Kuna wanamuziki ambao wamejipatia umaarufu mkubwa kupitia tasnia ya muziki, kwa kuufanya uvutie ndani na nje ya nchi. Vile vile wanamuziki hao wamedumu kwenye tasnia hiyo kwa zaidi ya miaka 40, miongoni mwa wanamuziki hao ni pamoja na Hamza Kalala, ambaye amewahi kupewa majina kadhaa kama vile mzee wa Madongo na Komandoo. Historia ya Kalala kwa ufupi Alizaliwa mkoani Tanga na kusoma shule za msingi na sekondari mkoani humo.(Martha Magessa) Baba yake Komando alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Reli, katika Stesheni ya Mpanda, ambaye baadaye alihamishiwa mkoani Tanga ambako alibahatika kuoa mke wa kabila la Kizigua, ambaye ndiye mama wa Komando Kalala. Mara baada ya Komando kuzaliwa alipewa jina la 'Kapesula,' akiwa ni mchanganyiko 'chotara' wa makabila ya Kinyamwezi na Kizigua. Komando Kalala alianza kuhamasika katika mambo ya muziki mwaka 1966 akiwa darasa la nne, wakati alipokuwa akimshuhudia baba yake akiimba na kucheza ngoma ya Kinyamwezi ya 'Manyanga' ambayo ilitokana na ngoma ya 'Hiyari ya Moyo', huko huko Tanga. Wakati huo wakata mkonge walikuwa wakifanya mashindano ya ngoma kati ya Wanyamwezi na ngoma za makabila mengine waliokuwa katika mashamba tofauti ya mkonge ya Kibaranga, Amboni na mengine mengi. Lakini ngoma ya 'Manyanga' ya Wanyamwezi na ile ya 'Sindimba' ya Wamakonde ndizo zilizokuwa zikitia fora katika mashindano hayo kila mara. Kalala anaeleza, hakufundishwa muziki na mtu bali ni kutokana na ngoma hizo alizokuwa akicheza na kuimba baba yake, na kumuiga kupiga gitaa mjomba wake ambaye alikuwa na gitaa nyumbani. Anasema alipima uwezo wake wa muziki alipokuwa kwenye bendi zilizokuwapo kwenye mashamba ya Mkonge kama Kwanduru Jazz Band, na Amboni Jazz. Hakuvutiwa na maisha ya mashambani hivyo alirudi Tanga Mjini, ambako aliendelea na mazoezi ya kupiga gitaa nyumbani kwao, siku moja alipita Mkongo mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina moja la Chivosha, akavutiwa kwa jinsi alivyokuwa akipiga gitaa na kumuomba ajiunge na bendi yao ya Villa Negro Successes. Anasimulia huku kote alikuwa anatoroka na baba yake hakuwahi kufahamu kama anaimba, alichelea kumwambia kwa kuogopa kukatishwa tamaa. CHANZO:MWANANCHI