2.
Mheshimiwa Spika, ninasimama mbele ya Bunge lako tukufu kwa mara ya
kwanza toka niteuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania,
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
Kwa hiyo kabla ya kuwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/2015, naomba
nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa heshima
hii kubwa. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais na Watanzania
wenzangu wote kwamba nitafanya kazi kwa bidii, uadilifu na kujituma kwa
uwezo wangu wote.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu nitoe pole zangu za dhati kwako
kufuatia vifo vya wabunge mahiri, Mheshimiwa Dkt. William Augustao
Mgimwa, aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kalenga na Waziri wa Fedha wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania; na Mheshimiwa Saidi
Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Chalinze. Mungu
azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
4.
Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kuwapongeza wabunge wenzangu ambao ni
wapya, Mheshimiwa Yusuf Salim Hussein, kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa
jimbo la Chambani; Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa kwa kuchaguliwa
kuwa Mbunge wa jimbo la Kalenga; na Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete
kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Chalinze. Ninawatakia kheri na
mafanikio katika majukumu yao mapya.
5.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee natoa pongezi na shukurani zangu
za dhati kwa Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mbunge wa jimbo la
Mpanda Mashariki, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa
hotuba yake ambayo imetoa mwelekeo wa ujumla wa shughuli za Serikali
kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
6.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii pia kutoa shukurani zetu za
dhati kwa Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria
na Utawala chini ya uongozi mahiri wa Mwenyekiti wake Mheshimiwa
William Mganga Ngeleja, Mbunge wa jimbo la Sengerema. Maoni, ushauri na
maelekezo yao yameiwezesha Wizara yangu kutekeleza majukumu yake kwa
mafanikio. Tutaendelea kuzingatia ushauri wa Kamati hii wakati
tukitekeleza malengo yetu kwa mwaka huu wa fedha na katika siku zijazo
kwa ujumla.
7.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu
wake Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani kwa kuiongoza vema Tume hiyo.
Ninawapongeza pia wajumbe wote kwa kazi kubwa waliyoifanya. Rasimu ya
Katiba waliyoiwasilisha imetuwekea msingi mzuri wa kujadili uandishi wa
Katiba mpya, jambo ambalo lina mchango wa pekee katika kujenga
mustakabali wa taifa letu. Ni matumaini yangu kwamba tutapata Katiba
bora itakayotuongoza kwa miaka mingi ijayo, itakayoimarisha umoja wetu
na itakayoleta utangamano wa kitaifa na ustawi wa nchi yetu.
B. MUUNDO NA MAJUKUMU YA WIZARA
8.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria inajumuisha Mahakama ya
Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Utumishi
wa Mahakama, Wakala wa Usajili, Ufilisi, na Udhamini (RITA), Taasisi ya
Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, na Chuo cha Uongozi wa Mahakama. Kwa
pamoja taasisi hizi ndizo zinazotekeleza majukumu ya Wizara kama
yalivyoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Namba 20 la mwaka 2010.
9.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuzingatia dira yake
ya upatikanaji haki kwa watu wote na kwa wakati, inasimamia na
kutekeleza majukumu yafuatayo: masuala ya kikatiba na kisheria;
shughuli za uendeshaji wa mashauri na utoaji haki; utekelezaji wa haki
za binadamu na utawala bora; shughuli za utafiti, urekebu na uandishi wa
sheria; kuishauri na kuiwakilisha Serikali katika masuala ya kisheria
ndani na nje ya nchi; shughuli za usajili, ufilisi na udhamini; kuratibu
taasisi za mafunzo zilizo chini yake na kusimamia maslahi na maendeleo
ya watumishi.
C. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2013/2014
10.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara yangu
ilitekeleza malengo iliyojiwekea ambayo ni yafuatayo: kuratibu mchakato
wa mabadiliko ya Katiba; kusikiliza na kuendesha mashauri nchini;
kusimamia masuala ya haki za binadamu na utawala bora; kutoa huduma za
kisheria; kuhakiki na kushiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali;
uandishi wa sheria na hati za Serikali; kufanya tafiti na tafsiri ya
sheria; kuendesha shughuli za usajili, ufilisi na udhamini; na kuratibu
mafunzo ya uanasheria kwa vitendo na uongozi wa Mahakama. Pia, Wizara
iliboresha miundombinu ya utoaji haki; ilitoa elimu na habari kuhusu
upatikanaji haki kwa jamii; iliratibu shughuli za maboresho ya Sekta ya
Sheria na kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika matumizi ya
rasilimali za umma. Utekelezaji wa majukumu hayo umefanyika kwa
mafanikio na viwango mbalimbali vya utekelezaji.
Kuratibu Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba
11.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na mfumo
imara wa sheria unaozingatia mahitaji ya wakati tulionao, Wizara ya
Katiba na Sheria ilisimamia na kuratibu mchakato wa kihistoria wa
kuandika Katiba. Tofauti na michakato miwili iliyopita (mwaka 1965 na
mwaka 1977), safari hii mchakato wa kuandika Katiba ulihusisha watu
wengi zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kwa kutoa maoni yao
mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba au kwa maandishi. Hali kadhalika
watashiriki kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba inayopendekezwa
kupitia kura ya maoni. Aidha, wananchi walipata fursa ya kupendekeza
majina ambayo Mheshimiwa Rais aliyazingatia katika kufanya uteuzi wa
wajumbe wa Tume.
12.
Mheshimiwa Spika, Tume hii ilifanya kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa
wananchi moja kwa moja na kupitia mabaraza ya Katiba ya wilaya na ya
kitaasisi. Baada ya zoezi hili Tume iliandaa Ripoti iliyojumuisha Rasimu
ya Katiba. Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, na Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
mnamo tarehe 30 Desemba, 2013.
13.
Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea Ripoti ya Tume, Mheshimiwa Rais
aliitisha Bunge Maalum ambalo lilianza kazi rasmi kwa kupokea Rasimu ya
Katiba iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba tarehe 18 Machi, 2014. Tume
ilihitimisha kazi zake na kuvunjwa rasmi kwa Tangazo la Serikali Namba
81 la tarehe 21 Machi, 2014.
14.
Mheshimiwa Spika, Bunge Maalum lilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais
tarehe 21 Machi 2014. Hadi sasa Bunge Maalum limefanya kazi ya kuandaa
Kanuni za kusimamia uendeshaji wa shughuli zake za kila siku. Aidha,
Bunge Maalum limejadili Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya
Katiba kama hatua za awali za uchambuzi wa Rasimu hiyo.
Kuimarisha Haki za Binadamu na Utawala Bora
15.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2013/2014 Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora imetoa elimu kwa umma katika masuala ya haki za
binadamu na utawala bora. Elimu iliyotolewa ilihusu sheria za ardhi na
umiliki wa mali, ambapo wananchi 8,529 kutoka katika kata 69 na Shehia 7
walifikiwa. Pamoja na kutoa elimu, Tume ilipokea malalamiko 923 ya aina
mbalimbali katika kipindi hicho yakiwemo yale yanayohusu migogoro ya
ardhi. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 324 yalishughulikiwa na
kutolewa uamuzi.
16.
Mheshimiwa Spika, Tume iliandaa Mwongozo wa Utawala Bora wenye lengo la
kukuza uelewa katika eneo hili. Jumla ya nakala 25,000 za Mwongozo huo
zilisambazwa kwa watendaji wa ngazi za vijiji na kata ili waweze
kuzingatia misingi ya utawala bora na haki za binadamu wakati
wanapotekeleza majukumu yao.
17.
