PINDA AIASA JUMUIYA YA UMOJA WA WAZAZI NCHINI Lazima iwe na kitu cha kujivunia
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Jumuiya ya Wazazi nchini ni miongoni mwa
jumuiya inayoongoza na kusimamia masuala yote yanayohusu elimu, malezi
bora kwa vijana wa taifa letu hivyo lazima iangalie jinsi ya kuweza
kujipambanua katika utekelezaji wa Umoja wa Jumuiya yao.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumamosi,
Februari 22, 2014), wakati akifungua rasmi semina ya siku tatu ya
viongozi na watendaji wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ngazi ya Taifa,
Mikoa na Wilaya Tanzania inayofanyika kwenye Ukumbi wa NEC, Mkoani
Dodoma.
Akizungumza
katika ufunguzi huo, Waziri Mkuu Pinda aliwaeleza wana jumuiya hao
kuangalia malengo wanayojipangia aidha yawe ya muda mfupi au mrefu ili
kuyatekeleza kwa kuzingatia yale mambo ya msingi na yenye kipao mbele
kwa wananchi.
“Changamoto kubwa iliyopo mbele yenu kama viongozi na watendaji wakuu wa Jumuiya hii ni namna ya kutimiza malengo mliyojiwekea“.
Alisema,
dhana ya Jumuiya ya Umoja wa Wazazi nchini ni kuongeza na kuboresha
masuala yote yanayohusu Sekta ya elimu hapa nchini: ‘‘Tumieni semina hii
kujipima kwamba mmefikia wapi katika utelelezaji wa malengo yenu kwa
kuangalia mapungufu na maboresho katika jumuiya yenu‘‘.
Jumuiya
ya Wazazi ndio magwiji mnaoongoza kwa kuwa na shule nyingi hapa nchini,
hivyo jumuiya yenu ijipange na kusimamia vema shule hizo ili kuwa
vinara katika kuboresha masuala ya elimu hapa nchini. Akitoa mfano,
alisema: “Kwanini shule za binafsi zinakuwa zinaongoza kuliko shule
zilizopo ndani ya Jumuiya yenu, walau katika kumi bora iwepo shule moja
kutoka Jumuiya ya Umoja wa Wazazi alisema Waziri Mkuu”.
Kutokana
na kauli hiyo, Waziri Mkuu aliiambia Jumuiya hiyo kutumia dhana ya
elimu kama ngao yao katika kuleta maendeleo katika Sekta hiyo kwani
Ilani ya chama cha Mapinduzi imetamka wazi kuongeza kasi ya upanuzi wa
Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari lengo ambalo ni moja ya jukumu kuu
la msingi la Jumuiya ya Umoja wa Wazazi.
Aliendelea
kusema kuwa Jumuiya ya Wazazi inajukumu la kusimamia masuala yote
yanayohusu maadili, jukumu ambalo halina tofauti sana na jukumu la
madhehebu ya dini kuzungumza bayana masuala ya malezi ya watoto na
vijana ambayo yamekuwa yakiporomoka kila kukicha, hivyo Waziri Mkuu
alisema, jumuiya hii itumia jukumu na nafasi waliyopewa kuhakikisha
watoto wote walio ndani na nje ya jumuiya wanafundishwa maadili.
Waziri
Mkuu aliendelea kusema kuwa, Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ina majengo,
viwanja na ardhi inayofaa kwa kilimo na shughuli za kiuchumi, tumieni
fursa hizi kwa kujenga vyuo, kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo
itawasaidia katika kuongeza kipato katika jumuiya yenu.‘‘Mnachotakiwa ni
kupanga bajeti zenu vizuri na kusimaia utekelezaji pamoja kusimamia
vizuri miradi na fursa zinazojitokea“
Pamoja
na hayo, Waziri Mkuu aliiomba Jumuiya ya Wazazi kujitokeza kuzungumzia
masuala ya Dawa za Kulevya kwa kusema kuwa, wako vijana ambao
wametumbukia katika dimbwi la Dawa za Kulevya ambaa pia wanahatarisha
maisha yao kwa kupata UKIMWI: “Ni matumaini yangu kwamba Jumuiya ya
Umoja wa Wazazi itakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii, kutoa ushauri
kwa vijana kuhusu athari za dawa za kulevya, UKIMWI na hata mkiweza
kuanzisha vituo vya ushauri”, alisisitiza Waziri Mkuu.
“Ili
kuweza kuwa na Jumuiya ya Wazazi imara ni dhahiri kuwa wanajumuiya
wasimamie kanuni na maadili yanayoongoza jumuiya yao kwa kuwaasa kuacha
kujiingaza katika makundi yasiyokuwa na msingi hasa kwa kutanguliza
maslahi ya fedha katika kupata nafasi za uongozi katika kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mkuu ambao huleta migawanyiko kati ya Viongozi na
wanachama na wapiga kura”. Mzingatie masuala yanayohusu kujenga na
kukuza utekelezaji wa jumuiya yenu ambayo itawasaidia kujenga jumuiya
imara na kujenga chama imara kitakacho leta viongozi imara”alisisitiza
Waziri Mkuu.
Mapema,
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi Taifa, Bw. Majura Bulembo,
alisema lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo na kuwaongeza ufanisi
Jumuiya ya Wazazi katika utekelezaji kazi zao na kuwasisitiza
kuhudhuria semina hiyo ipasavyo ili kuweza kukumbusha mapungufu na
changamoto zinazojitokeza katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi
mkuu.
“Viongozi
wamekuwa wakitumia vibaya nafasi za uongozi walizopewa kwa kujiona wao
ndio viongozi wakuu kwa kujifanyia maamuzi yao, viongozi kama hao
wataondolewa madarakani mara moja”.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAMOSI, FEBRUARI 22, 2014.