Header Ads

TAIFA STARS KWENDA OMAN, UTURUKI BILA YA NGASSA, SAMATTA


Kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kinachonolewa na kocha, Boniface Mkwasa, Jumamosi ya wiki hii, kinatarajia kwenda nchini Uturuki kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Nigeria utakaopigwa Septemba 5, mwaka huu.

Kikosi hicho cha Stars kitaenda nchini Uturuki kwa kupitia Oman ambapo kitacheza mchezo wa kirafiki na timu ya taifa ya nchi hiyo, lakini kitawakosa nyota wake wanaocheza soka la kimataifa kutokana na wachezaji hao kubanwa na majukumu ya klabu.

Msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, ameliambia Championi Jumatano kuwa, kikosi hicho kitaondoka hapa nchini kikiwa na jumla ya wachezaji 22, watakaoitwa na Mkwasa.

“Kikosi chetu cha Taifa Stars wikiendi hii kitaondoka hapa nchini na kwenda Uturuki kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria ambao utapigwa katika Uwanja wa Taifa, Dar, Septemba 5, mwaka huu.

“Lakini kikosi hicho ambacho kitaundwa na wachezaji 22, kitawakosa nyota wanaocheza soka la kimataifa, Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao wamebanwa na majukumu ya klabu ila wataungana na timu pale itakaporejea hapa nchini,” alisema Kizuguto.
Powered by Blogger.