Mheshimiwa Spika, hadhi ya Tanzania kuhusu haki za binadamu imeendelea
kuwa nzuri ndani na nje ya nchi yetu. Ni wajibu wa Wizara yangu kukuza
na kuendeleza mafanikio yaliyokwishapatikana. Wizara imekamilisha Rasimu
ya Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu hapa nchini
ambayo itawasilishwa kwenye Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu na
Watu. Taarifa hiyo inaeleza namna ambavyo Serikali yetu inatekeleza
mikataba mbalimbali ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukuza na
kulinda haki hizo.
18.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha 2013/2014, Wizara iliandaa Mpango
Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu (2013–2017) uliozinduliwa na Makamu
wa Rais Mheshimiwa, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 10 Desemba, 2013.
Wizara yangu ina wajibu wa kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mpango
Kazi huu katika taasisi kadhaa za umma na za kijamii. Kupitia Mpango huu
wadau mbalimbali watapata fursa ya kujadili na kutekeleza masuala ya
haki za binadamu. Pia ni fursa kwa Wizara kuimarisha usimamizi na
ufuatiliaji wa masuala mbalimbali yanayohusu haki za binadamu na utawala
bora.
19. Mheshimiwa
Spika, uzinduzi huo ulikwenda sambamba na uzinduzi wa Mpango Mkakati wa
Miaka Mitano wa Haki za Watoto (2013-2017). Mpango huo uliandaliwa
kutokana na tafiti mbili zilizofanywa juu ya upatikanaji haki kwa watoto
wanaokutana na mkono wa sheria na hali ya watoto wanaokinzana na
sheria. Matokeo ya tafiti hizo yaliwezesha kubaini vipaumbele vya
kimkakati ndani ya mkakati wenyewe na hatua madhubuti zinazopaswa
kuchukuliwa katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango
huo.
20. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu inaratibu shughuli za Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia
Mauaji ya Kimbari iliyoundwa chini ya Itifaki ya nchi za Maziwa Makuu ya
kuzuia mauaji ya kimbari. Kamati hii ina jukumu la kujenga uelewa na
kuishauri Serikali juu ya viashiria vinavyoweza kuathiri amani na
kusababisha vitendo vya ukatili kwa binadamu. Katika kipindi cha mwaka
2013/2014, pamoja na kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya amani
kupitia redio na luninga, Wizara imewajengea uwezo viongozi wa dini na
madhehebu mbalimbali katika kulinda amani katika mikoa ya Arusha, Mbeya,
Mwanza, Mjini Magharibi, Morogoro na Tanga. Katika mikoa hii, viongozi
wa dini waliunda Kamati za amani zenye wajumbe kutoka dini na madhehebu
mbalimbali. Kamati hizi zina jukumu la kuhakikisha amani inadumishwa
katika mikoa hiyo.
21.
Mheshimiwa Spika, katika uendeshaji wa shughuli zake, azma ya Serikali
ni kuongeza uwazi katika ngazi zote za utendaji. Ili kufikia lengo hilo
Serikali ilijiunga na Mpango wa Kimataifa wa uendeshaji wa Serikali kwa
Uwazi (Open Government Partnership) mwaka 2011. Tamko la Tanzania katika
kutelekeza matakwa ya ubia huu ni kuweka mazingira ya upatikanaji wa
taarifa kuhusu shughuli zinazofanywa na Serikali. Wizara yangu iliandaa
Rasimu ya Waraka wa Baraza la Mawaziri wa mapendekezo ya kutunga sheria
ya haki ya kupata taarifa kutoka katika taasisi za umma kwa lengo la
kuongeza uwazi na uwajibikaji wa Serikali.
22.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali nzuri ya utawala bora na kuzingatiwa
kwa haki za binadamu katika nchi yetu, hivi karibuni kumekuwa na tuhuma
nzito kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu. Tuhuma hizo zilitokana na
utekelezaji wa “Operesheni Tokomeza” ambayo ililenga kuwasaka na
kuwafikisha kwenye vyombo vya Sheria watu wote waliokuwa wanajihusisha
na vitendo vya ujangili katika hifadhi za taifa na mapori tengefu. Kwa
kuzingatia uzito wa tuhuma hizo Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya
Uchunguzi chini ya Sheria inayohusu uundwaji wa Tume za Uchunguzi
(Commissions of Inquiry Act, Cap. 32). Kuundwa kwa Tume hiyo
kulitangazwa katika Gazeti la Serikali na. 131 la tarehe 2 Mei, 2014.
Tume hiyo yenye makamishna watatu (3) imepewa hadidu za rejea ambazo ni:
(i) Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyofanyika;
(ii) Kuchunguza kama maofisa walioendesha Operesheni hiyo walifuata sheria, taratibu na hadidu za rejea walizopewa;
(iii) Kuchunguza endapo maofisa walioendesha Operesheni hiyo walivunja sheria, taratibu na hadidu za rejea zilizotolewa;
(iv)
Kuchunguza kama kuna watu waliovunja sheria wakati wa Operesheni hiyo
na kuona kama hatua walizochukuliwa wenyewe au mali zao zilikuwa sahihi;
(v)
Kushauri hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa mtu yeyote aliyevunja
sheria, taratibu na kwenda kinyume na hadidu za rejea zilizokuwepo
katika kutekeleza Operesheni hiyo;
(vi)
Kushauri mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kuandaa Operesheni
nyingine kama hiyo ili mambo yaliyojitokeza katika Operesheni hii
yasijirudie.
Kusikiliza na kuendesha mashauri nchini
23.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Dira ya upatikanaji haki kwa watu wote
na kwa wakati, Wizara yangu imeongeza kasi ya kuendesha na kusikiliza
mashauri yaliyosajiliwa Mahakamani. Kasi hiyo imetokana na mikakati
mbalimbali na malengo mahsusi ambayo Mahakama ya Tanzania imejiwekea ya
kusikiliza mashauri kwa ngazi zote za Mahakama. Utaratibu huu unaweka
wastani wa idadi ya mashauri yatakayosikilizwa na kila ngazi ya Mahakama
kwa kila mwaka. Katika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu lengo ni
kumaliza mashauri mapya ndani ya miezi 24, Mahakama ya Hakimu Mkazi
katika muda usiozidi miezi 18 na Mahakama ya Mwanzo kumaliza mashauri
mapya ndani ya miezi 12.
24.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu umesaidia kupunguza mlundikano wa
mashauri kwa kiasi kikubwa ambapo hadi kufikia Desemba, 2012 Mahakama ya
Tanzania ilikuwa na jumla ya mashauri 114,278 yaliyohusu masuala ya
madai, jinai na ardhi. Katika mwaka 2013 Mahakama ilisajili mashauri
mapya ya aina hiyo 168,068 na kufanya idadi ya mashauri yaliyokuwepo
kufikia 282,346. Hadi mwezi Desemba 2013 jumla ya mashauri 182,237
yalisikilizwa na kutolewa uamuzi, sawa na asilimia 65 ya mashauri yote
yaliyosajiliwa mahakamani. Mashauri yaliyobaki Mahakamani ni 100,109.
(Kiambatisho “A”).
25.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu umeanza kwa mafanikio ambapo hivi sasa
mashauri mengi yanayosajiliwa Mahakamani yamekuwa yakimalizika katika
kipindi kisichozidi miaka miwili. Wizara yangu itaendelea kubuni njia
mbalimbali zitakazosaidia kuondokana na tatizo la mlundikano wa mashauri
na ambalo linaathiri utoaji haki.
