Hali ya Hewa yatabiri mvua za maafa pwani
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania (TMA), imetabiri kuwa mvua kubwa zitanyesha hasa maeneo
ya ukanda wa pwani huku ikitahadharisha uwezekano mkubwa kusababisha
maafa.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema
jana kuwa utabiri huo unaonyesha kuwa maeneo mengi zaidi ya nchi
yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani... “Hata shughuli za kilimo
zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo.”
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari TMA pia
imewahadharisha watumiaji wa bahari juu ya mabadiliko ya tabianchi
yanayoweza kusababisha bahari kuchafuka.
Taarifa hiyo imesema kunatarajiwa kuwapo kwa
vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50, kati ya jana na kesho
ambazo zitanyesha mfululizo na kwamba huenda zikasababisha madhara
katika ukanda wote wa pwani.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mvua hizo
zinasababishwa na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa Mashariki mwa
Bahari ya Hindi, sanjari na kusogea haraka kwa mvua za masika hivyo
kuongeza kiwango cha unyevunyevu kuelekea ukanda wa pwani.
Mikoa iliyopo katika ukanda huo ambayo inaweza
kuathiriwa na mabadiliko hayo ya hali ya hewa ni Mtwara, Lindi, Pwani,
Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar.
“TMA inazitaka mamlaka zinazohusiana na majanga
kuchukua hadhari zinazostahiki ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea
kutokana na mvua hizo,” ilisema taarifa hiyo.
Katika taarifa ya tathmini ya mvua za msimu
kuanzia Machi hadi Mei, mwaka huu iliyotolewa mwishoni mwa wiki
iliyopita, Mamlaka hiyo ilizitaka menejimenti za maafa na wadau wa sekta
ya afya, kuchukua hatua za hadhari kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi yanayoweza kutokea kwa kuwa baadhi ya maeneo yanatarajiwa
kupata mvua za juu ya wastani.