CHAMA KIPYA CHA ACT CHASHUSHA BENDERA ZA CHADEMA HUKO KIGOMA,WANACHAMA 3,500 WA CHADEMA WAJIUNGA NACHO
Chama
cha Alliance For Change and Transparency Mkoa wa Kigoma,kimeshusha
Bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA tawi la Ujiji
stendi ya zamani na kupandisha bendera ya (ACT) wakati wa uzinduzi rasmi
wa matawi sita katika manispaa ya kigoma ujiji .
Akizungumza
na wananchi wa eneo hilo, Katibu wa ACT Mkoa Athuman Kabogo alidai
lengo la kushusha bendera hiyo ni hatua ya kukataa kugeuzwa kuwa
vibaraka wa watu wengine kwa kukosa haki ya kuhoji na kuwania nyadhifa
za chama hicho na hivyo kuanzisha ACT kama chama cha wanyonge kinachoweza kuwasikiliza na kutoa haki kwa kila mmoja.
Kabogo
aliwataka wanachama wahitaji, wachukue kadi za ACT ili chama kipate
usajili kamili kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu husika pamoja na
kutoa michango endelevu ,ikiwa ni jitihada za makusudi kuhakikisha chama
kinasonga mbele kwa maslahi ya Taifa.
“Wananchi
nyie ni chachu ya chama kuwepo kwenye mchakato wa uchaguzi mdogo wa
wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kukiamini na kukipatia ridhaa kiweze
kuleta mabadiliko ya kimaendeleo” alisema Juma Ramadhan aliyekuwa katibu kampeni wa CUF kigoma.
Kwa
upande wa Katibu ACT Kanda Magharibi Wiston Moga alisema, lengo la
chama ni kuleta mabadiliko kwenye ulingo wa siasa,ambapo wao
wamedhamiria kutetea maslahi ya umma kwa lengo la kuondoa mfumo wa
maslahi binafsi ambayo ni chachu ya vyama vya siasa kushindwa kuleta
mabadiliko chanya kwa wananchi.
Katika
ziara hiyo ya uzinduzi wa matawi ya chama husika,ACT kimefanikiwa
kufungua matawi kwenye kata sita kati ya kata 19 zilizopo katika
manispaa ya kigoma ujiji,huku baadhi ya viongozi kutoka UPD,CHADEMA na
CUF wakijiunga na chama hicho.kwa kudai wanahitaji chama chenye uchungu na kukabiliana na changamoto za wanyonge.
Hata
hivyo wanachama 3500 wa chama cha Democrasia na Maendeleo Chadema
katika tawi la Ujiji mkoani Kigoma wamehamia chama kipya cha Alliance
For Change and Transparency (ACT).