Header Ads

Mbowe, Lipumba, Mbatia hapatoshi



UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umeendelea kupingwa kila kona ya nchi huku viongozi wa umoja huo wakifananishwa na wanafiki katika ulingo wa kisiasa nchini.
Umoja huo unaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF chini ya wenyeviti wao, Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia.
Umoja huo umepingwa vikali na viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema kutoka mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu na Kagera na kubainisha kuwa hauvumiliki machoni mwa Watanzania.
Akisoma tamko la kulaani Ukawa kwa niaba ya viongozi wa mikoa hiyo mjini Geita jana, Mwenyekiti wa Makatibu wa Mabaraza ya Kanda ya Ziwa Magharibi, Fikiri Migiyo alisema
wanaungana na wajumbe wengine wa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Tanga kupinga Ukawa.

"Wanahabari itakubukwa kuwa chama chetu ni chama makini kinachoamini katika nguvu ya umma na si ya viongozi, sasa cha kushangaza hapa viongozi wetu wameendelea kutuburuza sisi wanachama na viongozi wa ngazi za chini bila kushirikishwa katika uamuzi wa chama.
"Kwa mfano kitendo cha ubabe wa mwenyekiti wetu (Mbowe) kuendelea kufikiri kwa niaba yetu na kufanya uamuzi pekee yake ni kutudhalilisha sisi kama viongozi na Watanzania.
"Tunalaani kwa nguvu zote kitendo cha viongozi wetu wa juu kufanya uamuzi wa kihuni kususia Bunge la Katiba na sasa hivi kuanza kutoa masharti ya kitoto kwamba ili warudi bungeni ni lazima yatekelezwe masharti hayo.
"Tunasikitishwa na unafiki huu uliiopitiliza, viongozi wetu wamekubali kuwa sehemu ya matapeli wa kisiasa, wamekwenda kwenye Bunge la Katiba wamekula posho zinazotokana na kodi zetu walala hoi, halafu wameacha kufanya walichotumwa,"alidai Migiyo.
Migiyo alidai kuwa kuanzisha Ukawa na kususia Bunge la Katiba ni muendelezo wa siasa za kinafiki, huo ni muendelezo wa mipango ile ile ya kuwahadaa Watanzania kupitia misimamo yetu isiyosadikika.
Alidai kuwa njia bora na nzuri  ni kupambana kupitia hoja, na wabunge wao walitakiwa  kupambana kupitia hoja na si kukimbia bungeni.
"Kuungana na washirika wa CCM, ambao ni CUF na NCCR-Mageuzi kwenye kufanya harakati hizi kunatupa wakati mgumu sisi wananchi na viongozi wa huku chini na tunaamini kwamba kama imewezekana kwa viongozi wetu kuungana na CCM B, kamwe haitashindikana siku moja Mbowe akituambia tuungane na CCM, na kwamba kwenye siasa hakuna adui wa kudumu.

"Kususia vikao vya Bunge la Katiba kwa sababu tu Serikali tatu zinakataliwa na CCM, ni kudhihirisha kiasi gani viongozi wetu hawa ni waroho wa madaraka na kwamba wanataka kuutumia mchakato huu wa Katiba Mpya kama ngazi yao ya kupata madaraka kiurahisi,"alidai.

Migiyo aliongeza kuwa,"viongozi wetu kwenye hili wameboronga na wanapaswa si tu kujiuzulu lakini pia wanachapwe viboko hadharani kwa kutusaliti na kuzisaliti nafsi zao".
Alidai kuwa huko mikoani idadi ya namba za Serikali si agenda ya msingi na kubainisha kuwa tatizo lao kubwa ni mbolea, tatizo la ajira kwa vijana na jamii kwa ujumla, migogoro ya mipaka, mkiundombinu, afya na nyingine za aina hiyo.
"Kama mmesusa kushiriki vikao vya kuandaa katiba nani atatusemea haya masuala kama kweli mnajiita Ukawa ni umoja wa katiba ya wananchi. Acheni unafiki kwa kuwashirikisha CUF na NCCR Kwenye kambi rasmi bungeni.
"Kuna viongozi wa chama ngazi mikoa na wilaya tuliwahi kuhoji pale viongozi wetu waliposema hatuwezi kuwashirikisha CUF na NCCR kwani wao ni CCM B na sisi tuliamini hivyo na kuona CUF na NCCR ni kikwazo kwetu...sasa tunashangaa leo bila hata kuja kwetu sisi kama viongozi na wanachama kuelezwa kilichoibadilisha CUF na NCCR ghafla kutoka kwa CCM B na kuwa wapinzani imara," alihoji.

"Tunalaani kwa nguvu kubwa ujanja ujanja huu wa kisiasa, hatuwezi kukubali kutumiwa kila siku na mabwana wakubwa hawa na sisi tuendelee kuwavumilia na kuwakalia kimya kila uchao, tunataka waache kuendelea kutufanya sisi viongozi wa chini kama mandondocha wa kisiasa kama walivyo wao," alidai Migiyo.  

Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alipoulizwa kuhusu kauli ya Migiyo alionesha kushangaa na kubainisha kuwa hafahamu cheo cha Mwenyekiti wa Makatibu wa Mabaraza ya Kanda ya Ziwa Magharibi, hivyo hana cha kuzungumza.
"Mimi siangalii jina bali ninaconcetrate kwenye cheo, hivyo kwa sababu hicho cheo sijawahi kukisikia sina la kuzungumza," alisema Makene.
Powered by Blogger.