BASATA YABARIKI TAMASHA LA PASAKA.
BARAZA la Sanaa la Taifa
(BASATA) mwishoni mwa wiki iliyopita lilikabidhi kibali kupitia Katibu
Mtendaji wa baraza hilo, Godfrey Mngereza kwa ajili ya uendeshaji wa Tamasha la
Pasaka linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotions ya
jijini Dar es Salaam.
Tamasha
hilo ni muendelezo wa Tamasha la Pasaka lililoasisiwa tangu mwaka 2000 likiwa
na lengo la kumtukuza na kumtumikia Mungu kupitia nyimbo mbalimbali za waimbaji
wa Tanzania na nje ya nchi.
Akizungumzia
juu ya kupata kibali hicho,Mratibu wa tamasha hilo ambaye pia ni
mjumbe wa BASATA,Bwan Alex Msama, alisema kuwa kibali kilitolewa
wiki iliyopita kwa ajili ya tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Aprili 20,
jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamia katika mikoa nane itakayochaguliwa
kufanyika kwa tamasha hilo kupitia mfumo wa upigaji kura kupitia ujumbe mfupi
wa maandishi.
Msama
alisema taratibu za maandalizi ya tamasha hilo zinaendelea ikiwa ni pamoja na
waimbaji kupigiwa kura na kufanya mazungumzo na wale watakaoshinda kwa kupigiwa
kura nyingi ndio watakaotumbuiza na pia kupata mahali litakapofanyika.
“Maandalizi
kwa ujumla yanaendelea vizuri kabisa, kibali kimepatikana kinachoendelea sasa
ni kwamba tumewapa nafasi watanzania wenyewe wachague mgeni rasmi na waimbaji wataoimba
katika tamasha la mwaka huu, kwa mgeni rasmi tunaomba waendelee kupiga kura kwa
wingi ili kuchagua mahitaji hayo,” alisema Msama.
Msama
amendelea kuwakumbusha watanzania namna ya kuwapigia kura waimbaji, mgeni rasmi
na mikoa ambako ukitaka kumpigia mwimbaji andika pasaka acha nafsi kisha andika
jina la mwimbaji unatuma kwenda namba 15327.
Pia kwa mgeni rasmi andika neno pasaka acha nafasi kisha andika jina la mgeni rasmi unayetaka kumpigia kura tuma kwenda 15327, wakati mikoa unaandika pasaka acha nafasi jina la mkoa unaotaka kuupigia kura tuma kwenda namba 15327 piga kura uwezavyo ili upate mwimbaji na mgeni rasmi na mkoa unaopenda tamasha lifanyike.