26.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inaratibu na kusimamia utekelezaji wa
mpango wa kutenganisha kazi ya upelelezi wa jinai na uendeshaji wa
mashtaka. Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni pamoja na
kupungua kwa tuhuma za wananchi za kubambikiziwa kesi katika Mahakama
ambazo Mawakili wa Serikali wanaendesha mashauri ya jinai na kupungua
kwa idadi ya wafungwa na mahabusu magerezani. Kabla ya kuanza kwa mpango
huu, mwaka 2007 kulikuwa na wafungwa 22,622 na mahabusu 20,210. Tangu
wakati huo idadi ya wafungwa na mahabusu imekuwa ikipungua kadri Wizara
inavyoendelea kueneza utekelezaji wa mpango huu katika mikoa na wilaya
mbalimbali. Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 idadi ya wafungwa
ilipungua kutoka 16,869 mwezi Juni 2013 hadi wafungwa 15,659 mwezi Machi
2014 na idadi ya mahabusu ilipungua kutoka 17,046 mwezi Juni 2013 na
kufikia mahabusu 16,647 mwezi Machi 2014.
27.
Mheshimiwa Spika, Kurugenzi ya Mashtaka pamoja na Mahakama ya Tanzania
zimeanza kutekeleza utaratibu maalum wa kukamilisha usikilizaji wa
mashauri 28 ya dawa za kulevya yaliyosajiliwa Mahakama Kuu. Mashauri
haya yamepangwa kusikilizwa katika kikao maalumu cha Mahakama Kuu
kitakachofanyika kuanzia mwezi Juni 2014. Mashauri 110 yapo Mahakama za
wilaya na mikoa kwa hatua za awali za kuyaandaa ili yahamishiwe Mahakama
Kuu kwa ajili ya kusikilizwa. Mashauri haya ni yale yenye thamani
inayoanzia shilingi milioni kumi na kuendelea.
28.
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na utekelezaji wa mkakati maalumu
wa kusikiliza mashauri 9 ya jinai ya wizi wa shilingi bilioni 29.8
zilizokuwa katika akaunti ya madeni ya nje (external payments arrears
account - EPA) iliyokuwa Benki Kuu. Hivi sasa Kurugenzi ya Mashtaka
inaendesha jumla ya mashauri 14 yanayotokana na makosa ya utakatishaji
wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 56 zilizopatikana kwa njia ya
uhalifu, na mashauri mengine 70 ya kukutwa na nyara za Serikali, zenye
thamani ya shilingi bilioni 45 kinyume cha sheria.
29.
Mheshimiwa Spika, kufikia mwezi Aprili 2014 kulikuwa na jumla ya
majalada 404 ya uchunguzi wa makosa mbalimbali ya rushwa
yaliyowasilishwa katika Kurugenzi ya Mashtaka kutoka TAKUKURU. Kati ya
hayo, majalada 202 yaliandaliwa hati za mashtaka, 103 yalirudishwa
TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi zaidi, na majalada 98 yanaendelea
kufanyiwa uchambuzi.
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara ikishirikiana
na taasisi mbalimbali iliongeza jitihada zake za kukabiliana na vitendo
viovu wanavyofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi. Jitihada hizi
zimechangia kiasi kikubwa kupungua kwa idadi ya matukio ya aina hii
katika kipindi cha Julai 2013 hadi Mei 2014, ambapo hakuna tukio lolote
lililoripotiwa Polisi. Hali hii ni tofauti na mwaka wa fedha 2012/2013
ambapo matukio matatu yaliripotiwa Polisi. Hivi sasa Wizara yangu
inaendelea na mashauri 9 ya aina hiyo yanayotokana na matukio ya miaka
ya nyuma.
31. Mheshimiwa
Spika, kuhusu mashauri ya ukiukwaji wa Haki za Binadamu, Wizara yangu
iliendesha mashauri 6 kwenye Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na
Watu iliyopo Arusha. Mashauri haya yanajumuisha mashauri 4 mapya ambayo
bado yanaendelea na mashauri 2 ambayo yametupiliwa mbali na Mahakama
hiyo kutokana na waombaji kutotimiza matakwa ya sheria.
32.
Mheshimiwa Spika, jumla ya mashauri ya madai ambayo Serikali ilishitaki
au kushitakiwa, na yale yanayohusu Katiba yaliyokuwa Mahakama Kuu,
Mahakama ya Rufani na katika mabaraza ya usuluhishi (mediation and
arbitration) katika kipindi cha Julai 2013 hadi Aprili 2014 ni 750.
Kati ya hayo mashauri yaliyosikilizwa na kutolewa uamuzi ni 89.
Serikali ilishinda mashauri 77 yenye thamani ya Shilingi
2,216,502,356,629 na kuokoa kiasi hicho cha fedha. Serikali ilishindwa
mashauri 12 yenye thamani ya Shilingi 25,986,416,661.
33.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali za kupambana na
vitendo vya uhalifu, bado kumekuwepo na matukio ambayo baadhi ya watu
wamejipatia mali kinyume cha sheria. Kwa kutambua hilo, Wizara yangu
imekuwa ikitenga fedha kwenye mipango yake ya mwaka kwa ajili ya kujenga
uwezo wa Kitengo cha utaifishaji na urejeshaji wa mali zilizopatikana
kwa njia ya uhalifu (Assets Recovery and Forfeiture Section). Kati ya
Julai 2013 na Machi 2014, Mahakama iliamuru kurejeshwa Serikalini jumla
ya mali na fedha zinazofikia thamani ya zaidi ya shilingi milioni 233
baada ya watuhumiwa kutiwa hatiani.
Kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria
34.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeboresha mazingira ya upatikanaji haki kwa
wananchi ikitambua kuwa uwakilishi mbele ya vyombo vya sheria ni haki ya
msingi. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014 Wizara iliandaa
Rasimu ya Waraka wa Kutunga Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria ili
kuwapa fursa wananchi kupata msaada wa kisheria. Rasimu ya Waraka huo
imewasilishwa Serikalini. Sheria hii itakapotungwa itawawezesha wananchi
wengi wasio na uwezo kupata ushauri na kuwakilishwa katika vyombo vya
sheria.
35. Mheshimiwa
Spika, wakati utaratibu wa kutunga sheria hii ukiwa unaendelea, Wizara
imeanzisha chombo cha mpito kijulikanacho kama Sekretarieti ya Msaada wa
Kisheria, ili kuratibu utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 jumla ya wananchi 12,809
walipata huduma ya msaada wa kisheria kupitia Sekretarieti hii.
Kuhakiki na kushiriki majadiliano ya mikataba mbalimbali
36.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mikataba, Wizara yangu imetoa ushauri
wa kisheria kwa Serikali unaozingatia ubora na weledi, na pia imeendelea
kushiriki katika majadiliano mbalimbali ya mikataba ya kibiashara,
mikutano ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa manufaa ya nchi. Katika
kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ilitekeleza jukumu hili kwa kushiriki katika mikutano ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika, Nchi za Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ulaya na Umoja wa Mataifa.
37.
Mheshimiwa Spika, ili kulinda maslahi ya nchi katika mikataba kati ya
Serikali na wadau mbalimbali, Serikali imefanya mabadiliko ya Sheria ya
Ununuzi (Public Procurement Act, 2011). Pamoja na mambo mengine, Sheria
hii inazitaka wizara, taasisi na idara za Serikali kupata ushauri wa
kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kufunga
mkataba wowote wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 50. Mabadiliko
haya yamechangia kuongezeka kwa mikataba inayowasilishwa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuhakikiwa, kutoka mikataba
120 mwaka 2013 hadi mikataba 375 kufikia Machi 2014. Hali hii imeiepusha
Serikali na mikataba isiyo na maslahi kwa taifa.
Uandishi wa sheria na hati za Serikali
38.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/2014, Wizara yangu iliandaa jumla
ya miswada 11 iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu kuwa
sheria. Miswada hiyo ilihusu: Sheria ya Fedha na Sheria ya Matumizi ya
Fedha inayopitishwa wakati wa Bunge la Bajeti; Sheria ya Taifa ya
Umwagiliaji; Sheria ya Vyama vya Ushirika; Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni. Miswada mingine ni
Sheria ya Mfuko wa Akiba ya Wafanyakazi Serikalini, Sheria ya Takwimu,
Sheria ya Marekebisho ya Ushuru na Bidhaa na Sheria ya Marekebisho ya
Sheria Mbalimbali (Na. 1) na (Na. 2). Aidha, Sheria Ndogo 136
zilitayarishwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali tayari kuanza
kutumika.
