Sketi yamtia mashakani polisi Kenya
Afisaa mmoja wa polisi mwanamke
nchini Kenya amepewa onyo kali kwa kuvalia sketi iliyokuwa imembana
kiasi cha kuonyesha umbo lake.
Wakuu wake walichukua hatua ya kumuonya polisi
huyo baada ya picha yake kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na
kupigiwa gumzo kubwa.Alipigwa picha akiwa amevalia sketi yake fupi na yenye kumbana akiwa anashika doria katika eneo ambako mashindano ya magari yalikuwa yanafanyika eneo la Kati mwa Kenya.
Afisaa huyo kwa jina Linda Okello, alitakiwa kufika mbele ya mkuu wake James Mugeria na kuonywa vikali dhidi ya kuvalia hivyo kwa mara nyingine, kitendo ambacho alifahamishwa kuwa ni utovu wa nidhamu kwa kuvalia nguo isiyo ya heshima kwa polisi
Maafisa mjini Kiambu walisema kuwa kupewa onyo kwa afisa Linda na kuonywa dhidi ya kuvalia sketi yake iliyokuwa imembana sana ni jambo la kawaida na kwamba ameruhusiwa kuendelea na majukumu yake.
Waliongeza kuwa afisa huyo ameamrishwa kuanza kuvalia kiheshima.
Alipigwa picha na mwanahabari mmoja wa gazeti moja maarufu nchini Kenya akiwa na wenzake kazini mjini Kiambu. Lakini punde si punde picha hiyo ikaanza kusambazwa kwa mitandano ya kijamii na baadhi wakiikejeli.
Taarifa ya polisi huyo kuonywa ilizua hasira kwenye mitandao ya kijamii baadhi wakihoji ikiwa ni makosa kwa afisaa wa polisi kuvalia sketi ya kumbana. Nini Kauli yako?