TAIFA STARS KUIKABILI NAMIBIA HUKO WINDHOEK!
>>30 TWIGA STARS WAITWA KUIVAA ZAMBIA
>>RAMBIRAMBI MSIBA WA KANALI MMARI
>>MAOFISA TFF KUKAGUA VIWANJA 19 VYA VPL, FDL
>>RAIS MALINZI KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI LEO
Release No. 005
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Januari 14, 2014
30 TWIGA STARS WAITWA KUIVAA ZAMBIA
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian 
Kaijage ametaja kikosi cha wachezaji 30 wanaoingia kambini kesho 
(Januari 15 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi dhidi ya
 Zambia mwezi ujao.
Mechi hiyo ya kwanza ya mchujo kuwania 
tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika 
baadaye mwaka huu jijini Windhoek, Namibia itafanyika jijini Lusaka.
Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho 
ni Amina Ally (Lord Baden Sekondari), Amisa Athuman (Marsh Academy), 
Anastazia Anthony (Lord Baden Sekondari), Asha Rashid (Mburahati 
Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar) na Belina Julius (Lord Baden 
Sekondari).
Donisia Daniel (Lord Baden Sekondari), 
Esther Chabruma (Sayari Queens), Evelyn Sekikubo (Kwimba Chuoni), Fatuma
 Bushiri (Simba Queens), Fatuma Hassan (Mburahati Queens), Fatuma Issa 
(Evergreen) na Fatuma Mustapha (Sayari Queens).
Fatuma Omari (Sayari Queens), Happiness 
Hezron (Copa Coca-Cola Ilala), Maimuna Hamisi (U20 Tanzanite), Maimuna 
Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Real Tanzanite), Mwapewa Mtumwa (Sayari 
Queens), Najiat Abbas (Makongo Sekondari) na Neema Paul (U20 Tanzanite).
Pulkeria Charaji (Sayari Queens), Semeni
 Abeid (Real Tanzanite), Shelder Boniface (Makongo Sekondari), Sophia 
Mwasikili (Sayari Queens), Theresa Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa 
(Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).
RAMBIRAMBI MSIBA WA KANALI MMARI
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania 
(TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mwanzilishi wa wa timu ya Oljoro
 JKT, Kanali Mmari kilichotokea jana (Januari 13 mwaka huu) jijini Dar 
es Salaam.
Kanali Mmari ambaye aliasisi timu hiyo 
na kuifikisha hadi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom amefia Hospitali ya Taifa 
Muhimbili (MNH) ambapo alikuwa amelazwa baada ya kupata ajali ya gari 
Chalinze mkoani Pwani, Januari Mosi mwaka huu.
Msiba huu ni mkubwa kwa jamii ya mpira 
wa miguu kwani mbali kuasisi timu ya Oljoro JKT alikuwa mhamasishaji 
mkubwa wa mchezo huo mkoani Arusha, hivyo mchango wake tutaukumbuka 
daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu
 Kanali Mmari, klabu ya Oljoro JKT, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA) na kuwataka kuwa na 
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
MAOFISA TFF KUKAGUA VIWANJA 19 VYA VPL, FDL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania 
(TFF) limeteua maofisa wanaoanza leo (Januari 14 mwaka huu) kukagua 
viwanja 19 vitakavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na 
Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Ukaguzi huo pia unahusisha viwanja 
ambavyo Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilizuia mechi za VPL na FDL 
kuchezwa mpaka hapo vitakapokuwa vimefanyiwa marekebisho ili kukidhi 
sifa za kutumiwa kwa mechi hizo.
Viwanja vinavyokaguliwa ni Ali Hassan 
Mwinyi (Tabora), CCM Kirumba (Mwanza), Jamhuri (Dodoma), Jamhuri 
(Morogoro), Kaitaba (Bukoba), Kambarage (Shinyanga), Kumbukumbu ya 
Karume (Musoma) na Kumbukumbu ya Samora (Iringa).
Kumbukumbu ya Sokoine (Mbeya), Lake 
Tanganyika (Kigoma), Mabatini (Pwani), Majimaji (Songea), Mbinga 
(Mbinga), Mkwakwani (Tanga), Mwadui (Shinyanga), Wambi (Mufindi, 
Iringa), Sheikh Kaluta Amri Abeid (Arusha), Umoja (Mtwara) na Vwawa 
(Mbozi).
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa husika na mameneja wa viwanja husika wanatakiwa kuwapa ushirikiano wakaguzi hao kutoka TFF.
RAIS MALINZI KUFUNGA SEMINA YA WAAMUZI LEO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu 
Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atakuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa 
semina ya waamuzi na makamisha leo (Januari 4 mwaka huu) saa 4 asubuhi 
kwenye ukumbi wa mikutano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi zaidi ya 100 na makamishna 50 
wameshiriki katika semina hiyo. Makamishna hao ni baadhi ya wale 
wanaosimamia mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza
 (FDL) wakati waamuzi ni wale wa daraja la kwanza (class one) ambao 
ndiyo wanaochezesha mechi za VPL na FDL.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania 
(TFF) linatarajia kuandaa semina nyingine baadaye mwaka huu kwa 
makamishna wapya wanaotaka kusimamia mechi za VPL na zile za FDL.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
+++++++++++++++++++++++++++++++++
Release No. 006
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Januari 14, 2014
TAIFA STARS KUIKABILI NAMIBIA FIFA DATE
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) 
itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Namibia (Brave Warriors) ikiwa ni 
sehemu ya maandalizi ya michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za
 Afrika (AFCON) zitakazochezwa mwakani nchini Morocco.
Stars na Brave Warriors zitacheza mechi 
hiyo Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Namibia. Mechi hiyo ipo katika 
kalenda ya mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa 
Miguu (FIFA).
Makubaliano ya kucheza mechi hiyo 
yamefikiwa kutokana na mazungumzo kati ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa
 Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu
 Namibia (NFA), John Muinjo.
Benchi la Ufundi la Brave Warriors 
linaongozwa na kocha mzawa Ricardo Mannetti, na mechi hiyo itachezwa ama
 Uwanja wa Sam Nujoma au Uwanja wa Uhuru jijini Windhoek.
Taifa Stars inayodhaminiwa na 
Kilimanjaro Premium Lager inafundishwa na kocha Kim Poulsen kutoka 
Denmark na inatarajia kuanza kucheza mechi za mchujo za AFCON Septemba 
mwaka huu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
 
 
 
 
 
 