Kufanya utafiti na tafsiri ya sheria
39.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014, Tume ya
Kurekebisha Sheria ilifanya mapitio na utafiti wa mifumo ya sheria
mbalimbali. Utafiti wa kwanza ulihusu mfumo wa sheria wa utatuzi wa
migogoro ya ardhi. Utafiti huu umekamilika na Ripoti yake imekabidhiwa
kwa Waziri wa Katiba na Sheria. Ni azma ya Wizara yangu kuipitia Ripoti
hii kwa kushirikiana na Wizara nyingine zinazoshughulika na utatuzi wa
migogoro ya ardhi. Utafiti wa pili ulihusu mfumo wa sheria inayosimamia
huduma ya hifadhi ya jamii kwa wazee. Mwisho, Tume ilifanya utafiti
kuhusu sheria zinazolinda watumiaji wa bidhaa na huduma ili kubaini
upungufu uliopo.
40.
Mheshimiwa Spika, ufanisi katika utekelezaji wa sheria unategemea sana
uelewa wa wananchi kuhusu sheria hizo. Kwa kutambua hilo Wizara
imetafsiri Sheria 7 kutoka Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili. Wizara
itaendelea kutafsiri Sheria nyingi zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya
jamii na uwezo uliopo. Wizara inapenda kutoa mwito kwa wadau mbalimbali
ndani na nje ya Serikali kuchangia katika kuhamasisha wananchi kuwa na
mwamko wa kupenda kusoma na kuzifahamu sheria za nchi. (Kiambatisho
“B”).
41. Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara
yangu kwa kushirikiana na nchi wanachama imeendelea kufanya mapitio ya
Sheria zinazosimamia haki za ubunifu na haki miliki (Intellectual
property laws). Lengo ni kuhakikisha kuwa sheria za nchi wanachama
zinawiana na sheria za Jumuiya hiyo kama ambavyo nchi hizo
zimekubaliana katika kutekeleza Itifaki ya Soko la Pamoja.
Kuimarisha shughuli za Usajili, Ufilisi na Udhamini
42.
Mheshimiwa Spika, usajili wa matukio muhimu ya binadamu (vizazi, vifo,
ndoa, talaka na watoto wa kuasili) unalenga kulinda na kuhifadhi haki za
binadamu na za uraia. Aidha, usajili huu unaiwezesha Serikali kupata
takwimu sahihi kwa ajili ya mipango mbalimbali ya maendeleo. Katika
kipindi cha kuanzia Julai 2013 hadi Machi 2014 Wizara imeboresha mfumo
wa usajili wa vizazi kwa kusogeza huduma hii hadi ngazi za chini kama
vile kata na vituo vya tiba. Maboresho haya yamefanyika kupitia Mpango
wa usajili wa vizazi kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano
uliozinduliwa rasmi mkoani Mbeya mwezi Julai 2013.
43.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango huu umeongeza idadi ya watoto
wa umri chini ya miaka mitano waliopatiwa vyeti vya kuzaliwa kutoka
watoto 37,090 kabla ya mpango huu kuanza, hadi 169,477 Machi 2014. Hii
ni sawa na ongezeko la asilimia 31.4 la watoto wote wa umri wa chini ya
miaka mitano mkoani humo. Mbali na usajili huu mkoani Mbeya, Wizara
imefanya usajili wa kawaida katika sehemu nyingine za Tanzania bara wa
jumla ya vizazi 493,887, ndoa 14,031, talaka 53, vifo 34,460, na watoto
wa kuasili 30. Hali kadhalika jumla ya hati 182 za wadhamini wa vyama
vya siasa, makanisa, misikiti na mali za vikundi vya kijamii
zilisajiliwa. (Kiambatisho “C”)
Kuimarisha Taasisi za Mafunzo ya Sheria
44.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara imeimarisha
taasisi ya mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Chuo cha Uongozi wa
Mahakama. Hadi kufikia Machi 2014, jumla ya wanafunzi 293 walihitimu
mafunzo ya uanasheria kwa vitendo na kustahili kusajiliwa kuwa mawakili,
ikilinganishwa na mwaka 2012/2013 ambapo wahitimu walikuwa 272. Jumla
ya wanafunzi 896 walihitimu mafunzo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama,
kati ya hao wahitimu 267 walitunukiwa Stashahada ya Sheria na 629 Cheti
cha Sheria. Vile vile, Wizara imeanzisha Tawi la Chuo cha Uongozi wa
Mahakama katika jiji la Mwanza na kudahili wanafunzi 95 kwa mara ya
kwanza mwaka 2013/2014. Jitihada hizi zitaongeza idadi ya watalaam wenye
sifa za kuajiriwa katika fani mbalimbali za sheria.
Kuboresha miundombinu ya utoaji haki
45.
Mheshimiwa Spika, ubora wa huduma unaotolewa na taasisi za sheria
unategemea ubora wa mazingira na miundombinu ya utoaji haki. Kwa
kuzingatia umuhimu huo, katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014,
Wizara imefanya yafuatayo:-
• Imekarabati masijala kwenye Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Kanda za Dar es Salaam na Mtwara;
•
Imepata washauri elekezi kwa ajili ya kukarabati Mahakama za Mwanzo
10, na kujenga Mahakama za Mwanzo 25. Utaratibu wa kupata wakandarasi
umetangazwa kwenye magazeti ya tarehe 11 na 12 Mei 2014;
•
Imejenga uzio wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba; kutenga vyumba vya ofisi
za majaji na makatibu muhtasi; na kuziba sehemu ya wazi ya paa;
• Imeboresha masijala 71 za Mahakama za Mwanzo kwa kuziwekea mfumo wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za majalada;
• Imekamilisha ukarabati wa Mahakama za Mwanzo za Mgandu na Mwamagembe katika mkoa wa Singida;
• Inakamilisha ujenzi wa bweni la wanafunzi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama;
•
Imefungua ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mkoa wa Geita;
na inakamilisha taratibu za kuanza ukarabati wa Ofisi katika mikoa ya
Simiyu na Katavi;
• Imekamilisha ujenzi wa jengo la Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini;
•
Imekamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa mfumo mpana wa mawasiliano
(Wide Area Network) utakaounganisha Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Kurugenzi ya Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali mkoa ya Dar es Salaam.
46.
Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu kuhusu mradi wa e-justice
utakaorahisisha uendeshaji wa mashauri ya jinai umekamilika. Mradi huu
utaunganisha Mahakama, Magereza na Ofisi za mikoa za Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kwa njia ya mtandao. Ripoti ya zoezi hili imewasilishwa Ofisi
ya Rais -Tume ya Mipango na Wizara ya Fedha kwa hatua za maamuzi.
47.
Mheshimiwa Spika, Wizara imetumia fursa za maendeleo zinazotokana na
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuboresha huduma
zinazotolewa. Mahakama ya Tanzania imejiimarisha katika matumizi ya
TEHAMA kwa kuanzisha mfumo endelevu wa upatikanaji wa takwimu mbalimbali
za Mahakama. Mfumo huo umeanza kufanya kazi katika Mahakama ya Rufani,
Mahakama Kuu katika Divisheni za Biashara, Kazi na Ardhi, na Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Itakapofika Desemba 2014 Mahakama Kuu zote
nchini, mahakama za mikoa na mahakama zote za wilaya zitatumia TEHAMA
katika ukusanyaji na utunzaji wa takwimu.
48.
