Header Ads

Amini usiamini Malori yanaua maelfu, hakuna anayejali

Hakuna asiyejua kwamba malori katika barabara zetu ni tatizo kubwa. Wiki iliyopita, gazeti hili lilichapisha habari za uchunguzi uliofanyika katika sehemu mbalimbali nchini, ukionyesha jinsi malori mengi yanayosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi, yanavyosababisha ajali ambazo mpaka sasa zimeua maelfu ya watu, huku wengine wengi wakiachwa na vilema vya maisha. Inaonekana Serikali haijatambua ukubwa wa tatizo hilo.
Tunasema hivyo kwa sababu tatu kubwa; kwanza, ukiichambua hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa wiki iliyopita bungeni, utagundua kwamba Serikali inalifahamu tatizo la ajali za barabarani juujuu tu. Imebakia tu kuimba nyimbo zilezile za kuwataka madereva kuzingatia sheria za barabarani. Pili, takwimu zinazotolewa na Serikali zimepitwa na wakati na kwa kiasi kikubwa haziendani na takwimu za Kikosi cha Usalama Barabarani. Tatu, Serikali haina mkakati wa kupunguza ajali hizo isipokuwa imejivua jukumu hilo kwa kuagiza Jeshi la Polisi, Sumatra na Serikali za Mitaa 'kukaa pamoja ili kuweka mkakati wa kukabiliana na ajali hizo'.
Kwa maneno mengine, Serikali haitambui kwamba ajali nyingi za barabarani zinazosababisha vifo vya maelfu ya watu zinasababishwa na malori ya mizigo. Takwimu zinaonyesha kuwa, kati ya mwaka 2010 na Machi mwaka huu malori yalisababisha ajali 23,746 na kuua watu 2,413 na kuacha majeruhi 7,958. Mwaka 2010 pekee, zilitokea ajali za magari 24,665 na kuua watu 3,582. Kati ya hizo, ajali 3,134 zilisababishwa na malori na kuua watu 493 na kuacha majeruhi 1,926.
Mwaka 2011 kulitokea ajali 33,943 na kuua watu 3,981. Kati ya hizo, zilizosababishwa na malori ni 3,219. Mwaka huo malori yalisababisha vifo vya watu 506 na kuacha majeruhi 1,792. Wakati mwaka 2012 zilitokea ajali 33,115 na kuua watu 3,969, kati ya ajali hizo 3,559 zilihusisha malori na kuua watu 692, huku zikiacha majeruhi 1,877. Mwaka 2013 mambo yalikuwa yaleyale, kwani ajali 34,344 zilitokea na kuua watu 4,002. Kati ya hizo, ajali 3,561 zilisababishwa na malori na kuua watu 608 na kuacha majeruhi 2,075. Takwimu zinaonyesha pia kuwa, kati ya Januari na Machi, 2014, ajali 4,893 zimetokea na kuua watu 854. huku ajali 655 zikisababishwa na malori na kuua watu 114 na majeruhi 288.
Tumetoa takwimu hizo ili kuonyesha jinsi malori ya mizigo yalivyo janga. Tunaambiwa kwamba wamiliki wake wengi ni vigogo serikalini na katika sekta ya umma na pengine ndiyo maana usafiri wa reli ulikufa na juhudi za kuurejesha hazifanikiwi. Serikali inasema ni sikivu, lakini inashangaza kuona inakuwa kaidi linapokuja suala la kudhibiti malori hayo. Wakati tukisubiri kufufuliwa kwa usafiri wa reli, tunaishauri Serikali ijenge na kutenga sehemu maalumu za kuegesha magari hayo katika miji na barabara zote kuu.(E.L)
Powered by Blogger.