Na Hudugu Ng'amilo Bukoba. Polisi wanamshikilia mganga wa jadi kutoka Kijiji cha Matera, Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza kwa tuhuma za kumnyonga mwanafunzi wa darasa la kwanza, Fausta Geofrey (8) na kukata viungo vyake na kuvibanika ili kupata dawa ya uganga. Anadaiwa kufanya mauaji hayo Mei 21 katika Kijiji cha Bisole, Kata ya Muhutwe, wilayani Muleba. Mtuhumiwa huyo anadaiwa kumkata mikono yote, masikio, ngozi ya mgongoni na sehemu za siri na kuvibanika. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga alisema mwanafunzi huyo akiwa na wenzake wawili saa 1:30 asubuhi alipita karibu na nyumba ya mganga wakielekea shuleni. Mayunga alisema mganga huyo alimwita na kumkaba shingo na mdomo ili asipige kelele kabla ya kumpeleka ndani ya nyumba alikomnyonga. Baada ya kukata viungo vyake, mtuhumiwa anadaiwa kuchimba shimo chini ya kitanda chake na kuuzika mwili. "Baada ya kumnyonga alikata mikono yote, masikio, sehemu za siri na sehemu nyingine kwenye mwili na kuanza kuvibanika ili vikauke aweze kutengeneza dawa ya uganga kwa wateja wake," alisema Mayunga. Aidha, Mayunga alisema kuwa mganga huyo amekuwapo kijijini hapo kwa zaidi ya mwaka mmoja. Alisema wazazi wa mwanafunzi huyo waliingiwa na hofu baada ya kufika saa 10:00 jioni bila kurejea nyumbani. "Baada ya kumsaka bila mafanikio, waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi ili kuomba msaada zaidi," alisema Kamanda Mayunga. Katika msako uliofanyika Jumapili Mei 22, polisi na wananchi walimtilia shaka mganga huyo baada ya kumhoji alikiri kufahamu alipo mtoto huyo na kuwaeleza kuwa alikuwa tayari amekufa. Kamanda Mayunga alisema mganga huyo aliwapeleka hadi nyumbani na kuwaonyesha vifaa alivyotumia kwenye mauaji. "Alituonyesha vifaa na alipomfukia mtoto huyo pamoja na viungo vilivyokuwa katika hatua ya ukaushwaji.Akihojiwa na gazeti hili, mganga huyo alidai amefanya mauaji hayo kutokana na hali ngumu ya maisha. Alisema maisha yalikuwa magumu zaidi baada ya wazazi wake kufariki na kuwaacha bila shamba akiwa na mdogo wake. "Ni kweli nimemuua, hali ya maisha ni ngumu nililazimika kufanya hivyo ili kutengeneza dawa ya bahati na dawa kwa wateja wangu," alisema mganga huyo. Mganga huyo alidai baada ya viungo hivyo kukauka, angetengeneza dawa za aina mbalimbali kwa ajili ya wateja wake, ikiwamo kuwachua wateja baada ya kuchanganya dawa nyingine. Alisema kuwa alilazimika kumuua mtoto mdogo kwa vile isingekuwa rahisi kumkamata mtu mzima na kumnyonga kama alivyofanya kwa mwanafunzi huyo. Alisema: "Kuna watu wameniagiza dawa ambayo ni lazima ifanyike kwa kutumia viungo vya mtu kama mikono, miguu, sehemu za siri na ngozi." Kamanda Mayunga alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kusikitisha. "Tunafanya uchunguzi kwa kumhoji zaidi mtuhumiwa pamoja na kwamba amekiri kuhusika na mauaji ya mtoto huyu," alisema Kamanda Mayunga.