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini umeanzisha
utaratibu wa kupokea taarifa za usajili wa vizazi kupitia simu za
mkononi mara tu mtoto anaposajiliwa kwenye kata au kituo cha tiba. Hivi
sasa utaratibu huu unafanyika mkoani Mbeya kupitia mpango wa kusajili
watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano (U5BRI). Sambamba na hilo
mwananchi yeyote nchini anaweza akapata taarifa za huduma za RITA
kupitia simu za mkononi kwa kutuma neno RITA kwenda namba 15584 na
Tovuti ya Wakala (www.rita.go.tz).
Elimu kwa Umma
49.
Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua kuwa wananchi wana nafasi muhimu
katika kuimarisha utawala wa sheria, misingi ya haki za binadamu na
utawala bora. Kwa kuzingatia hilo, Wizara imetoa elimu kwa umma kwa njia
mbalimbali zikiwemo redio na luninga. Katika kipindi cha mwaka wa fedha
2013/2014 Wizara ilirusha vipindi 35 vya redio na vipindi 9 vya luninga
vilivyotoa elimu kuhusu mapambano na rushwa; haki za watoto na misingi
ya haki za binadamu na utawala bora. Vile vile, Wizara iliandaa mikutano
ya wadau katika mikoa ya Rukwa na Tanga kwa lengo la kuwajengea uelewa
wa sheria. Pia Wizara ilishiriki maonesho ambapo jumla ya vitabu 25,000
na vipeperushi 2,800 kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora
vilisambazwa. Katika mikutano hiyo, vitabu 500 na vipeperushi 1000
kuhusu historia ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na majukumu
ya Wizara vilisambazwa.
Uratibu na Utekelezaji wa Maboresho ya Sekta ya Sheria
50.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imetekeleza na kuratibu programu na
miradi mbalimbali ya kuboresha Sekta ya Sheria. Utekelezaji wa Programu
ya Maboresho ya Sekta ya Sheria unalenga kuimarisha mifumo ya utoaji
haki na kukuza uwezo wa taasisi za sheria katika kutoa huduma bora. Hadi
sasa Programu hii imewezesha, pamoja na mambo mengine, kutenganishwa
kwa shughuli za upelelezi na mashtaka, kufanya mapitio ya sheria
mbalimbali na kuanzishwa kwa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa
Vitendo.
51. Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, shughuli
nyingine muhimu za kuboresha sekta ya sheria zilizotekelezwa ni pamoja
na:- kufanya tathmini ya hali ilivyo sasa na kuishauri Serikali namna ya
kuendeleza maboresho katika sekta ya sheria; kuimarisha utendaji wa
Sekretarieti ya Huduma ya Msaada wa Kisheria; kuratibu uanzishwaji wa
maeneo ya kuhifadhi watoto waliokinzana na sheria ili kulinda haki zao,
na kuimarisha madawati ya jinsia na watoto katika vituo vya Polisi na
Magereza.
52.
Mheshimiwa Spika, maboresho ya sekta ya sheria ni pamoja na mapambano na
rushwa. Wizara yangu ni moja ya taasisi zinazotekeleza mradi wa
Uimarishaji wa Mapambano na Rushwa Tanzania (Strengthening Tanzania
Anti-Corruption Action - STACA) unaolenga kuziba mianya ya rushwa katika
taasisi zake. Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka wa fedha 2011/2012 na
unatarajia kukamilika mwaka 2014/2015. Kwa kipindi cha mwaka wa fedha
2013/2014 jumla ya pikipiki 214 zilinunuliwa kwa ajili ya Mahakimu wa
Mahakama za Mwanzo kwa nia ya kuondoa kero ya usafiri na kuongeza kasi
ya usikilizaji wa mashauri. Pia jumla ya masijala 68 za Mahakama za
Mwanzo ziliboreshwa kwa kuwekewa mfumo wa kielektroniki wa kutunza
kumbukumbu za majalada. Mfumo huo umerahisisha upatikanaji wa taarifa za
kimahakama na hivyo kuondoa mianya ya rushwa.
53.
Mheshimiwa Spika, kupitia mradi huu kitengo cha utaifishaji na
urejeshaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu (Assets Recovery
and Forfeiture Section) kimeimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi ambavyo
vimesambazwa katika ofisi za Mikoa na Wilaya za Mwanasheria Mkuu wa
Serikali. Vifaa hivyo ni kompyuta 35, mashine za uchapishaji, vitabu vya
rejea na samani za ofisi. Hali kadhalika mawakili 64 wa Serikali
wamepatiwa mafunzo kuhusu stadi za kuendesha mashauri ya rushwa na namna
ya kushughulikia mali zinazopatikana kwa njia ya rushwa. Kwa kuwa
Kurugenzi ya Mashtaka ni kiungo muhimu katika uendeshaji wa kesi na
upelelezi, Kurugenzi iliandaa mikutano ya kikazi na kiutendaji na wadau
mbalimbali chini ya Jukwaa la Haki Jinai. Vikao hivyo vilikuwa kati ya
Mawakili wa Serikali Wafawidhi, Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa na Vikosi
Tanzania Bara, TAKUKURU, Mkemia Mkuu wa Serikali, Idara ya Uhamiaji,
Idara ya Wanyamapori na Tume ya Uratibu wa Dawa za Kulevya. Lengo la
mikutano hiyo lilikuwa ni kuboresha uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka.
Ubia huu unasaidia kukusanya nguvu pamoja ili kuleta ufanisi zaidi
katika utendaji.
54.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu
ilichukua hatua za kuziimarisha Kamati za Maadili za Mahakama za mikoa
na wilaya. Tume ya Utumishi wa Mahakama ilifanya ukaguzi wa Kamati za
Maadili za Mahakama kwenye ngazi ya mkoa na wilaya katika mikoa ya
Iringa, Njombe na Ruvuma. Katika ukaguzi huo, Tume ya Utumishi wa
Mahakama ilibaini changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
fedha. Wizara imeanza kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuzipatia fedha
Kamati za Maadili za Mahakama ngazi za mikoa na wilaya. Katika mwaka wa
2013/14 jumla ya shilingi 36,000,000 zilitolewa kwa mikoa 18 na
shilingi 136,500,000 kwa wilaya 91.
Kwa
upande wa mawakili, Kamati ya Maadili ya Mawakili wa Kujitegemea
(Advocates’ Committee) ilishughulikia malalamiko 18 katika kipindi cha
Julai 2013 hadi Aprili 2014. Kati ya hayo, malalamiko 6 yamekwishatolewa
uamuzi.
55. Mheshimiwa
Spika, Wizara yangu imewajengea uwezo watumishi waliopo na kuajiri
watumishi wapya ili kuleta tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu
yake. Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi, 2014 Wizara iliajiri
watumishi wapya 541; ilipandisha vyeo watumishi 487; na kuwezesha
watumishi 1,081 wa kada mbalimbali kupata mafunzo ya muda mrefu na
mfupi ndani na nje ya nchi.
Utekelezaji wa masuala mtambuka
56.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria inazingatia masuala
mtambuka katika utekelezaji wa majukumu yake. Haya ni kama vile kuingiza
masuala ya jinsia katika sera, mipango na uendeshaji; kuzingatia
mahitaji ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI; na masuala yanayohusu
maadili. Kwa upande wa kuzingatia jinsia katika ajira jumla ya watumishi
541 waliajiriwa. Kati yao wanawake ni 241 (44.5%) na wanaume ni 300
(55.5%). Vile vile, jumla ya watumishi 487 walipandishwa vyeo ambapo
wanawake walikuwa 217 (44.56%) na wanaume walikuwa 270 (55.44%). Aidha,
jumla ya watumishi waliopata mafunzo ni 1,081 kati yao wanawake ni 588
(54%) na wanaume 493(46%) (Kiambatisho ”G”). Aidha, Wizara imeendelea
kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha watumishi wake wa kike na wa
kiume kuweka uwiano muafaka wa kutekeleza kazi zao na vilevile kumudu
majukumu ya uzazi na ulezi.
