pale halmashauri,” alisema.
Kilufi alipoulizwa kuhusu hoja hizo, alisema aliteuliwa na viongozi wa kitaifa wa Chadema kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye ubunge wa Jimbo la Mbarali.
Wakati mgogoro huo ukiendelea, mwenyekiti wa CCM Mbarali, Mathayo Mwangomo amesema Kilufi alikuwa mzigo ndani ya chama hicho hivyo wanashukuru kujiengua kwake na kujiunga na Chadema.
Pia, Kilufi alijitetea kuwa hakuwa mzigo, bali mzigo ni viongozi wa CCM ambao alidai wanapenda rushwa.
Wafuasi wa Chadema, Kata ya Forest Mbeya waliandamana hadi katika ofisi  za wilaya za chama hicho wakipinga shinikizo la uongozi wao kutaka aliyekuwa diwani, Boyd Mwabulanga achukue fomu za kuwania tena nafasi hiyo.
Mwanachama wa chama hicho aliyejitambulisha kwa jina la Mwamakamba, alisema anashangazwa na kitendo cha baadhi ya viongozi kutumia mbinu za kiujanja ujanja kutaka Mwabulanga agombee tena badala ya Henry Mwakikambu aliyeshinda kura za maoni.
Viongozi wa wilaya walilazimika kuwatuliza wandamanaji hao kwa kuwaeleza kwamba kaimu katibu mkuu  wa Chadema, John Mnyika aliruhusu Mwakikambaku achukue fomu haraka na kuapishwa mahakamani ili agombeee nafasi hiyo. Pia, katika Jimbo la Handeni Mjini vyama vya CUF na Chadema vimesimamisha wagombea ubunge licha ya mgawanyo wa majimbo hayo kuonyesha kuwa CUF ndiyo kimeachiwa nafasi hiyo.
Katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Zaharia Yohana alisema ni kweli wamesimamisha wagombea ubunge na udiwani katika majimbo yote pamoja na kata zote Handeni Mjini na Vijijini ili kushiriki uchaguzi mkuu.
Kuhusu mchakato huo kukiuka makubaliano ya vikao vya Ukawa, alisema hawezi kulizungumzia hilo bali anafuata maelekezo ya viongozi wake.
Powered by Blogger.