57.
Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya UKIMWI, watumishi wa Wizara
walipata mafunzo ya jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kupitia Kamati za UKIMWI zilizopo katika Wizara na taasisi zake.
Wizara inawahudumia watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI kwa
matibabu na lishe.
58.
Mheshimiwa Spika, kuhusu masuala ya maadili, mafunzo yametolewa kwa
watumishi 100 wa kada mbalimbali kutoka Kurugenzi ya Mashtaka kwa nia ya
kutoa uelewa wa masuala ya rushwa, kujenga maadili na uhusiano wenye
staha kazini.
MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2013/14
Ukusanyaji wa Maduhuli ya Serikali
59.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara yangu
ilipanga kukusanya jumla ya Shilingi 5,250,454,700 kama maduhuli ya
Serikali kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato. Hadi kufikia mwezi Machi
2014 Wizara ilikusanya jumla ya Shilingi 6,007,714,285, sawa na
asilimia 114 ya lengo. Tofauti hii inatokana na ongezeko la makusanyo ya
ada za wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na
maduhuli ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Mapato na Matumizi ya Fedha 2013/2014
60.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Wizara iliidhinishiwa
jumla ya Shilingi 260,656,733,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na
miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo Shilingi 205,397,547,000 ni
matumizi ya kawaida na Shilingi 55,259,186,000 ni fedha za miradi ya
maendeleo. Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi 42,537,099,000
ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi 162,860,448,000 ni kwa ajili ya
matumizi mengineyo. Kati ya fedha za matumizi ya maendeleo Shilingi
44,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 11,259,186,000 ni fedha za
nje.
61. Mheshimiwa
Spika, kufikia Machi 2014, Wizara imepokea kiasi cha Shilingi
120,363,046,912 sawa na asilimia 46 ya fedha zilizoidhinishwa. Kati ya
fedha hizo Shilingi 110,763,667,097 ni fedha za matumizi ya kawaida,
sawa na asilimia 54. Kati ya fedha hizi za matumizi ya kawaida, shilingi
36,312,510,030 ni mishahara ya watumishi; na Shilingi 74,451,157,067 ni
kwa ajili ya matumizi mengineyo. Fedha za maendeleo zilizopokelewa ni
Shilingi 9,599,379,815, sawa na asilimia 17 ya fedha zote za Maendeleo.
Kati ya fedha hizo, Shilingi 5,157,500,000 ni fedha za ndani na Shilingi
4,441,879,815 ni fedha za nje. Ufafanuzi wa taarifa hizi unapatikana
katika (Kiambatisho ”D”).
D. CHANGAMOTO ZILIZOPO
62.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio ambayo Wizara yangu imeyapata,
zipo changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa kutekeleza majukumu
yake. Changamoto hizi ni pamoja na:
• Bajeti ndogo inayotengwa ikilinganishwa na mahitaji halisi ya Wizara na taasisi zake;
•
Mapokezi ya fedha kidogo zilizoidhinishwa hayatabiriki na hivyo
kuifanya Wizara na taasisi zake kushindwa kutekeleza Mipango Kazi yao
kwa namna endelevu;
•
Wizara kutotengewa fedha za maendeleo za ndani kwa ajili ya ujenzi wa
ofisi na makaazi. Hali hii inazilazimu baadhi ya taasisi za Wizara
kutumia pesa nyingi kwa ajili ya kulipia kodi ya pango, na hivyo
kuathiri utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki na mazingira ya kazi;
•
Wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo kutopatiwa
mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kunachangia kuwepo kwa
malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanafunzi na kuathiri utulivu
masomoni;
• Uhaba wa vitendea kazi na rasilimali watu;
• Ongezeko la matukio ya makosa ya jinai pamoja na mbinu mpya za kutenda uhalifu;
•
Kuwepo kwa mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama wa majaji, mahakimu
na mawakili wa Serikali na hivyo kuathiri utendaji kazi wao; na
• Kuongezeka kwa mmonyoko wa maadili miongoni mwa baadhi ya watendaji wanaoshughulika na utoaji haki katika sekta ya sheria.
E. MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2014/2015
63.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara yangu
imepanga kuimarisha utekelezaji wa malengo mkakati iliyojiwekea ili
kutoa haki kwa watu wote na kwa wakati. Ili kufikia azma hiyo, Wizara
itasimamia na kufuatilia utekelezaji wa majukumu yake katika maeneo ya
kipaumbele yafuatayo:
i. Utekelezaji wa Katiba ya nchi na Sheria
a) Kufuatilia mchakato wa kutunga Katiba;
b) Kufanya maandalizi ya mapitio na marekebisho ya sheria zitakazoguswa na mabadiliko ya Katiba;
c) Kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi kuhusu taratibu za kimahakama zinazopaswa kuzingatiwa katika kudai haki;
d) Kushughulikia maswala ya urekebu wa Sheria;
e) Kushughulikia uandishi wa Miswada ya Sheria, Sera na Hati za Serikali;
f) Kuhakiki rasimu za mikataba ya Serikali na kushiriki katika majadiliano yanayohusu mikataba hiyo.
ii. Kusimamia na kufuatilia utoaji haki
a) Kusimamia shughuli za uendeshaji na usikilizaji wa mashauri;
b)
Kuziimarisha Kamati za Maadili za Mahakama katika ngazi ya mikoa na
wilaya kwa kuzipa mafunzo na kuzifanyia ukaguzi. Kazi hii itaanzia
katika mikoa ya Dodoma, Katavi, Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga,
Singida, Tabora;
c) Kuimarisha utekelezaji wa mpango wa kutenganisha shughuli za upelelezi na mashtaka.
iii. Kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria
a) Kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na kuendelezwa;
b)
Kuwasilisha Bungeni miswada mbalimbali inayohusu upatikanaji wa msaada
wa kisheria; kulinda mashahidi na waathirika wa vitendo vya jinai
(witness and victims of crime protection law); kulinda watu wanaotoa
taarifa kwa siri (whistle blowers) kuhusu vitendo vya uhalifu au vya
ukiukwaji wa maadili; marekebisho ya sheria ya usajili wa vizazi na
vifo; sheria ya ufilisi;
c) Kueneza mfumo wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga;
d) Kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa taasisi za mafunzo za Wizara.
iv. Kuimarisha miundombinu ya utoaji haki
a) Kujenga nyumba za majaji, majengo ya Mahakama na majengo ya Ofisi;
b) Kuimarisha huduma za masjala;
c) Kufunga mfumo wa kielektroniki wa e-justice kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri;
d) Kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa Taasisi za mafunzo za Wizara.
v. Kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa
a) Kupunguza mlundikano wa mashauri katika Mahakama zote;
b) Kuharakisha ufunguaji na uendeshaji wa mashauri;
c) Kufanya mapitio na utafiti wa sheria zinazohusu uwekezaji na biashara;
d) Kuhakiki mikataba mapema na kwa weledi.
vi. Utekelezaji wa Masuala Mtambuka
a)
Kuimarisha Kamati za Amani za Mikoa kupitia Kamati ya Kitaifa ya kuzuia
mauaji ya kimbari katika mikoa na wilaya. Vilevile, kutoa elimu na
hamasa kwa Wabunge, Wanahabari na wanafunzi wa vyuo vikuu ili kujenga
utamaduni wa amani na utangamano kwa kila Mtanzania;
b) Kuandaa na kuratibu awamu ya pili ya shughuli za maboresho ya Sekta ya Sheria;
c) Kuimarisha usimamizi wa maadili na uwajibikaji wa watumishi kazini.
64.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na changamoto zilizopo, Wizara yangu
imejizatiti kufanikisha malengo iliyojiwekea katika kutekeleza mpango na
bajeti kwa kipindi cha mwaka 2014/2015.
F. SHUKRANI
65.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wadau wetu
wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha
Sekta yetu ya Sheria. Kwa namna ya pekee napenda kushukuru nchi za
Canada, Denmark, Sweden, Uswisi na Uingereza kupitia Mashirika yao ya
Maendeleo ya CIDA, DANIDA, SIDA na DFID. Vilevile, nayashukuru Mashirika
na Taasisisi za Kimataifa zifuatazo: Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo
(UNDP) na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) katika kuchangia
maendeleo ya Sekta ya Sheria.
66.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za pekee kwa wadau mbalimbali
wa Sekta ya Sheria kwa ushirikiano na ushauri wao uliowezesha
kutekelezwa kwa majukumu ya Wizara kwa mwaka 2013/2014 kama
yalivyobainishwa katika hotuba hii. Ninapenda kumshukuru Mheshimiwa
Angellah Jasmine Kairuki (Mb), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu, Mheshimiwa Jaji Frederick
Mwita Werema, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Fakih A.R Jundu,
Jaji Kiongozi, Ndugu Fanuel E. Mbonde, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria, Ndugu Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, na Ndugu George Masaju, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
67.
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru Mheshimiwa Ignas Paul Kitusi,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. Eliezer M. Feleshi,
Mkurugenzi wa Mashtaka, Bi. Winifrida Korosso, Katibu Mtendaji wa Tume
ya Kurekebisha Sheria, Bibi. Mary Massay, Katibu Mtendaji Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Jaji Dkt. Gerald Ndika, Mkuu wa
Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, Mheshimiwa Jaji Ferdinand
Wambali, Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama, Ndugu Phillip Saliboko,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa RITA, Bibi Enzel William Mtei, Katibu
Msaidizi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Wakurugenzi wa Idara na
Taasisi zilizo chini ya Wizara yangu na Watumishi wote kwa ushirikiano
na kazi kubwa waliyoifanya katika kuandaa Mpango na Bajeti hii. Mwisho
nitoe shukurani kwa Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha
uchapishaji wa hotuba hii.
G. MAJUMUISHO
68.
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Sheria ina umuhimu wa pekee katika
kuchangia maendeleo ya nchi kiuchumi, kisiasa na kijamii. Wizara yangu
ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa inakuza na kuimarisha amani,
utawala wa sheria na haki za raia. Kwa kuzingatia dhana hii, napenda
kutoa mwito kwa wananchi wote pamoja na Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha
kuwa dhamira ya Serikali ya kulinda amani, utulivu na haki za binadamu
inazingatiwa na kupewa kipaumbele kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho.
H. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2014/2015
69.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa
katika mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara yangu inaomba kuidhinishiwa
kiasi cha Shilingi 231,372,948,000 kwa ajili ya Taasisi, Idara na
vitengo vyake. Kati ya fedha hizo, Shilingi 134,006,144,000 ni kwa ajili
ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 48,804,234,000 ni Mishahara. Fedha
za Maendeleo ni Shilingi 48,562,570,000, kati ya hizo Shilingi
44,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 4,562,570,000 ni fedha za
nje.
Fedha za Matumizi
70. Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa matumizi ya bajeti kwa Mafungu saba ya Wizara ni kama ifuatavyo:-
Fungu 12: Tume ya Utumishi wa Mahakama
Matumizi ya Mishahara Sh. 208,764,000
Matumizi Mengineyo Sh. 2,871,716,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo (nje) Sh. 0.0
Jumla Sh. 3,080,480,000
Fungu 16: Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Matumizi ya Mishahara Sh. 2,426,898,000
Matumizi Mengineyo Sh. 8,332,865,000
Matumizi ya Maendeleo
(Ndani) Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh. 457,149,000
Jumla Sh. 11,216,912,000
Fungu 35: Kurugenzi ya Mashtaka
Matumizi ya Mishahara- Sh. 5,215,201,000
Matumizi Mengineyo Sh. 16,460,826,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh. 468,299,000 Jumla Sh. 22,144,326,000
Fungu 40: Mfuko wa Mahakama
Matumizi ya Mishahara Sh. 35,040,061,000
Matumizi Mengineyo Sh. 89,660,284,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) Sh. 40,000,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(nje) Sh. 1,687,748,000
Jumla Sh. 166,388,093,000
Fungu 41: Wizara ya Katiba na Sheria
Matumizi ya Mishahara Sh. 3,154,642,000
Matumizi Mengineyo Sh. 8,028,651,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 4,000,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(nje) - Sh. 1,048,621,000
Jumla - Sh. 16,231,914,000
Fungu 55:Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Matumizi ya Mishahara Sh. 2,041,593,000
Matumizi Mengineyo Sh. 4,795,802,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) - Sh. 900,753,000
Jumla - Sh. 7,738,148,000
Fungu 59: Tume ya Kurekebisha Sheria
Matumizi ya Mishahara Sh. 717,075,000
Matumizi Mengineyo Sh. 3,856,000,000
Matumizi ya Maendeleo
(ndani) - Sh. 0.0
Matumizi ya Maendeleo
(nje) - Sh. 0.0
Jumla - Sh. 4,573,075,000
Makusanyo ya Maduhuli ya Serikali
71.
Mheshimwa Spika, kwa mwaka 2014/2015 Wizara yangu inatarajia kukusanya
kiasi cha Shilingi 8,577,362,121 kama maduhuli ya Serikali, kama
ifuatavyo:-
Fungu 12: Tume ya Utumishi wa Mahakama Sh. 0.0
Fungu 16: Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Sh. 4,502,000
Fungu35: Kurugenzi ya Mashitaka Sh. 17,103,000
Fungu 40: Mfuko wa Mahakama Sh. 4,115,843,000
Fungu 41: Wizara ya Katiba na Sheria Sh. 4,434,270,121
Fungu 55: Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sh. 5,644,000
Fungu 59: Tume ya Kurekebisha Sheria Sh. 0.0
JUMLA Sh. 8,577,362,121
72. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Kiambatisho “A” Kiambatisho “B”SHERIA ZILIZOTAFSIRIWA KUTOKA LUGHA YA KIINGEREZA KWENDA KISWAHILINa. SHERIA YA KIINGEREZA SHERIA YA KISWAHILI1. The Local Government (District Authorities), Act, Cap.287 Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 2872. The Local Government (Urban Authorities), Act, Cap.288 Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 2883. The Local Government (Finance), Act, Cap.290 Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura ya 2904. The Local Government Authorities (Decoration of Buildings), Act, Cap.293 Sheria ya Serikali za Mitaa (Upambaji wa Majengo), Sura ya 2935. The Urban Planning Act, Cap.355 Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 3556. The Law of the Child Act, Cap.13 Sheria ya Mtoto, Sura ya 137. The Judicial Services Act, Cap.237 Sheria ya Utumishi wa Mahakama, Sura ya 237 Kiambatisho “C”: Usajili wa Matukio-RITAMwaka Vizazi Vifo Ndoa Talaka Udhamini Wosia Mirathi Kuasili2009/2010 469,274 47,118 17,106 85 277 83 13 462010/2011 625,670 73,810 23,108 69 203 36 14 332011/2012 519,511 66,463 13,631 51 204 33 2 182012/2013 511,160 80,239 14,477 66 213 52 2 272013/2014 493,887 34,460 14,031 53 182 24 3 30 Kiambatisho “D1”UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA, 2013/2014BAJETI YA MATUMIZI MENGINEYO BAJETI YA MISHAHARAFungu Maelezo Bajeti ya OC iliyoidhinishwa 2013/2014 Julai-Machi 2014 Julai-Machi 2014 Bajeti ya Mishahara iliyoidhinishwa 2013/2014 Julai-Machi 2014 Julai-Machi 2014 Bajeti iliyopangwa Fedha iliyotolewa % Bajeti iliyopangwa Fedha iliyotolewa8 TUME YA MABADILIKO YA KATIBA 33,944,588,000 - 16,440,720,746 48% - - - 12 TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA 2,871,716,000 2,489,256,000 1,057,594,391 37% 161,882,000 139,225,600.00 139,225,600.00 16 OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI 8,332,865,000 5,794,614,500 2,905,557,820 35% 2,174,186,000 1,630,630,500.00 1,839,657,420.00 35 MKURUGENZI WA MASHTAKA 16,460,826,000 14,342,929,262 4,240,860,800 26% 4,383,211,000 3,137,675,250.00 3,853,201,900.00 40 MAHAKAMA 86,600,000,000 64,950,000,000 45,453,980,625 52% 30,980,157,000 25,817,000,000.00 26,579,502,895.00 41 WIZARA YA KATIBA NA SHERIA 8,028,651,000 7,069,331,500 2,355,175,821 29% 2,447,110,000 2,002,393,557.90 2,002,393,557.90 55 TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA 3,795,802,000 2,891,649,957 1,179,908,931 31% 1,814,993,000 1,385,794,386.77 1,382,791,762.37 59 TUME YA KUREKEBISHA SHERIA 2,856,000,000 2,142,000,000 817,357,933 29% 575,560,000 515,736,895.00 515,736,895.00 JUMLA 162,890,448,000 99,679,781,219 74,451,157,067 42,537,099,000.00 34,628,456,189.67 36,312,510,030.27 Kiambatisho “D2”UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MIRADI YA MAENDELEOFungu Maelezo Fedha iliyoidhinishwa Fedha iliyotolewa Fedha iliyobaki Ndani Nje Ndani % Nje % Ndani Nje8 TUME YA MABADILIKO YA KATIBA - - - 0% - 0% - - 12 TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA - - - 0% - 0% - - 16 MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI - 826,000,000 - 0% - 0% - 826,000,000 35 MKURUGENZI WA MASHTAKA - 2,167,759,000 - 0% 1,312,542,840 61% - 855,216,160 40 MAHAKAMA 40,000,000,000 2,716,068,000 5,000,000,000 13% 508,842,840 19% 35,000,000,000 2,207,225,160 41 WIZARA YA KATIBA NA SHERIA 4,000,000,000 3,898,840,000 157,500,000 4% 1,849,600,000 47% 3,842,500,000 2,049,240,000 55 TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA - 1,034,169,000 - 0% 770,894,135 75% - 263,274,865 59 TUME YA KUREKEBISHA SHERIA - 616,350,000 - 0% 0% - 616,350,000 JUMLA 44,000,000,000 11,259,186,000 5,157,500,000 4,441,879,815 38,842,500,000 6,817,306,185 Kiambatisho “E”Makadirio Halisi v. Makadirio ya Ukomo wa Bajeti 2014/2015 Mahitaji Halisi (TSh) Ukomo wa Bajeti (TSh) Upungufu (TSh) Mahitaji Halisi (TSh) Ukomo wa Bajeti (TSh) Upungufu (TSh)Fungu Maelezo Matumizi Mengineyo Matumizi Mengineyo Matumizi Mengineyo Maendeleo Ndani Maendeleo Ndani Maendeleo Ndani12 Tume ya Utumishi wa Mahakama 4,341,738,000 2,871,716,000 1,470,022,000 0 0 016 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali 13,400,000,000 8,332,865,000 5,067,135,000 50,000,000,000 0 50,000,000,00035 Kurugenzi ya Mashtaka 28,300,000,000 16,460,826,000 11,839,174,000 0 0 040 Mahakama ya Tanzania 116,000,000,000 89,660,284,000 26,339,716,000 100,000,000,000 40,000,000,000 60,000,000,00041 Wizara ya Katiba na Sheria 11,600,000,000 8,028,651,000 3,571,349,000 4,000,000,000 4,000,000,000 055 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora 9,500,000,000 4,795,802,000 4,704,198,000 0 0 059 Tume ya Kurekebisha Sheria 4,850,000,000 3,856,000,000 994,000,000 780,000,000 0 780,000,000JUMLA 187,991,738,000134,006,144,00053,985,594,000154,780,000,00044,000,000,000110,780,000,000Kiambatisho “F”BAJETI ILIYOIDHINISHWA 2013/2014 NA MAKADIRIO YA 2014/2015Fungu Maelezo Bajeti ya Matumizi Mengineyo Bajeti ya Mishahara Bajeti ya Miradi ya Maendeleo Jumla ya Bajeti ya 2014/2015 Kiasi Kilichoidhinishwa 2013/2014 Makadirio ya 2014/2015 Kiasi Kilichoidhinishwa 2013/2014 Makadirio ya 2014/2015 Kiasi Kilichoidhinishwa 2013/2014 Makadirio ya 2014/2015 Nje Ndani Nje Ndani 8 Tume ya Mabadiliko ya Katiba 33,944,588,000 - - - - - - - - 12 Tume ya Utumishi wa Mahakama 2,871,716,000 2,871,716,000 161,882,000 208,764,000 - - - - 3,080,480,000 16 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali 8,332,865,000 8,332,865,000 2,174,186,000 2,426,898,000 826,000,000 - 457,149,000 - 11,216,912,000 35 Kurugenzi ya Mashtaka 16,460,826,000 16,460,826,000 4,383,211,000 5,215,201,000 2,167,759,000 - 468,299,000 - 22,144,326,000 40 Mahakama 86,600,000,000 89,660,284,000 30,980,157,000 35,040,061,000 2,716,068,000 40,000,000,000 1,687,748,000 40,000,000,000 166,388,093,000 41 Wizara ya Katiba na Sheria 8,028,651,000 8,028,651,000 2,447,110,000 3,154,642,000 3,898,840,000 4,000,000,000 1,048,621,000 4,000,000,000 16,231,914,000 55 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora 3,765,802,000 4,795,802,000 1,814,993,000 2,041,593,000 1,034,169,000 - 900,753,000 - 7,738,148,000 59 Tume ya Kurekebisha Sheria 2,856,000,000 3,856,000,000 575,560,000 717,075,000 616,350,000 - - - 4,573,075,000 Jumla 162,860,448,000 134,006,144,000 42,537,099,000 48,804,234,000 11,259,186,000 44,000,000,000 4,562,570,000 44,000,000,000 231,372,948,000 Kiambatisho “G” TAKWIMU ZA WATUMISHI WALIOHUDHURIA MAFUNZO TAASISI 2009/2010 2010/2011 2011/2012 2012/2013 2013/2014 Jumla ME KE ME KE ME KE ME KE ME KE Wizara ya Katiba na Sheria 10 14 10 13 5 10 21 15 5 8 111Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali 261 164 77 56 156 86 76 103 62 97 1138Tume ya Utumishi wa Mahakama 4 4 8 7 8 6 9 11 7 9 73Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora 11 12 8 8 3 4 12 13 10 11 92Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) 0 0 0 0 0 0 48 23 46 18 135Tume ya Kurekebisha Sheria 14 19 9 10 0 6 11 5 9 5 88Mahakama ya Biashara 14 8 1 3 5 9 0 0 0 0 40Mahakama ya Ardhi 13 11 17 18 7 5 0 0 0 0 71Mahakama ya Kazi 10 8 8 4 6 5 0 0 0 0 41Mahakama 206 145 297 141 26 41 453 449 595 449 2802Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) 0 0 0 0 0 0 5 3 2 1 11Jumla 5433854352602161726356227365984602
SOMA HOTUBA YA BAJETI YA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA DKT ASHA-ROSE MIGIRO KWA MWAKA 2014/2015
Reviewed by
Unknown
on
1:37 AM
Rating:
5